Serikali Mkoani Iringa, imewaomba wafanyabiashara wenyeji wa Mkoa wa Iringa kurudi kuwekeza nyumbani kwa kuwa sasa usafiri utakuwa rahisi na wa uhakika.

Ombi hilo limetolewa na Mkuu wa mkoa huo, Ally Hapi, baada ya Shirika la Ndege Nchini (ATCL) kutangaza kuanza safari za ndege za shirika hilo katika kiwanja cha ndege cha Iringa kuanzia April 29, mwaka huu.

Mwaka jana serikali ilitangaza kukarabati viwanja vya ndege nchini kikiwamo kiwanja cha ndege cha Iringa ambapo mkuu huyo wa mkoa aliishukuru serikali na wadau walioshirikiana kujenga miundombinu ya kiwanja hicho.

Kiwanja hicho kimekarabatiwa njia ya kuruka na kutua ndege pamoja na kujenga majengo mawili ya abiria wanaoingia na kutoka katika kiwanja hicho, na kuwaomba wawekezaji kutumia fursa hiyo kuwekeza katika sekta mbalimbali mkoani hapo ikiwamo ya utalii.

Hapi alisema kuwa jengo peke yake na kuweka mitambo fedha za wadau umegharimu zaidi ya Sh.milioni 400.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa ATCL,  Ladislaus Matindi, alitangaza neema hiyo kwa wasafiri wanaotumia kiwanja cha ndege cha Iringa na kusema kwamba gharama za usafiri wa ndege zitashuka kutoka Sh. 1,000,000 kwa safari ya kwenda na kurudi hadi kufikia Sh. 280,000.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: