MAONI YA DAVID KAFULILA KUHUSU RIPOTI YA CAG NA MSIMAMO WA ACT.
1.    Baada ya Chama Cha ACT kutoa tamko lao kwa kina Jana kuhusu Ripoti ya CAG kwa hesabu za 2016/17, nimeulizwa na wadau wengi kuhusu maoni yangu kufuatia tamko hilo wakihusianisha na msimamo wangu  kwamba serikali ya awamu ya tano ni tofauti sana na hivyo kutaka kunisikia maoni yangu kufuatia kilichoitwa madudu yaliyobainishwa katika uchambuzi wa chama cha ACT kuhusu serikali hii kwa mujibu wa ripoti hiyo.

Kwanza niwapongeze  ACT kwa kuunguza bongo hata kutoka na tamko lililosababisha mjadala wa masuala muhimu kwa Taifa. Binafsi naamini kwamba Ripoti za CAG ni kioo kwa Serikali na Mamlaka zake,nakwasasa ni kioo kwa vyama vya siasa pia, ndio sababu serikali huzipa uzito wa kipekee kwa kuchukua hatua haraka na hivyo kutoa somo kwa vyama vya siasa kufanya hivyo pia.Hivyo nawapongeza ACT kuipa joto hoja ya CAG ili tujadili na kubadilishana mawazo kwa maslahi ya Taifa.

Katika hoja ya 7, ACT wanasema ” Kwa ujumla Serikali imepata hati Chafu.Taarifa ya CAG ya ukaguzi wa kwanza wa makusanyo na matumizi ya kibajeti ya Serikali ya awamu ya tano, imeonesha kuwa , kwa ujumla , Serikali ya Jamhuri ya Muungano imepata hati Chafu , kwakuwa Hesabu Jumuifu za Taifa ( Consolidated Accounts ) zimepata Hati ISIYORIDHISHA ( Chafu).”

UKWELI nikwamba  Nimesoma Ripoti hiyo yenye kurasa 434, sikukuta mahala CAG ameandika kwa kigezo chochote kwamba Serikali kwa ujumla imepata hati Chafu.Nikajaribu kusoma mijadala kutafuta nani ameweza kutoa Rejea ya ni wapi CAG kasema hilo, nikakuta kwenye mjadala wa Jamiiforum, Kiongozi Mkuu wa ACT amemjibu mmoja wa waliotaka kujua ni wapi CAG kasema kwa ujumla Serikali imepata hati Chafu, katibu majibu yake, Kiongozi huyo katika majibu yake kwenye mjadala huo muda(8:09PM)  ameandika kwamba CAG amesema hilo kwenye ukurasa wa

 298. NIMERUDIA KUSOMA UKURASA HUO NENO KWA NENO HAKUNA  KITU HICHO. Ukurasa huo umeleza mapungufu ya hesabu, lakini hakuna maneno ambayo ACT inataka kuaminisha Umma kuwa yametajwa na CAG.

Inawezekana ACT baada ya kusoma maelezo hayo wakahitimisha kwamba Serikali kwa ujumla imepata hati Chafu.Hata hivyo, Mwenye Mamlaka ya kuamua madaraja ya Hati si Mwingine bali CAG kwa kuzingatia viwango vya Kimataifa vya Ukaguzi wa Taasisi za Umma( ISSAIs) na Bodi ya Kimataifa ya Maadili kwa kanuni za Maadili ya wahasibu ( Kanuni ya IESBA). Hivyo sio mtu yeyote au chama au taasisi inamamlaka ya kusoma hesabu na kuzipangia daraja la Hati kama ACT wanavyotaka kufanya. Ni kwa msingi huo maneno kwamba Serikali imepata hati Chafu yanabaki kuwa kwa mujibu wa chama cha ACT na sio CAG .

2. Kwenye hoja 1, ACT wanasema Mawaziri wanafanya makosa kujibu hoja za CAG kwa waandishi wa habari na kwamba sheria ya Ukaguzi wa Umma kifungu38(1)&(2) kinaeleza Maafisa Masuuli/ Makatibu Wakuu  ndio wanapaswa kujibu hoja zilizoibuliwa na CAG tena mbele ya Kamati ya PAC&LAAC.

UKWELI Nikwamba Mawaziri wangejibu hoja za CAG mbele ya Kamati za PAC& LAAC wangekuwa wamevunja Sheria hiyo, lakini Mawaziri kueleza Waandishi wa Habari maoni yao au hatua wamezokwisha kuchukua  kuhusu Ripoti ya CAG haijakatazwa popote kwenye sheria hiyo kwani wanahabari sio kamati ya PAC wala LAAC kama ilivyotajwa katika sheria hiyo.Ndio sababu tamko hilo hilo la ACT, pamoja na kujua kwamba Ripoti hiyo haijaanza kufanyiwa kazi na Kamati za PAC& LAAC ,  ACT wamepongeza Serikali kuanza kuchukua hatua hadharani kufuatia Ripoti hiyo. Hivyo walichokipongeza ndicho wanachokihoji tena kwenye tamko hilo hilo.

3.Kuhusu kinachoitwa upotevu wa 1.5trilioni. Kwa mujibu wa ACT nikwamba kwakuwa kwenye ukaguzi wa matumizi imeonekana kiasi kilichotolewa ni trilioni 23.8..wakati kwenye makusanyo kilichopatikana ni trilioni 25.3 .hivyo kuna upotevu wa 1.5trilioni.

UKWELI ni kwamba kwamba ACT ilipaswa kuweka hoja hii katika mfumo wa swali badala ya kuhitimisha kwani hata CAG hakuna mahala amehitimisha  kuwa kuna upotevu wa trilioni1.5. Nasema walipaswa kuuliza kwasababu Mimi baada ya kusoma Hotuba ya Bajeti 2017/18, kwenye eneo la Mapitio ya Bajeti ya 2016/17 ambayo ndio hesabu zake zimekaguliwa, Waziri wa Fedha kwenye Hotuba yake alibainisha wazi kwenye Paragrafu ya 2 kipengele cha mapitio ya matumizi  kwamba Kati ya Pesa za miradi ya maendeleo kutoka nje( trilioni trilioni 3.047).Kuna kiasi cha Pesa hizo   Matumizi yake hayakupitia mfumo wa malipo wa Serikali baada ya baadhi ya washirika wa maendeleo kuzipeleka moja kwa moja kwenye miradi.

Nanukuuu ” Hata hivyo ,baadhi ya fedha za nje za kugharimia miradi ya Maendeleo hazikujumuishwa kwenye matumizi  kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo kuchelewa kupata thamani halisi ya vifaa vilivyopelekwa moja kwa moja kwenye miradi kutokana na baadhi ya washirika wa Maendeleo kuendelea kupeleka fedha moja kwa moja bila kupitia mfumo wa malipo wa Serikali”

Katika msingi huo ni wazi fedha ambazo hazikutolewa kupitia mfumo wa malipo wa Serikali CAG asingeweza kuziona na hivyo kujitokeza kwa tofauti ya makusanyo na fedha iliyolipwa sio jambo la kushangaza katika mazingira hayo.Najua Serikali inaweza kueleza hili kwa takwimu zaidi.

4.    Hoja kwamba Serikali imetekeleza Bajeti kwa asilimia 68% huku Bajeti ya Serikali za mitaa ikitekelezwa kwa asilimia 51ni utekelezaji hafifu nadhani ingekuwa vema kama ACT wangefanya ulinganisho.waseme kiasi hicho ni kidogo kulinganisha na miaka gani. Kwani navyojua miaka michache iliyopita Bajeti ya Serikali za mitaa ilitekelezwa mpaka kwa asilimia35%.
Hivyo utekelezaji huu wa asilimia 51 % ni hatua kubwa  hata kama haitoshi kwakuwa haijafika asilimia100%.

5. Kwamba  ACT wanasema Madeni ya nyuma yaliyolipwa bila idhini ya bunge ni madeni hewa, Nadhani ACT wangetafuta msamiati tofauti kwani madeni hewa ni Yale yasiyokuwepo, lakini kama yamehakikiwa kuwa ni madeni halali hayawezi kuitwa madeni hewa.

6. Kwamba CAG hakukagua ATCL hivyo nikasoro kwa CAG,  nadhani ibaki kama walivyoshauri kwamba ukaguzi ujao CAG aone haja ya kukagua lakini huwezi kumlaumu kutokagua kwa hoja tu manunuzi ya ndege yalifanyika katika mwaka huo wa fedha uliokaguliwa 2016/17 kwani hakuna mwaka CAG alikagua mashirika yote. laiti ingekuwa yamekaguliwa mashirika yote likaachwa ATCL kulikuwa na uhalali wa kuhoji kulikoni.

