KESI YA DADA YAKE BILIONEA ERASTO YAZIDI KURINDIMA MAHAKAMANI.
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu itatoa uamuzi wa malalamiko ya
washtakiwa wa mauaji ya dada wa bilionea Erasto Msuya, mnamo Septemba
27.
Mahakama ilipanga kutoa uamuzi huo jana baada ya kusikia majibu ya hoja za upande wa mashtaka.
Washtakiwa
katika kesi hiyo, Miriam Stephen Mrita (41) na mfanyabiashara Revocatus
Evarist Muyela (40) wanadaiwa kumuua kwa makusudi Anathe Msuya, kwa
kumchinja, nyumbani kwake, Kibada Kigamboni Mei 25, 2016.
Miriam
ambaye ni mshtakiwa wa kwanza katika kesi hiyo alikuwa mke bilionea
Msuya. Bilionea Msuya aliuawa kwa risasi Agosti, 2015 eneo la
Mijohoroni, kando ya Barabara ya Arusha – Moshi wilayani Hai mkoani
Kilimanjaro.
Washtakiwa hao kupitia kwa Wakili wao Peter Kibatala
wamedai kuwa walikubali kosa hilo baada ya kuteswa na polisi na
kulazimishwa kukubali.
Mbele ya Hakimu anayesikiliza kesi hiyo,
Magreth Bankika, Wakili Kibatala amedai kuwa washtakiwa hao wana
vielelezo vya mateso waliyoyapata ikiwamo kuvimba miguu na majeraha ya
mwili.
Kutokana madai hayo, ameiomba Mahakama iamuru uongozi wa
Magereza kuwafanyia uchunguzi wa afya na matokeo ya uchunguzi huo
yawasilishwe mahakamani na kuwekwa katika kumbukumbu.
Hata hivyo,
upande wa mashtaka umepinga madai hayo na Wakili wa Serikali, Diana
Lukondo ameieleza Mahakama kuwa shtaka linajitosheleza kiasi kwamba
washtakiwa wanaelewa kile wanachoshtakiwa.
Wakili Lukondo amedai
kuwa si kweli kwamba waliteswa na kama ingekuwa hivyo, wangefuata
taratibu na kwamba uongozi wa Magereza hauwezi kumtibu mtu ambaye hana
Fomu namba tatu ya Polisi .www.msumbanews.blogspot.com
Back To Top
Post A Comment: