Friday, 20 March 2020

Wahamiaji haramu 51 wakamatwa Pwani


Na GUSTAPHU HAULE,PWANI,

JESHI la Polisi Mkoa wa Pwani limewakamata Wahamiaji haramu 51 walioingia nchini kupitia bandari bubu ya ya Makurunge iliyopo katikaTarafa ya Yombo Wilayani Bagamoyo Mkoani humu.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani  Wankyo Nyigesa, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo, ambapo alisema wahamiaji hao walikamatwa  majira ya saa 11 alfajiri Mach 19.

Wankyo alisema, watuhumiwa hao walikabidhiwa kwa vyombo vingine vya dola kwa taratibu za kisheria  ili waweze kuchukuliwa hatua.

Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Zainabu Kawawa ,alisema wahamiaji hao wamekutwa katika pori wakiwa katika harakati za kutafuta usafiri kuelekea Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini ili waweze kuendelea na safari yao hadi Afrika Kusini.

Kawawa, alisema, Wahamiaji hao walikuwa wanaotokea nchini Ethiopia, ambapo katika mahojiano ya awali walikiri kuingia Nchini kwa kupitia Pwani ya Bagamoyo, wakitumia majahazi.

Alisema, Wahamiaji hao walichukuliwa hadi katika kituo cha afya Matimbwa (Bagamoyo) ili kupimwa kama Wana maambukizi ya Virusi vya Corona lakini hatahivyo majibu bado hayajatolewa.

"Wahamiaji hao wamefikishwa katika kituo hicho ili kufanyiwa vipimo vya awali kujiridhisha kama hawana maambukizi ya ugonjwa wa Corona,  kabla ya kupelekwa katika gereza la Kigongoni  Wilayani Bagamoyo wakisubiri kusomewa mashtaka yao ya kuingia Nchini bila kibali,"alisema Kawawa


Wakati huo huo, Jeshi la Polisi Mkoani Pwani linawashikilia watu watatu kwa tuhuma za kuhusika na mauaji na baadae kuzika mwili wa marehemu katika Shamba la Mahindi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani Wankyo Nyigesa alisema, watuhumiwa hao walikamatwa Machi 19 huko Kibindu Wilaya ya Bagamoyo wakituhumiwa kuua na kuzika mwili wake marehemu katika shamba la mahindi.

Wankyo alisema, Machi 3, majira ya saa nane mchana huko Kibindu mtuhumiwa Chacha Machangu (27) alimfumania mke wake akiwa na mwanaume mwingine .

Kamanda alisema, Machangu alimshambulia mke wake kwa kumkata na panga maeneo mbalimbali ya mwili wake na kumsababishia majeraha yaliyopelekea kifo.

Wankyo alisema, Machangu kwa kushirikiana na ndugu zake Emmanuel Machangu (19) na Hamis Machangu (22 walichimba shimo kwenye shamba la mahindi na kufukia mwili wake marehemu.

Kamanda alibainisha kuwa, Machi 19 Jeshi la Polisi lilipata taarifa kutoka kwa wasamaria wema ambapo lilifanikiwa kuwakamata watuhumiwa hao watatu ambao walionyesha shimo lilipo na lilipofukuliwa mwili wake marehemu ulipatikana.

Alisema, mwili wake marehemu ulifanyiwa uchunguzi na daktari na kufanyiwa mazishi kwa kufuata taratibu.

Hatahivyo,kamanda Nyigesa alisema kuwa jeshi hilo bado linaendelea kuwasaka watuhumiwa wengine wanaodaiwa kushiriki katika tukio hilo.

Mwisho

No comments:

Post a comment