7. Hoja kwamba Matumizi ya Serikali yanapangwa na Ikulu siku hizi badala ya Serikali ni tuhuma nzito, ingawa kwakuwa wameitoa bila uthibitisho wowote ni ngumu kwa mtu makini kuipa uzito sawia na hivyo  inakosa uzito na kuonekana kama vijembe vya kisiasa tu.
8. Hoja kwamba namna serikali inavyokopa ndani kupitia minada ya dhamana za Serikali inasababisha Benki za biashara kuvutiwa zaidi kuikopesha serikali badala ya sekta binafsi na hivyo kufanya biashara isichangamke ni hoja inayohitaji mjadala mpana.

Nasema hivyo kwasababu kwenye awamu ya nne tulilalamika kwamba Serikali ilikuwa inakopa ndani kwa mfumo huo  lakini kwa riba juu sana mpaka zaidi ya asilimia17% mwaka 2015  kwa TBs za Sik182&365 na hivyo hoja ikawa ni kwamba Benki zinapoteza hamu ya kukopesha sekta binafsi na hata kuongeza riba zaidi kwa kulinganisha na riba ambayo Benki huvuna inapoikopesha serikali( kwasababu Benki zinajua Serikali ni Risk free).

Ni kwasababu hiyo tukawa tunajenga hoja bungeni serikali isikope kwa riba ya juu katika masoko ya dhamana ili Benki za biashara ziwe na hamu ya kukopesha sekta binafsi na kwa riba nafuu.

Kitu ambacho Serikali hii imetekeleza, kwamba kwasasa Serikali inakopa kwenye mfumo huo wa TBs kwa riba ya asilimia 5% kwa TBs za siku365 na riba ya  kwa TBs za siku182.Hii inathibitisha wazi dhamira ya serikali kutozivutia Benki za biashara ziikopeshe n badala yake zijielekeze kwenye sekta binafsi kwani riba zinayopata sasa kwa kuikopesha Serikali ni pungufu kwa zaidi ya asilimia 300% kulinganisha na mwaka 2015.

9. Mwisho nihitimishe kwa kuipongeza Serikali kwa namna  imevyofanikiwa kutekeleza kilichokuwa kilio cha Bunge la 9&10 kuhusu misamaha ya kodi ambapo kwa miaka10 mabunge hayo yalipigania misamaha ishuke mpaka asilimia1% ya pato la Taifa ikitolewa mifano ya nchi wanachama Afrika Mashariki kama kigezo( misamaha yake ilikuwa asilimia1% ya Pato la Taifa). Miaka miwili yote ya Serikali hii, misamaha ya kodi ni asilimia1% kutoka asilimia2 % mpaka asilimia3% ya pato la Taifa kabla ya awamu hii( Kwa mujibu wa Ripoti hii ya CAG).

Aidha ufanisi wa TRA katika kukusanya kodi tangu mwaka 2016 upo juu kuliko miaka mingi kama inavyojieleza kwenye Ripoti ya CAG ukurasa wa 31&32. Ambapo imebainishwa kwamfano, mwaka 2013/14 makadirio ya makusanyo ya kodi  yalikuwa billion10,320 lakini ikakusanywa bilioni 9289 , sawa na pungufu ya bilioni 1031, Mwaka 2014/15 Makisio ilikuwa kukusanya billion11262 lakini ikakusanywa billion9919 sawa na pungufu ya billioni1343. Lakini Mwaka wa Kwanza wa awamu ya tano, hesabu za 2015/16 , Makadirio yalikuwa billioni12363 lakini makusanyo yakafika billion12464 sawa na ziada ya billion101 na hata mwaka 2016/17 ambapo makisio yalikuwa juu kuliko mwenendo wa awali kwa kuwekwa billioni 15105 lakini bado makusanyo yalifika billioni14271 sawa na pungufu ya billioni834,pungufu ambayo bado ni kidogo kulinganisha na miaka iliyotangulia.( Rejea Ripoti ya CAG ukurasa31&32).

Niwashukuru watanzania wote mliohitaji kusikia maoni yangu.
David KAFULILA
Leo Aprili16,2018.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: