Articles by "TTB UTALII"
Showing posts with label TTB UTALII. Show all posts
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) akiwa ameambatana na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Hassan Abbasi, ametua jijini London, Uingereza, kwa ajili ya kushiriki Maonesho ya Kimataifa ya Utalii ya WTM London 2026 yanayotarajiwa kufanyika Novemba 3–5, 2026.

Katika siku ya kwanza ya ziara yake, akiwa katika Ubalozi wa Tanzania nchini Uingereza, Dkt. Kijaji leo Novemba 2, 2026 amekutana na kufanya mazungumzo na wadau mbalimbali wa utalii kwa lengo la kujadili fursa na mikakati ya kukuza na kuitangaza Tanzania kama kituo cha utalii katika soko la kimataifa.

Katika mazungumzo hayo, Dkt. Kijaji amepokea wasilisho kuhusu utalii kutoka kwa Bw. Tim Henshall, Afisa anayeshughulikia masuala ya Utalii katika Ubalozi wa Tanzania nchini Uingereza (Tanzania High Commission UK).

Aidha, amekutana na kufanya mazungumzo na Bw. Craig Rix, Mtendaji Mkuu wa Gecko Publishing, ambapo wamejadili fursa za kuitangaza Tanzania kupitia machapisho ya Gecko Publishing, ikiwemo jarida la Travel Africa Magazine, ili kuongeza mwonekano wa vivutio vya utalii vya Tanzania katika masoko ya kimataifa.

Katika kikao kingine, Dkt. Kijaji amekutana na Bw. George Bartlam, Meneja wa Mauzo ya Ubia wa Klabu ya Soka ya Brentford (Brentford Football Club) ambayo kwa sasa inashika nafasi ya 6 katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) ambapo wamejadili uwezekano wa kutumia klabu hiyo kuitangaza Tanzania.

Vikao hivyo vimehudhuriwa pia na Mwakilishi wa Balozi wa Tanzania nchini Uingereza, Bw. Patrick Mwakalobo na Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Dkt. Thereza Mugobi.

Mazungumzo hayo ni sehemu ya juhudi za Wizara ya Maliasili na Utalii za kupanua wigo wa ushirikiano na wadau wa kimataifa, kubuni njia bunifu za kuitangaza Tanzania na kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea nchini.
























 BODI ya Utalii Tanzania (TTB) imemkabidhi rasmi mwanautalii na mtangazaji wa vivutio vya utalii kutoka Oman, Khalid Hamed Al Barwani, Ubalozi wa Hiari wa Utalii wa Tanzania, ikiwa ni hatua ya kimkakati ya kuimarisha juhudi za kuitangaza Tanzania katika masoko ya kimataifa na kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea nchini.

Ubalozi huo umekabidhiwa na Mkurugenzi Mkuu wa TTB, Ephraim Mafuru, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, ikiwa ni kutambua mchango mkubwa wa Al Barwani katika kuitangaza Tanzania kupitia majukwaa mbalimbali ya kimataifa.

Al Barwani alipata umaarufu mkubwa baada ya kuongoza kundi la Dream Team Explorers kutembelea Shamba la Miti la Sao Hill mwaka 2024, ambapo walijionea vivutio vya kipekee vinavyopatikana katika eneo hilo, ikiwemo misitu ya kupandwa, mandhari ya kuvutia ya asili na eneo la Mto Ruaha. 

Maudhui waliyoyashiriki kupitia majukwaa yao ya kidijitali yalichangia kuongeza mwonekano wa Sao Hill na kuibua hamasa ya watalii wa ndani na nje ya nchi kutembelea eneo hilo.

Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi ubalozi huo, Mafuru alisema TTB itaendelea kushirikiana na watu mashuhuri, watengeneza maudhui na wadau wa kimataifa wenye ushawishi mkubwa katika masoko mbalimbali ili kuendelea kuitangaza Tanzania kama moja ya vivutio bora vya utalii duniani.

“Ubalozi huu ni kutambua mchango wa Khalid Al Barwani katika kuitangaza Tanzania na ni sehemu ya mkakati wetu wa kupanua wigo wa masoko ya utalii kupitia mabalozi wa hiari wanaotumia ushawishi wao kufikisha ujumbe wa Tanzania kwa mamilioni ya watu duniani,” alisema Mafuru.

Kwa upande wake, Al Barwani alishukuru kwa heshima hiyo na kuahidi kuendelea kuitangaza Tanzania kupitia majukwaa yake ya kimataifa, akieleza kuwa nchi ina vivutio vya kipekee vinavyostahili kufahamika zaidi duniani.

“Tanzania ni nchi yenye uzuri wa kipekee, kuanzia hifadhi za wanyamapori, misitu, fukwe, utamaduni hadi ukarimu wa wananchi wake. Nitaendelea kuwa balozi wa kuitangaza Tanzania kwa dunia,” alisema.

TTB inaendelea kutumia ushirikiano na wadau wa kimataifa pamoja na mabalozi wa hiari wa utalii kama sehemu ya mkakati wa kuongeza ushindani wa Tanzania katika soko la utalii duniani na kuunga mkono malengo ya taifa ya kukuza sekta ya utalii, kuongeza idadi ya wageni wa kimataifa na kuongeza mchango wa sekta hiyo katika maendeleo ya uchumi wa nchi.




 BODI ya Utalii Tanzania (TTB), imesema moja ya jukumu lake kubwa ni kutangaza utalii wa Tanzania ndani na nje ya nchi, hivyo Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba)yanayoendelea ni jukwaa muhimu la kuendelea kutangaza utalii wetu.


Aidha imesema kupitia maonesho hayo ya Sabasaba pia yamekuwa jukwaa muhimu la kuhamasisha utalii wa ndani, kutangaza vivutio vya utalii na kuwaandaa wadau kunufaika na fursa mbalimbali ikiwemo mashindano ya AFCON yanayotarajiwa kufanyika mwaka ujao.

Akizungumza katika maonesho hayo Naomi Mbilinyi ambaye ni Ofisa Utalii Mwandamizi wa Bodi ya Utalii Tanzania amesema kupitia banda la TTB, wananchi wanapata taarifa kuhusu fursa zilizopo katika sekta ya utalii, ikiwemo namna ya kuanzisha kampuni za utalii, kushiriki maonesho ya kimataifa na kutembelea vivutio mbalimbali vilivyopo nchini.

“TTB pia inatumia maonesho hayo kutangaza Swahili International Tourism Expo, yatakayofanyika mwezi Oktoba, ambapo wadau wanapata fursa ya kujisajili kama waoneshaji, wadhamini na washiriki wa maonesho hayo ya kimataifa.”

Ameongeza pia bodi hiyo inaendelea kujenga mfumo wa kidijitali utakaowezesha wadau wa utalii kusajili taarifa za biashara zao ili kutangaza huduma na vivutio vyao kwa urahisi katika masoko ya ndani na nje ya Tanzania.

Kwa mujibu wa Mbilinyi, banda la TTB pia limetenga eneo maalum la kutoa elimu kuhusu fursa zitakazotokana na mashindano ya AFCON, likiwaelimisha watoa huduma za malazi, usafiri na sekta nyingine jinsi ya kujiandaa kupokea wageni wengi watakaoingia nchini wakati wa mashindano hayo.

Amesema wageni wengi wanaotembelea banda hilo, hususan wakazi wa Dar es Salaam, huonyesha hamu ya kujifunza kuhusu maeneo ya utalii yaliyo karibu nao, ikiwemo fukwe, maeneo ya kihistoria, makumbusho na vivutio vingine vinavyoweza kutembelewa kwa safari za siku moja (city tour).

Pia amesema wananchi wengi huulizia gharama za kutembelea hifadhi za taifa na maeneo mengine ya utalii, ambapo TTB hushirikiana na taasisi mbalimbali za sekta hiyo kuwapa taarifa sahihi na kuwaelekeza kwenye mabanda husika.

Ametoa wito kwa wananchi, Mbilinyi aliwahimiza kutembelea banda la TTB katika Maonesho ya Sabasaba ili kupata taarifa mbalimbali ambazo si rahisi kuzipata sehemu nyingine, ikiwemo usajili wa mifumo ya kidijitali, taarifa kuhusu Swahili International Tourism Expo na maandalizi ya AFCON.

“Maonesho hayo yanatoa nafasi ya wananchi kuzungumza moja kwa moja na wataalamu wa utalii, kuuliza maswali, kutoa maoni na kupata mwongozo kuhusu fursa zilizopo katika sekta ya utalii nchini.”