"Mmeridhika?"  ndivyo anavyosikika Ofisa Upelelezi (OC CID) wilaya ya Mtwara, Gilbert Kalanje na mshtakiwa namba moja wa kesi ya mauaji inayowakabili maafisa saba wa Polisi mkoani Mtwara huku kesi hiyo ikiahirishwa.

Kalanje na maofisa wenzake sita leo Jumanne Machi 8, 2022 wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mtwara kwa ajili ya kesi hiyo ya mauaji inayowakabili kutajwa.

Tofauti na washtakiwa wengine sita ambao mara zote wakifikishwa mahakamani hapo kwa ajili ya kesi hiyo kutajwa, wamekuwa wakijifunika nyuso zao au kuvaa barakoa zilizoficha sehemu kubwa ya nyuso zao, Kalanje amekuwa akiachia sura yake na kuruhusu waandishi waendelee na kazi ya kumpiga picha.

Maafisa saba wa polisi wanaoshtakiwa kwa mauaji ya mfanyabiashara wa madini, Musa Hamis wakiwa katika mahakama ya Hakimu Mkazi Mtwara, Machi 8, 2022. Picha na Mwanamkasi Jumbe

Leo, Kalanje akiwa na pingu mkononi baada ya kushuka kwenye gari ya mahabusu alisimama vizuri mbele ya wanahabari na wapiga picha waliokuwa wakihangaika kupata picha nzuri za washitakiwa hao baada ya gari iliyowabeba kusimama mbele ya lango la kuingilia chumba cha mahakama, akiwaruhusu wampige picha.

Hata hivyo, wakati wakifikishwa mahakamani hapo askari polisi waliwazuia waandishi wa habari kupiga picha na kuingia mahakamani mpaka uongozi wa mahakama ulipotoa agizo la kuwaruhusu.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo, Lugano Kasebele ameahirisha kesi hiyo hadi Machi 22, 2022 itakapotajwa tena kwa vile upelelezi wake haujakamilika.

Washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Januari 25 na kusomewa shtaka la mauaji ya kukusudia.

Siku hiyo mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Kasebele ilidaiwa kuwa Januari 5 mwaka huu maofisa hao wa polisi walimuua Musa Hamis Hamis (25), mkazi wa Nachingwea mkoani Mtwara.

Maofisa wanaohusishwa na mauaji hayo ni Ofisa Upelelezi  (OC CID) Wilaya ya Mtwara Gilbert Kalanje, Mkuu wa Kituo cha Polisi Mtwara (OCS), Charles Onyango, Ofisa wa Intelijensia ya Jinai Mkoa wa Mtwara, Charles Kisinza na Mkaguzi wa Polisi, John Msuya pamoja na Mganga mkuu wa Zahanati ya Polisi, Marco Mbuta. Wengine ni Mkaguzi wa Polisi, Shirazi Mkupa na Koplo Salum Juma Mbalu.

Share To:

Post A Comment: