Na Jeshi la Polisi.
Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Simon Sirro amewaomba Viongozi wa dini nchini kuendelea kufanya doria za kiroho huku Jeshi hilo likiendeleza doria za kimwili kwa pamoja ili kuukabili uhalifu ikiwemo mauaji yanayosababishwa na wivu wa mapenzi ambayo yameanza kuongezeka katika siku za hivi karibuni.
IGP Sirro ameyasema hayo kwa nyakati tofauti katika Wilaya za Ukerewe na Sengerema mkoani Mwanza wakati wa Ziara yake inayoendelea katika Mikoa ya Kanda ya Ziwa yenye lengo la kubaini changamoto za kiuhalifu na kuzipatia ufumbuzi wa haraka ili wananchi waendelee kufanya kazi zao kwa Amani na utulivu.
Amesema Polisi wanafanya doria za kimwili ambazo wakati mwingine hutumia nguvu kushurutisha watu kutii sheria lakini Viongozi wa dini nao wana nafasi yao katika jamii kwa kufanya doria za kiroho na kukemea maovu.
IGP Sirro amesema makosa ya mauaji yanayosababishwa na wivu wa mapenzi yameanza kujitokeza kwa kasi katika siku za karibuni hivyo viongozi wa dini wana nafasi kubwa zaidi kuwaelimisha waumini wao kabla vifo havijatokea kwa kuwa wengi wao wanakuwa nao kila siku za ibada.
Katika hatua nyingine IGP Sirro ameahidi kuchangia Shilingi milioni kumi na tano ili kusaidia ujenzi wa kituo cha Polisi katika Kisiwa cha Kome, Wilayani Sengerema baada ya Wananchi kuomba kujengewa kituo hicho ili kukabiliana na uhalifu.
Wakizungumza katika mkutano wa hadhara Kisiwani Kome Wananchi hao walisema kujengwa kwa kituo hicho kutasaidia kuimarisha usalam katika maeneo hayo huku wakiomba kufufuliwa kwa Vikundi vya Ulinzi Shirikishi.
IGP anaendelea na ziara yake huku akitumia usafiri wa Helkopta ili kujionea kwa uhalisia maeneo hayo ili kuweza kuzipatia ufumbuzi changamoto za uhalifu.
Post A Comment: