Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania TCRA imetangaza hukumu dhidi ya vituo viwili vya Redio vilivyofungiwa kutokana na kile serikali  ilichosema kuwa ni kuchochea ghasia na kumkashifu Rais John Magufuli.

Vituo vilivyokuwa vimefungiwa kwa muda usiojulikana kwa tuhuma za kukiuka Sheria za Utangazaji ni Magic FM cha jijini Dar es Salaam na Redio 5 cha jijini Arusha .

Kupitia maamuzi yaliyosomwa na Makamu mwenyekiti wa kamati ya maudhui Joseph Mapunda Kamati imeikuta Redio 5 na hatia ya kumkashifu rais na kuchochea uvunjifu wa amani na hivyo imehukumiwa kulipa shilingi milioni 5 za Tanzania.

Aidha, kituo hicho cha redio kimefungiwa kutorusha matangazo kwa miezi mitatu na kuwekwa chini ya uangalizi wa mwaka mmoja.

Wakati huo huo Radio Magic FM imepewa onyo na kutakiwa kumwomba radhi rais wa Tanzania pamoja na wasikilizaji wa redio hiyo kwa siku tatu mfululizo.

Tangu tarehe 29 mwezi Agosti 2016 Waziri wa Habari nchini humo Nape Nnauye alitangaza kuvifungia vituo hivyo viwili vya redio kwa muda usiojulikana kwa madai kuwa vilikiuka sheria za utangazaji.

Hukumu hiyo iliiibua minong'ono miongoni mwa wananchi wa Tanzania wakidai kuwa huo ni uminyaji wa uhuru wa habari hasa katika kipindi ambacho Tanzania iko katika vuguvugu kali la mvutano kati ya Serikali na vyama vya upinzani.


 


Share To:

msumbanews

Post A Comment: