WAKATI Kaimu Kocha wa Simba, Masoud Djuma, akiamini Asante Kwasi atawasaidia kutwaa mataji msimu huu, beki huyo amepania kufanya mambo makubwa zaidi hasa kufunga mabao muhimu.
Usiku wa kuamkia jana Ijumaa, Kwasi aliifungia Simba bao moja katika ushindi wa mabao 3-1 katika mchezo wa Kombe la Mapinduzi dhidi ya Jamhuri kwenye Uwanja wa Amaan visiwani Zanzibar.

Kwasi raia wa Ghana aliichezea Simba kwa mara ya kwanza baada ya kusajiliwa katika usajili wa dirisha dogo Desemba mwaka jana akitokea Lipuli FC ya Iringa. Msimu uliopita Kwasi alichezea Mbao FC.
Beki huyo aliliambia Championi Jumamosi kuwa: “Nimejisikia furaha kufunga bao lile katika mechi yangu ya kwanza, na naamini nitaendelea kufunga zaidi na kuisaidia timu yangu kufanya vizuri kwenye michuano hii.
“Najua kiu ya mashabiki ni kuniona nafanya yale niliyokuwa nayafanya katika timu niliyotoka awali, kazi ni kuzuia pia kufunga mabao muhimu kwa timu yangu.

“Nitaendelea kupambana kuhakikisha Simba inafanya vizuri si kwenye michuano hii pekee, bali hata kwenye michuano mingine ambayo tunashiriki msimu huu.”
Naye Kaimu Kocha wa Simba, Djuma ameonyesha kunogewa na uwezo wa Kwasi kiasi cha kusema, beki huyo atawapa mataji msimu huu.
Djuma ametoa kauli hiyo kutokana na ukweli kwamba, Kwasi ameonyesha uwezo mkubwa wa kulinda lango na kufunga mabao ndani ya wakati mmoja.
“Katika timu yangu nataka kuona kila mchezaji anafunga mabao bila ya kuangalia beki au kiungo
kwani kazi ya kufunga siyo ya washambuliaji peke yake, naamini uwezo mkubwa wa kufunga wa Kwasi licha ya nafasi anayocheza.
“Ujio wa Kwasi katika timu yetu kutaisaidia timu yetu kupata makombe, kwani tofauti na uwezo wake kulinda na kuokoa hatari golini ana uwezo wa kufunga mabao.
“Alitufunga wakati akichezea Lipuli na hapa amefunga, huyu ni mtu muhimu pia nimefuatilia rekodi yake akiwa Mbao FC kabla ya kwenda Lipuli alikuwa akifunga mabao,” alisema Djuma.
Kwasi leo anaichezea Simba dhidi ya Azam FC kwenye mechi ya Kundi A la Kombe la Mapinduzi.

Share To:

msumbanews

Post A Comment: