Articles by "Zanzibar"
Showing posts with label Zanzibar. Show all posts

 RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Mwinyi ameweka jiwe la msingi la jengo la Taaluma na Utawala awamu ya pili katika Taasisi ya Sayansi za Bahari (IMS) ya Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam iliyopo Buyu visiwani Zanzibar.


Ujenzi wa jengo hilo ni miongoni mwa shughuli za utekelezaji wa Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) unaotekelezwa kwa mkopo wa masharti nafuu wa Benki ya Dunia kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Akizungumza katika hafla hiyo Januari 5,2025 visiwani humo, Rais Dkt. Mwinyi amefurahishwa na hatua iliyofikiwa ya ujenzi huo na wanatarajia kazi hiyo itakamilika kama ambavyo mkandarasi ameahidi na kwa mujibu wa mkataba uliosainiwa

"Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar tunaahidi kuendelea kutoa ushirikiano wa kutosha kwa taasisi hii kwani ni taasisi muhimu na ina mchango mkubwa katika mipango yetu, na sera za Serikali ninayoiongoza katika kuendeleza uchumi wa buluu unaozingatia matumizi endelevu ya rasilimali za bahari". Amesema

Aidha Dkt. Mwinyi amesema kupitia Chuo hicho watapata wataalamu wa uvuvi na wataalamu wa wanaojihusisha na masuala ya bahari kwa ujumla wake.

"Ninafuraha leo tumefikia hatua hii ya kuweka jiwe la msingi ili Chuo hiki kiwe kikubwa zaidi, kiwe bora zaidi na kuweza kutoa taaluma nyingi zaidi kwaajili ya kutunufaisha sisi hapa Zanzibar lakini na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ujumla wake.

Amesema matarajio yao makubwa ya Chuo hicho ni kuona kinawapatia matokeo ya tafiti mbalimbali zinazofanywa na zinazohusiana na uchumi wa buluu.

Pamoja na hayo amesema kuwa katika miaka 61 ya Mapinduzi wamepata mafanikio makubwa ya Maendeleo katika kila sekta ikiwemo sekta ya elimu .

Kwa upande wake Mkuu wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam ambaye pia ni Rais Mstaafu, Dkt. Jakaya Kikwete amemshukuru Rais Mwinyi kwa uwamuzi wake kuwawezesha kupata Hatimiliki ya Ardhi ya eneo hili la Taasisi ya Sayansi za Bahari.

Pia amemshukuru kwa kukubali maombi yao ya kutengenezewa barabara inayokuja hapo chuoni ambayo haikuwa katika hali nzuri.

"Wote ni mashuhuda kwa muda mfupi tu baadaye ahadi yako ya kuiboresha barabara ya kuja Buyu imetimia, tena imewekwa lami! kwa kweli hatuna budi kusema asante sana. Changamoto ya barabara haipo tena, na imerahisisha sana usafiri wa wanafunzi wetu ambao mabweni yao yapo Mazizini. Hivi sasa, mabasi ya Chuo yanachukua muda mfupi zaidi kufika hapa kuwaleta wanafunzi na wafanyakazi". Amesema Dkt. Kikwete.

Pamoja na hayo ameishukuru Benki ya Dunia kwa ufadhili, Wamewapatia uwezo wa kukamilisha ujenzi wa Jengo la Taaluma na Utawala katika Taasisi hiyo. Kwa fedha walizopata pia watajenga Bweni moja la wanafunzi.

"Tunapendezwa sana na ushirikiano waliotuonesha ndugu zetu wa Benki ya Dunia. Katika hatua za utekelezaji wa mradi huu tumekuwa nao, na hata leo wawakilishi wao wameungana nasi kushuhudia uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi hapa Buyu". Ameeleza

Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia Mhe.Prof Adolf Mkenda amesema mkopo wa bilioni 972 kutoka benki ya dunia ni kwaajili ya kuimarisha elimu vyuo vikuu nchini.

Nae Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam, Prof. William Anangisye amesema hatua ya ujenzi imefikia asilimia 50 na tayari mkandarasi ameshalipwa Shilingi Bilioni 4.2 ambayo inajumuisha majengo yote mawili.

Vilevile, amesema Mradi umetenga bajeti ya vifaa vya maabara kwa ajili ya vyumba vyote vya maabara na hatua za awali za ununuzi wa vifaa hivyo zimeanza kwa kuzingatia hatua ya ujenzi ulipofikia.Amesema Jengo la taaluma na utawala lina maabara tano, madarasa yatakayochukua wanafunzi 250, ukumbi wa kisasa wa mikutano utakaochukua watu 150 na ofisi za wafanyakazi.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akiondoa pazia na Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete, kuweka Jiwe la Msingi la Ujenzi wa jengo la Taaluma na Utawala la Taasisi ya Sayansi za Bahari la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, linalojengwa Buyu Wilaya ya Magharibi “B” Unguja, ikiwa ni shamrashamra za Maadhimisho ya Miaka 61 ya Mapinduzi Matukufu wa Zanzibar.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Wananchi katika viwanja vya Chuo Buyu, wakati wa hafla ya uwekaji wa Jiwe la Msingi la Ujenzi wa Jengo la Taaluma na Utawala la Taasisi ya Sayansi za Bahari Buyu Zanzibar Wilaya ya Magharibi “B” Unguja Januari 5, 2025, ikiwa ni Shamrashamra za Maadhimisho ya Miaka 61 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.
Mkuu wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam ambaye pia ni Rais Mstaafu, Dkt. Jakaya Kikwete akizungumza na Wananchi katika viwanja vya Chuo Buyu, wakati wa hafla ya uwekaji wa Jiwe la Msingi la Ujenzi wa Jengo la Taaluma na Utawala la Taasisi ya Sayansi za Bahari Buyu Zanzibar Wilaya ya Magharibi “B” Unguja Januari 5, 2025, ikiwa ni Shamrashamra za Maadhimisho ya Miaka 61 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.
Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia Mhe.Prof Adolf Mkenda akizungumza na Wananchi katika viwanja vya Chuo Buyu, wakati wa hafla ya uwekaji wa Jiwe la Msingi la Ujenzi wa Jengo la Taaluma na Utawala la Taasisi ya Sayansi za Bahari Buyu Zanzibar Wilaya ya Magharibi “B” Unguja Januari 5, 2025, ikiwa ni Shamrashamra za Maadhimisho ya Miaka 61 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam, Prof. William Anangisye akizungumza na Wananchi katika viwanja vya Chuo Buyu, wakati wa hafla ya uwekaji wa Jiwe la Msingi la Ujenzi wa Jengo la Taaluma na Utawala la Taasisi ya Sayansi za Bahari Buyu Zanzibar Wilaya ya Magharibi “B” Unguja Januari 5, 2025, ikiwa ni Shamrashamra za Maadhimisho ya Miaka 61 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akiwa na Mkewe Mama Mariam Mwinyi wakisalimiana na Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, alipowasili katika viwanja vya Chuo Buyu kwa ajili ya uwekaji wa Jiwe la Msingi la Ujenzi wa jengo la Taaluma na Utawala la Taasisi ya Sayansi za Bahari Buyu Wilaya ya Magharibi “B” Unguja Januari 5, 2025, ikiwa ni Shamrashamra za Maadhimisho ya Miaka 61 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akielekea katika eneo lililoandaliwa kwa ajili ya kuzungumza na Wananchi na Wanataaluma wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, baada ya kuweka jiwe la Msingi la ujenzi wa jengo la Taaluma na Utawala la Taasisi ya Sayansi za Bahari Buyu Zanzibar,Wilaya ya ya Magharibi “B” Unguja Januari 5, 2025, ikiwa ni shamrashamra za Maadhimisho ya Miaka 61 ya Mapinduzi Matukufu wa Zanzibar.
Rais wa Zanzibar na Mwnyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akimsikiliza Prof.Bernadeta Killian akitowa maelezo ya kitaalamu ya ujenzi wa jengo la Taaluma na Utawala la Taasisi ya Sayansi za Bahari la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, linalojengwa katika eneo la Chuo Buyu Wilaya ya Magharibi “B”Unguja Januari 5, 2025, na (kushoto kwa Rais) Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia Tanzania Mhe.Prof. Adolf Mkenda na Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Mhandisi Zena Ahmed Said na (kulia kwa Rais) Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mariam Mwinyi.
Muonekano wa Jengo la Taaluma na Utawala la Taasisi ya Sayansi za Bahari la Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam, lililowekwa Jiwe la Msingi la ujenzi wake na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi ,linalojengwa katika eneo la Buyu Wilaya ya Magharibi “B” Unguja Januari 5, 2025,ikiwa ni Shamrashamra za Maadhimisho ya Miaka 61 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.
Baadhi ya wageni waalikwa na Wananchi katika hafla ya uwekaji wa Jiwe la Msingi la Ujenzi ya Jengo la Taaluma na Utawala la Taasisi ya Sayansi za Bahari Buyu Zanzibar Wilaya ya Magharibi “B” Unguja, hafla hiyo iliyofanyika Januari 5, 2025, katika viwanja vya Chuo Buyu, ikiwa ni Shamshamra za Maadhimisho ya Miaka 61 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.



 Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, ametoa wito kwa Mamlaka husika Nchini kuhakikisha Mapitio ya Sera ya Mazingira yanakuwa shirikishi katika ngazi zote, kwa kuzingatia kwamba maisha ya kila siku ya Wananchi yanategemea maliasili.

Mheshimiwa Othman ameyasema hayo leo wakati wa Uzinduzi wa Mchakato wa Mapitio ya Sera ya Mazingira ya Zanzibar ya Mwaka 2013, huko katika Ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip, Uwanja wa Ndege, Mkoa wa Mjini-Magharibi Unguja.

Amesema, Zanzibar hivi sasa inashuhudia mabadiliko makubwa ya kiuchumi na ya kijamii yanayopelekea matumizi makubwa ya maliasili ziliopo, ambayo yanachangia kwa kiasi kikubwa, kuongeza shinikizo katika ikolojia za baharini na nchi-kavu,  na kinachodhihiri ni kuwa Mabadiliko ya Sera ya Mazingira yanahitajika ili kwenda sambamba na kukabiliana na changamoto za kimazingira, ili hatimaye kuielekeza Nchi na Taifa kwa ujumla, katika maendeleo endelevu, yanayozingatia matumizi bora ya maliasili ziliopo, za nchi-kavu na baharini.

“Kwa ajili ya kufikia kwenye azma hiyo, ni vyema Mchakato wetu wa Kupata Sera Mpya ya Mazingira uwe shirikishi katika ngazi zote, ili pia kupata maoni kamili ya wadau juu ya mambo muhimu na ya msingi, ambayo yanafaa kuzingatiwa kwenye Sera hiyo, pamoja na kuelewa ni upi wajibu wa wadau katika kuhakikisha utekelezaji wake”, amesisitiza Mheshimiwa Othman.

Mheshimiwa Othman ameeleza kuwa Miaka 10 imepita tokea kuzinduliwa kwa Sera ya Mazingira ya Mwaka 2013, ambapo tangu Mwaka 2013, kumekuwepo na Maamuzi kadhaa ya Kitaifa, Kikanda na Kimataifa yanayoelekeza Visiwa vya Zanzibar kufikia Lengo la Maendeleo Endelevu, ambayo ni pamoja na Dira ya Maendeleo ya Zanzibar ya 2050; Mpango wa Maendeleo wa Zanzibar wa 2021-2026; Mpango wa Kuirithisha Zanzibar ya Kijani (Zanzibar Green Legacy Programme), kwa azma pia ya kusimamia utekelezaji wa Mikataba, Maazimio na Makubaliano ya Kimataifa juu ya Usimamizi wa Mazingira, ambapo pia Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeridhia na au imesaini pamoja na kuwepo kwa Sera nyengine Mpya za Kisekta, ikiwemo Sera ya Uchumi wa Buluu 2022.

“Kama mnavyofahamu, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais kupitia Idara ya Mazingira inalo jukumu kubwa la kuhakikisha kuwa nyezo za usimamizi wa mazingira ambazo ni pamoja na Sera, Sheria, Kanuni, Mikakati na Miongozo ya kimazingira, zinakuwepo na kutekelezwa kikamilifu, ili kusaidia katika usimamizi bora na endelevu wa mazingira hapa Visiwani; kutokana na majukumu hayo, mnamo Mwaka 2013 Sera ya Mazingira iliandaliwa ili kuchukua nafasi ya Sera iliyoitangulia ya Mwaka 1992; Sera hii ilihusisha Sekta mbalimbali zikiwemo Maji, Afya, Misitu, Utalii, Kilimo, Ufugaji, Nishati, Uvuvi na Rasilimali za Baharini kwa ujumla”, amefafanua Mheshimiwa Othman.

Amefahamisha kuwa Zanzibar katika hali yake ya asili ilikuwa na mazingira mazuri, yenye fukwe za kupendeza, bahari iliyosheheni rasilimali za aina tofauti, udongo wenye rutuba, miti na wanyama wa aina mbalimbali, mambo ambayo yalipelekea kuifikisha Nchi katika maendeleo yaliyopo sasa.

Hata hivyo amesema, hali hiyo kwasasa imeanza kubadilika na kuleta changamoto kadhaa za kimazingira ambazo zimeshajitokeza na kuwa tishio kwa mustakabali wa maendeleo endelevu ya Nchi na Taifa kwa ujumla.

Hivyo ameagiza kwa kusema, “tunapaswa kuhakikisha kwamba,  Mchakato wa Mapitio ya Sera ya Mazingira unatuhakikishia kuwa tunakuja na Sera Mpya ya Mazingira ambayo inatuvusha hapa tulipo na kuiweka Zanzibar kwenye ramani ya dunia, ikiwa na mazingira bora na endelevu kwa faida ya kizazi cha leo na kijacho”.

Mheshimiwa Othman amefahamisha kuwa Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, pamoja na Serikali kwa jumla, inategemea kupata Sera ya Mpya ya Mazingira ambayo ni shirikishi, iliyo bora kabisa, na yenye kutekelezeka, kwaajili ya maendeleo endelevu ya Zanzibar. Sekta ya Mazingira, na kwa kuzingatia kwamba yenyewe ni “Sera Mtambuka”.

Aidha Mheshimiwa Othman ameishukuru kwa dhati Taasisi ya Climate Action Network (CAN) Tanzania, kwa msaada wa kitaalamu na wa kifedha kwaajili ya kuwezesha mapitio ya Sera hiyo, ambapo amesema mategemeo yaliyopo ni pamoja na kuwa Wataalamu hao wataendelea kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, katika kutayarisha Mpango wa Utekelezaji wa Sera na pia maeneo mengine muhimu ya mabadiliko ya tabianchi.

Naye, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Bi. Harusi Said Suleiman, ameshukuru juhudi zinazochukuliwa na Serikali kwa kushirikiana na Taasisi nyengine, ili kutimiza lengo la kupambana na athari za mazingira zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi.

Akieleza Lengo Kuu la Mkutano huo ambalo ni Kuzindua Mapitio ya Sera ya Mazingira ya Zanzibar ya Mwaka 2013 ili kupata Sera ya Mpya ya Mazingira kwa maendeleo endelevu ya Zanzibar, Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Dokta Omar Dadi Shajak, ameitaja dhamira ya Hatua hiyo akisema,  “Sera ya Mazingira ya Mwaka 2013 imekuwa ikituongoza kwa takriban miaka 10, na sasa kwa kushirikiana na Taasisi ya Climate Action Network Tanzania, tunaanza mchakato wa kuifanyia mapitio na maboresho, ili hatimaye kupata Sera yenye kubeba maono mapana ya Sekta ya Mazingira, ambayo ni miongoni mwa Sekta Mtambuka”.

Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Climate Action Network (CAN) Tanzania, Dokta Sixbert Mwanga, ameeleza kwamba Taasisi yake inafanyakazi kwa kutarajia mabadiliko endelevu katika ngazi zote, kupitia nadharia ya 'Think' ambayo inalenga katika Sera, Ubunifu na Miongozo ya Kisekta; sambamba na 'Tank' inayoangaza dhamira ya utekelezaji wa vitendo katika nyanja zote za maisha ya watu ndani ya Jamii, kwa uhalisia na upana wake.

Viongozi mbalimbali wa Serikali, Wadau wa Mazingira, Washirika wa Maendeleo na Asasi za Kiraia wameshiriki katika Hafla hiyo wakiwemo  Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Mazingira Zanzibar, Bw. Sheha Mjaja Juma; Mkurugenzi wa Idara ya Mazingira Zanzibar, Madam Farhat Ali Mbarouk; Mrajis wa Asasi za Kiraia Zanzibar,  Bw. Ahmed Khalid Abdulla;  Mwenyekiti wa Bodi ya Climate Action Network (CAN) Tanzania, Dokta Catherine Massao; na Washiriki kutoka Wizara na Taasisi mbali mbali.

Mkutano huo wa Siku Moja, ambao umekijumuisha pia Kikosi-Kazi cha Kuandaa Sera Mpya ya Mazingira, umeandaliwa na Taasisi ya Climate Action Network (CAN) Tanzania yenye Makao yake Makuu Jijini  Dar es Salaam, kwa kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar.



Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Othman Masoud Othman akifungua rasmi Kongamano la Pili la Uwekezajikati ya Tanzania na Italia lililofanyika katika Hoteli ya Golden Tulip Zanzibar tarehe 28 Septemba, 2022. Pamoja na mambo mengine, Mhe. Othman ametoa wito kwa wawekezaji kutoka Italia na duniani kote kuwekeza Tanzania katika fursa mbalimbali za manufaa.


 Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Othman Masoud Othman amesema Serikali ya Zanzibar inaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji ili kuwawezesha Wawekezaji wenye tija kuwekeza katika sekta mbalimbali ikiwemo sekta ya Uchumi wa Bluu.


Mhe. Othman ametoa kauli hiyo wakati akifungua rasmi Kongamano la Pili la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Italia lililofanyika Zanzibar tarehe 28 Septemba, 2022 na kuwashirikisha wadau mbalimbali wa masuala ya biashara na uwekezaji kutoka Tanzania na Italia.

Mhe. Othman ambaye alimwakilisha Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwenye kongamano hilo amesema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imefungua milango kwa wawekezaji wenye nia ya kuwekeza kwenye maeneo mbalimbali na kwamba inaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji na ufanyaji biashara kwa kuzifanyia maboresho sheria na kanuni mbalimbali za uwekezaji.

Kadhalika alisema maboresho hayo yanakwenda sambamba na yale ya sekta ya utoaji huduma kama vile za viza, vibali vya kazi na ukaazi pamoja na kuboresha mawasiliano kupitia mifumo ya kidigitali ambapo Serikali hiyo inatarajia hivi karibuni kuzindua mfumo wa uombaji viza kwa njia ya mtandao.

"Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji ili kuifanya Zanzibar kuwa miongoni mwa maeneo bora ya uwekezaji duniani. Uwekezaji una manufaa makubwa ya kiuchumi kwa nchi ikiwa ni pamoja na kukuza pato la taifa pamoja na kutenegeneza ajira kwa vijana na wanawake " alisema Mhe. Othman.

Mhe. Othman ameeleza kuwa, katika kipindi cha miaka miwili kuanzia mwezi Novemba 2020 hadi wakati wa kongamano hilo Zanzibar imesajili miradi ya uwekezaji 196 yenye thamani ya dola za marekani bilioni 1. 4 ambapo miradi hiyo inatarajiwa kutengeneza ajira zipatazo 9,000. Hivyo alihimiza washiriki kutumia Kongamano hilo kama chachu ya kuhamasisha wawekezaji wengi zaidi kuja nchini.

“Kongamano hili liwe chachu ya kuvutia na kuhamasisha wawekezaji zaidi kuja Zanzibar na Tanzania kwa ujumla. Naendelea kutoa wito kwa wawekezaji kutoka Italia na duniani kote kuchangamkia fursa lukuki za uwekezaji tulizonazo. Namaliza kwa kusema Wekeza Zanzibar, Wekeza sasa” alisisitiza Mhe. Othman

Awali akizungumza wakati wa kongamano hilo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji, Mhe. Mudrick Soraga amepongeza jitihada zinazofanywa na Balozi wa Tanzania nchini Italia, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo na Balozi mwenzake wa Italia hapa nchini, Mhe. Marco Lombardi za kuandaa kongamano hilo kwa mara ya pili ikiwa ni mchango wao wa kuhakikisha nchi hizi mbili zinanufaika kupitia ushirikiano mzuri uliopo.

Pia aliwataka washiriki wote kutumia kongamano hilo kama fursa ya kubadilishana mawazo na uzoefu miongoni mwao ili kuendelea kuboresha sekta ya biashara na uwekezaji nchini.

Mhe. Soraga pia alitumia fursa hiyo kuainisha fursa za kipaumbele za uwekezaji Zanzibar kuwa ni pamoja na Sekta ya Uchumi wa Bluu, Kilimo, Usindikaji wa mazao ya kilimo, Utalii, ufugaji wa samaki, utalii unaozingatia utunzaji wa mazingira , miundombinu, nishati na uwekezaji katika mali zisizohamishika kama majengo.

Wakati wa Kongamano hilo mada mbalimbali ziliwasilishwa na kujadiliwa ikiwemo Maendeleo ya Miundombinu, Uchumi wa Bluu na Kilimobiashara na Kilimo cha Kisasa cha kutumia mashine na mitambo. Kongamano hilo ambalo limewashrikisha wadau kutoka sekta mbalimbali za biashara na uwekezaji wa hapa nchini na kutoka Italia litahitimishwa rasmi tarehe 30 Septemba 2022 jijini Dar es Salaam.


Sehemu ya Washiriki wa Kongamano wakifuatilia hotuba ya ufunguzi kutoka kwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Othman

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji, Mhe. Mudrick Soraga nae akizungumza wakati wa Kongamano hilo

Sehemu ya Mabalozi na wageni waalikwa wakifuatilia hotuba ya Mhe Soraga

Mkurugezni Mtendaji wa Mamlaka ya Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) akifafanunua fursa mbalimbali za uwekezaji zilizopo Zanzibar

Mhe. Makamu wa Kwanza wa Rais akiwa na Balozi wa Tanzania nchini Italia, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo (kushoto) na Balozi wa Italia nchini, Mhe. Marco Lombardi (katikati)

Sehemu ya washiriki wa kongamano

Sehemu nyingine ya washiriki

Mhe. Balozi Lombardi akizungumza na Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Ofisi ya Mambo ya Nje Zanzibar, Bi. Leluu Abdallah (kushoto) na Afisa Mambo ya Nje, Bi. Salma Baraka

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akiondoa Pazi kuweka Jiwe la Msingi la Ujenzi wa Mradi wa Hospitali ya Wilaya ya Magharibi “B” Unguja inayojengwa katika eneo la Mwanakwerekwe Ijitima, akiwa katika ziara yake leo 17-7-2022,kushoto Waziri wa Afya Zanzibar Mhe. Nassor Ahmed Mazrui, na (Kulia kwa Rais) Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja Mhe.Idrisa Mustafa Kitwana .(Picha na Ikulu) 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akiwa n a Waziri wa Afya Zanzibar Mhe. Nassor Ahmed Mazrui, akitembelea Jengo la Hospitali ya Wilaya ya Magharini “B” Unguja, baada ya kuweka Jiwe la Msingi la ujenzi wa Hospitali hiyo, akiwa katika ziara yake katika Wiliya ya Magharibui”B” Unguja leo 17-7-2022.(Picha na Ikulu) WAZIRI wa Afya Zanzibar Mhe.Nassor Ahmed Mazrui akizungumza katika hafla ya Uwekaji wa Jiwe la Msingi la Ujenzi wa Mradi wa Hospitali ya Wilaya ya Magharibi “B” Unguja, inayojengwa katika eneo la Mwanakwerekwe Ijitimaa ya zamani.(Picha na Ikulu) 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Mwananchi wakati wa ziara yake baada ya kuweka Jiwe la Msingi la Mradi wa Ujenzi Hospitali ya Wilaya ya Magharibi “B” Unguja inayojengwa katika eneo la Mwanakwerekwe Ijitimaa ya zamani Wilaya ya Magharibi “B” Unguja leo 17-7-2022.(Picha na Ikulu) MUONEKANO wa Jengo la Hospitali ya Wilaya ya Magharibi "B" Unguja. RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akipata maelezo ya Mradi wa Ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Magharibi “B” Unguja kabla ya kuweka Jiwe la Msingi la Ujenzi wa Mradi huo, kutoka kwa Mhandishi wa Wizara ya Afya Zanzibar Ndg. Ali Said Bakari na (kushoto kwa Rais ) Waziri wa Afya Zanzibar Mhe. Nassor Ahmed Mazrui na Naibu Waziri wa Afya Mhe.Hassan Hafidh, akiwa katika ziara yake Wilaya ya Magharibi “B” Unguja leo 17-7-2022.

 


Na Imma Msumba Dodoma

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, Leo Mei 16, amemuwakilisha Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti Baraza la Mapinduzi, Dokta Hussein Ali Mwinyi, katika Hafla ya Uzinduzi wa Wiki ya Taifa ya Ubunifu pamoja na Mashindano ya Ubunifu wa Sayansi na Teknolojia kwa Mwaka huu wa 2022.

Akizungumza wakati akifungua maonesho hayo mgeni rasmi Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Othman Masoud Othman amewataka watu mbalimbali wenye uwezo wa kuonesha bunifu mbalimbali kuendelea kujitokeza ili serikali ione namna itakavyowaunga mkono.

Huku akisistiza kuwa “Nimeridhika na mambo niliyo ona wakati napitia mabanda ya maonesho. Inaonekana kuna hatua kubwa iliofikiwa katika ubunifu wa bidhaa kwa kutumia teknolojia mbalimbali za kisasa.”

Hafla hiyo imefanyika katika Uwanja wa Jamhuri, Jijini Dodoma Tanzania, na kuhudhuriwa na Viongozi mbalimbali wa Serikali, Kidini na wa Kimila, Vyama vya Siasa, Wananchi, Vikosi vya Ulinzi na Usalama, Waandishi wa Habari, Wanafunzi, Vikundi vya Burudani, Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muugano wa Tanzania na Vijana wabunifu.

Pamoja na kuhutubia hafla hiyo, Mheshimiwa Othman aliyeambatana na Mke wake, Mama Zainab Kombo Shaib, alipata fursa ya kutembelea Mabanda mbali mbali ya Maonyesho ya Ubunifu na pia kupata maelezo ya Wajasiriambali kutoka Ndani na Nje ya Nchi, yakiwemo Mataifa ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.


 


MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, ameitaka Saudi Arabia kuendeleza umoja wa asili uliopo kati yake na Zanzibar, ili kukuza fursa za maendeleo baina ya pande mbili hizo.

Mheshimiwa Othman ameyasema hayo leo Ofisini kwake Migombani, Jijini hapa akiongea na Balozi wa Saudi Arabia nchini Tanzania, Sheikh Abdullah bin Aliy Alsheryan, aliyewasili hapo ili kujitambulisha.

Amesema Saudi Arabia na Zanzibar, zimekuwa na fungamano na udugu wa asili katika nyanja zote za maisha zikiwemo elimu, utamaduni na maisha ya jamii ambapo ni vigumu hata kubaini zama ambazo mahusiano hayo yalianza.

“Ni vigumu kuelewa ni lini mahusiano haya yalipoanza, kwani hakuna mtaa ambao utakosa mtu aliyefungamana na Saudia, na pia ni vigumu kuona msikiti ambao anakosekana mtu ambaye kasomea katika Nchi hiyo”, amesema Mheshimiwa Othman.

Mheshimiwa Othman amebainisha njia ambazo fungamano hilo linaweza kuendelezwa, na hivyo kufanikisha maendeleo kati ya watu wa pande mbili hizo, zikiwemo fursa za kuhamasisha huduma za kijamii ambazo ni pamoja na usimamizi wa mali za wakfu, sekta ambayo Zanzibar iliianzisha miaka mingi iliyopita.

Aidha Mheshimiwa Othman ameihakikishia Saudi Arabia akisema kwamba milango ya Zanzibar iko wazi katika kusaidiana na kushikamana, ili kukuza mahusiano mema na udugu wa asili baina ya pande mbili hizo muhimu.

Naye Balozi wa Saudi Arabia nchini Tanzania, Sheikh Abdullah Alsheryan, amesema kuwa azma ya nchi yake ni kuendelea kuiungamkono Zanzibar na Tanzania kwa ujumla ili kuhamasisha na kusaidia maendeleo ya watu wake katika sekta mbali mbali.

Amesema sekta hizo ni pamoja na kusaidia upatikanaji wa fursa za kitaaluma na nafasi za masomo katika ngazi mbali mbali, ili kuongeza kiwango cha wahitimu wa Nchi hii, wanaofadhiliwa na Taifa hilo.

Katika ujumbe wake, Balozi Alsheryan aliongozana na watendaji wake mbali mbali akiwemo Mkuu wao wa Itifaki, Sheikh Muhamed Alzabin.

Wakati huo huo, Mheshimiwa Othman amekutana na Balozi wa Jamhuri ya Kenya anayemaliza muda wake nchini, Mheshimiwa Dan Kazungu, aliyefika ofisini hapo kwaajili ya kuaga.

Katika kikao chake na Balozi huyo, Mheshimiwa Othman amesema kuwa pamoja na changamoto nyingi Nchi mbili hizo zinazozipitia, bado zipo fursa kadhaa za maendeleo baina yao zikiwemo za biashara, kilimo na utalii ambazo kupitia mashirikiano mema zinaweza kuchangia kujikwamua kiuchumi.

Pamoja na salamu zake kwa watu wa Kenya, Mheshimiwa Othman amemtakia dua Balozi Kazungu, huku akimtaka aendelee kuyakumbuka mema yote aliyoyapata alipokuwa katika kipindi cha utumishi wake hapa nchini.

Akitoa shukran zake, Balozi Kazungu ameeleza kuwa pamoja na mafanikio mengine, Zanzibar imeionyesha njia Jamhuri ya Watu wa Kenya katika kujenga amani, utulivu, umoja na mshikamano, kupitia maridhiano ya kisiasa.

Balozi Kazungu ambaye ameishi na kukulia katika Ukanda wa Pwani ya Kenya amesifia mazingira ya sasa ya Zanzibar na Tanzania kwa ujumla, ambayo amesema yanatoa fursa kwa wananchi wake, na hata kutoka majirani wa Afrika ya Mashariki, kushikamana na kujiletea maendeleo.