Dkt. Bashiru Ally:

Katibu Mkuu wa CCM, Dkt. Bashiru Ali amesema viongozi wote wa chama hicho, wanatakiwa kukutana na wananchi kwenye maeneo wanayoongoza, kusikiliza kero zao na kuzipatia ufumbuzi mapema iwezekanavyo.

Amesema hata Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli amekuwa akisikiliza kero za watu katika sekta walizomo na kuzipatia ufumbuzi papo kwa apo au baadaye hali ambayo imeleta mwamko wa kisiasa kwa wananchi.

Amesema Rais, Dkt. Magufuli amegeuza hali ya kisiasa na mtindo wa uongozi wa kisiasa nchini, ambao unatakiwa kufafanuliwa na kila mwana CCM.

“Kufuata mkondo huo wa siasa ni kazi ngumu sana, sana, ni kazi ya wana CCM wote kufafanua kuwa siasa yetu ni Siasa ya Ujamaa,” amesema Dkt. Bashiru na kuendelea,

Mkiniona nafanya ziara, mkimuona waziri mkuu na mawaziri wengine wanafanya ziara maeneo tofauti nchini, mfahamu tunatekeleza majukumu hayo…,hata wabunge na madiwani lazima wafanye ziara,wasiofanya wanajua hatima yao itakuwaje.”

Dkt. Bashiri akizungumzia Ujamaa amesema maana yake ni kuamini kwamba binadamu wote ni sawa na kila binadamu anastahili heshima ya utu wake.

“Kwamba nchi hii tutaijenga sisi kwa jasho letu kwa njia ya kujitegemea, Kwamba ni lazima tujilishe kwakuwa hakuna mjomba wa kutulisha, kwamba watoto wetu lazima tuwasomeshe, bila kujali hali ya uchumi wa wazazi wao,”amesema na kuendelea,

“Kwamba tugawane keki ya taifa kwa usawa na kama tunatekeleza miradi ya umeme, tupange mipango hiyo ya miradi ya umeme kwa uwiano, tugawane kidogokidogo.”

Dkt. Bashiru amesema hakuna atakayeachwa nyuma, kila kata, kila jimbo litaeleza limefanya nini katika kipindi cha miaka mitano kwa habari ya umeme,madaraja, barabara, madarasa, maji afya na hata masoko ya mazao.

Ingawa kila chama cha siasa kinaposajili hutakiwa kukiri kuzingatia misingi ya utaifa, ikiwemo msingi unaojali utu, haki na usawa, Dkt. Bashiru amesema CCM ndicho kimejipambanua kuzingatia msingi huo na kufanya siasa yenye demokrasia ya ushirika.

Kwa mfumo huo, amesema wanajenga utamaduni wa uongozi unaojali kero za wanyonge, unaoshirikisha, unaobuni mikakati ya kutatua kero na changamoto zilizopo.

“Na kwa kufanya hivyo tutakuwa tunabadilishana uongozi kwa amani, hatutakuwa na mbunge wa kuduma wala rais wa kudumu, tutakuwa na wabunge, rais watakaochaguliwa kwa ridhaa ya wananchi,” amesema Dkt. Bashiru.

Amezungumza hayo akiwa ziarani, alipokutana na viongozi, wanachama wa chama hicho kuanzia ngazi ya  vitongoji, mashina, kata na Wilaya ya Meatu, mkoani Simiyu.


Itaendelea…
Na Editha Majura.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: