Serikali imesema ujenzi wa reli ya kisasa (Standard Gauge) kutoka Morogoro hadi Makutopora mkoani Dodoma ambao utaanza kabla ya Machi mwaka huu, utagharimu dola 1.923bilioni za kimarekani (sawa na Sh4.3 trilioni).

Meneja Mradi huo wa Kampuni Hodhi ya Raslimali za Reli (Rahco) Mhandisi Maizo Mgedzi amesema mradi huo unatarajia kuanza wakati wowote kabla ya Machi.

Amesema  treni hiyo ina uwezo wa kwenda kilometa 160 kwa saa itahifadhi mazingira na kwamba itaweza kubeba mzigo mkubwa kwa zaidi ya mara tano ya reli ya sasa.

“Pia itaweza kubeba watu na mizigo kwa usalama kwa maana  hakutakuwa na ajali zinazosababishwa na ubovu wa miundombinu,” amesema

Meneja wa Kampuni ya Yapi Merkezi iliyopewa zabuni ya mradi huo, Abdullah Kilic amesema kuwa jiwe la msingi la mradi huo litawekwa wakati wowote kuanzia sasa.

“Tunachosubiri ni utaratibu wa Ikulu lakini jiwe la msingi tutaliweka wakati wowote kuanzia sasa,”amesema.

Mbunge wa jimbo la Dodoma Mjini, Antony Mavunde amesema Serikali ingependa mradi huo ulete matokeo chanya kwa watu wa Dodoma na si laana.

“Matokeo haya yasiwe laana kwa maana tusije kuiacha reli hii ipite tu hapana. Sisi tunataka kwa watu wa Dodoma reli hii iwe kichocheo cha kwanza cha uchumi ikiwezekana kubadilisha mji,”amesema.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kongwa alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Deogratius Ndejembi amesema viongozi watawapa ushirikiano wa kutosha katika kipindi cha miaka mitatu cha ujenzi wa reli hiyo na kurekebishana kwa baadhi ya mambo.

“Wamesema asilimia 80 (watu 3000) watachukua watu wa Dodoma kwa hiyo ni jambo kubwa sana. Hii ni fursa kubwa hata kipindi hiki cha ujenzi,”amesema.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: