Tuesday, 22 May 2018

WAANDISHI WAAHIDI KUSHIRIKIANA NA TFDA KATIKA KUHAMASISHA MATUMIZI SAHIHI YA BIDHAA

Mamlaka ya Chakula na Dawa nchini (TFDA) imeendesha kikao kazi cha wahariri na waandishi wa habari wa mikoa ya Shinyanga na Mwanza kwa ajili ya kuhamasisha kazi na majukumu ya TFDA na kujadiliana kwa pamoja mikakati ya Mamlaka ya kupambana na bidhaa duni na bandia katika soko na namna bora ya kushirikisha wananchi katika udhibiti na hatimaye kuhakikisha kuwa wanatumia bidhaa bora, salama na fanisi ili kumlinda mwananchi. 

Kikao kazi hicho kimefanyika Jumatatu Mei 21,2018 katika ukumbi wa mikutano wa TFDA Kanda ya Ziwa uliopo Buzuruga jijini Mwanza ambapo mgeni rasmi alikuwa mkuu wa mkoa wa Mwanza, Mhe. John Mongella. 

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao kazi hicho cha siku moja Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TFDA, Bi.Agnes Sitta Kijo, alisema kikao hicho kinahusu uhamasishaji wa Sheria ya Chakula, Dawa na Vipodozi Sura 219.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu alisema kuwa, TFDA itaendelea kufuatilia, kuondoa na kuteketeza bidhaa ambazo hazikidhi vigezo vya ubora, usalama na ufanisi ili kuepusha bidhaa duni na bandia  kutumika ambapo amewahimiza Wahariri na Waandishi kufikisha elimu watakayoipata kwa wananchi.

Alisema TFDA imeendelea kutoa elimu kwa wadau mbalimbali kuhusu usalama, ubora, ufanisi wa vyakula, dawa, vipodozi, vifaa tiba pamoja na vitendanishi ili kuwezesha wananchi kupata taarifa sahihi juu ya bidhaa zinazodhibitiwa na Mamlaka na hivyo kusaidia kuondokana na matumizi ya dawa na vyakula vyenye madhara kwa afya.

Aliongeza kuwa hatua hiyo imesaidia TFDA kutekeleza vyema majukumu yake ambapo kwa mwaka 2015/17 usajili wa bidhaa umeongezeka kutoka bidhaa 7,010 hadi kufikia 9,180 hii ikiwa ni ishara njema ya kuwepo ongezeko la uelewa wa matakwa ya sheria miongoni mwa wafanyabiashara.

Akifungua kikao hicho, Mhe. Mongella alivipongeza vyombo vya habari, wahariri na waandishi wa habari ambao wamekuwa wakitoa taarifa mbalimbali kuhusu umuhimu wa kudhibiti bidhaa unaofanywa na TFDA na hivyo kuongeza uelewa kwa jamii.

Baadhi ya wanahabari walioshiriki kikao kazi hicho wamesema kuwa bado jamii imeendelea kupenda kutumia bidhaa zenye viambata sumu kama vile vipodozi na hivyo watatumia vyema vyombo vyao vya habari kufikisha elimu kwa jamii ili waelewe madhara watakayopata na kujiepusha na matumizi ya bidhaa hizo.
1
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. John Mongela akifungua kikao kazi kati ya TFDA, wahariri na waandishi wa vyombo vya habari wa mikoa ya Mwanza na Shinyanga kilichofanyika katika ukumbi wa TFDA Kanda ya Ziwa, Mwanza tarehe 21 Mei, 2018.
2
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TFDA, Bi Agnes Sitta Kijo akitoa maelezo ya utangulizi wakati wa ufunguzi wa kikao kazi kati ya TFDA, Wahariri na Waandishi wa vyombo vya habari wa mikoa ya Mwanza na Shinyanga kilichofanyika katika ukumbi wa TFDA Kanda ya Ziwa, Mwanza tarehe 21 Mei, 2018. Kikao kazi hiki kilihusu uhamasishaji wa Sheria ya Chakula, Dawa na Vipodozi Sura Na.219.
3
Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Habari Maelezo, Bi. Zamaradi Kawawa akieleza wajibu wa waandishi na wahariri wa habari katika kuleta ufanisi wa utekelezaji wa Sheria ya Chakula Dawa na Vipodozi Sura Na. 219.
4
Mkurugenzi wa Dawa na Bidhaa Nyongeza wa TFDA, Bw. Adam Fimbo akifafanua jambo wakati akiwasilisha mada kuhusu udhibiti wa ubora, usalama na ufanisi wa chakula, dawa, vipodozi, vifaa tiba na vitendanishi nchini kwa wahariri na waandishi wa vyombo vya habari wa mikoa ya Mwanza na Shinyanga (hawapo pichani).
5
Mkurugenzi wa Uendelezaji Huduma wa TFDA, Bw. Chrispin Severe, akieleza jambo wakati akiwasilisha mada kuhusu Dira Dhima na majukumu ya TFDA kwa wahariri na waandishi wa vyombo vya habari wa mikoa ya Mwanza na Shinyanga. 
6
Mada kuhusu utambuzi wa dawa bandia na duni ikitolewa wakati wa kikao kazi

No comments:

Post a comment