Mwanamama Annie Kwayu mkazi wa Msasani jijini Dar es Salaam amemuomba Mkuu wa Mkoa, Paul Makonda na Rais John Magufuli kuingilia kati shinikizo la kutaka kutapeliwa nyumba yake na Ally Sumaye ambaye ni Ndugu wa Waziri Mkuu Mstaafu, Fredrick Sumaye.

Akizungumza na wandishi wa habari nyumbani kwake, Annie anasema Sumaye na Aliyekuwa balozi wa Tanzania nchini Msumbiji, Abubakary Abraham wamekuwa wakimuandama kwa takribani miaka tisa kushinikiza aondoke ndani ya nyumba yake wakidai wao ndio wamiliki halali.

" Hii nyumbani nilinunua kwa dada mmoja anaitwa Lydia Syria dola 180,000 lakini kwa sababu nyumba ilikua haina hati ikabidi nitoe dola laki moja halafu iliyobaki nitamalizia. Lakini matokeo yake wakaanza kujitokeza watu mbalimbali wakisema kwamba nao wamenunua hiyo nyumba.

" Kila nilipowasiliana na Lydia kumueleza kuwa kama ameuza nyumba kwa watu wengine anirudishie pesa yangu alikataa, tulifungua kesi nyingi sana mahakama kuu na zote nilishinda lakini huyu Sumaye na Balozi bado waliendelea kunisumbua na kunifanyia fujo nyumbani kwangu," alisema Annie.

Alisema chanzo cha misukosuko yote ambayo anakumbana nayo hivi sasa ni kutokana na yeye kuwa na msimamo mkali dhidi ya Sumaye na Aboubakry ambao walikuwa wakihitaji kufanya biashara na mume wake, Francis raia wa Ubelgiji lakini yeye alikuwa akikataa kwa sababu hakua akiwaamini.

" Hawa watu walishawahi kunifuata wakaniambia niwaache wafanye biashara na mume wangu na kama sitaki basi nijue sitodumu nae tutaachana, kweli mimi nilipoendelea kushikilia msimamo wangu wakafanya mbinu zote kutuachanisha.

" Kilio changu naomba kimfikie Rais Magufuli na RC Makonda, ninateseka sana kila siku nasumbuliwa na hawa watu nimeshazunguka kila sehemu, kituo cha Polisi Osterbay napo nilishawahi kufika kueleza shida yangu hata wakati Makonda anafanya operesheni yake ile nilifika lakini sikupata msaada kwa wale wanasheria mkoani.

" Mei mwaka jana walinivamia hapa nyumbani kwangu wakanifanyia fujo, wakanipiga na kunidhalilisha kwa kunichania nguo lakini hata nilipoenda kushitaki kituo cha Polisi Osterbay hakuna hatua yoyote ambayo ilichukuliwa na watu hao waliojitambulisha kama Sifimba kutoka kampuni ya udalali ambao walitumwa na Sumaye," alisema Annie.

Alidai kuwa Balozi Nkya amekuwa akisambaza uzushi kwamba yeye ni kichaa ili asisaidiwe kila anapokwenda kwenye taasisi na vituo mbalimbali kuomba msaada wa kisheria.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: