Articles by "PINDICHANA"
Showing posts with label PINDICHANA. Show all posts

 Waziri wa Maliasili na Utalii na Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Njombe Mhe. Balozi, Dkt. Pindi Chana, Januari 11 2025 ameshiriki katika Baraza la Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Wilaya ya Ludewa ambapo katika baraza hilo amechangia fedha kiasi cha shilingi mililioni 6 kwaajili ya kuwezesha shughuli mbalimbali za UWT Ludewa ikiwemo ujenzi wa nyumba ya mtumishi wa UWT Ludewa.





Na John Mapepele 

Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe, Balozi.Dkt. Pindi Chana ( Mb) amezitaka Halmashauri za wilaya zote nchini kuanzisha matamasha ya Utalii na Uhifadhi huku akielekeza suala la kuwalinda wananchi dhidi ya wanyamapori wakali na waharibifu kuwa ajenda ya kudumu.

Waziri Chana ametoa kauli hiyo leo Desemba 21, 2024 wakati akimwakilisha Mhe. Waziri Mkuu kufungua rasmi msimu wa pili wa Tamasha la Utalii la Same ambapo pia ametoa zawadi na tuzo kwa wadau mbalimbali kutambua mchango wao katika kufanikisha Tamasha hilo 

"Wakati leo tunasherekea Tamasha la pili la Utalii la Same ni lazima tuhakikishe tunawalinda wananchi kutokana na wanyama wakali wakati huo huo tunahifadhi rasilimali tulizopewa na Mwenyezi Mungu ili zitusaidie kutuletea watalii zaidi " amefafanua Mhe Chana. 

Amesema Wizara kwa kushirikiana na TAMISEMI na wananchi itaendelea kuhifadhi rasilimali kwa faida ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Aidha amefafanua kuwa usemi wa kiswahii usemao "Tunza mazingira yakutunze" unadhihirisha kuwa mazingira yakitunzwa vizuri ikiwemo misitu na maliasili yatasaidia kujenga uchumi.

 "Tukitunza mazingira tutapata mvua, tutapata maji, tutalima, tutapata vyakula na mazao ya biashara, hakutakuwa na njaa wala umaskini wa kipato na pia tutaishi kutokana na Kuvuta hewa safi.Usemi huo una mashiko ni vyema tukarithisha watoto wetu kuanzia wawapo shuleni ili waweze kutambua umuhimu wa kutunza mazingira"ameongeza Mhe. chana

 Amesema ni muhimu klabu za mazingira zilizopo katika maeneo yetu kuendelea kuzisimamia ili zilete tija kwani kupitia klabu hizo wanafunzi watajifunza hifadhi ya mazingira, utalii na pia watajenga uelewa wa kutosha kutenda popote wawapo kwa falsafa ya "Jenga kesho iliyo bora (BBT)".  

Amepongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassani kwa kuandaa Filamu ya Tanzania the Royal Tour na Amazing Tanzania ambapo amesema kuanzishwa kwa Tamasha la Utalii la Same ni kufuata maono ya Mhe. RAIS katika kutangaza utalii.

Akifafanua kuhusu faida ya Tamasha hilo amesema limesaidia kuwaletea wageni, pia kutoa elimu mbalimbali ya uhifadhi wa mazingira na utunzaji wa vyanzo vya maji kama misitu wa Chome.

Pia kuhusu kuboresha na Tamasha hilo, Mhe. Chana ametaka kuwepo na mikakati madhubuti ya kuendeleza Tamasha hilo kwa Halmashauri kutenga bajeti kuliko kuwaachia wadau wachache na uongozi wa Wilaya hiyo huku akisisitiza kuwa suala la uhifadhi na utalii lipo kwenye Ilani ya Chama Cha Mapinduzi.

"Ndugu zangu suala hili ni la msingi sana hata baba wa Taifa Mwalimu Nyerere alisisitiza kuwa rasilimali hizi lazima zilindwe na ndiyo maana tuna Jeshi la Uhifadhi"amefafanua Waziri Chana

Ametoa wito kwa wananchi kushirikiana na Serikali kuwabaini watu waovu, wanaotaka kuhujumu rasilimali za watanzania.

"Kuna changamoto za maingiliano tuliangalie ili wasilete madhara".

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo, Metheusela Ntonda amesisitiza kuendelea kufungamanisha Utalii na utamaduni kwenye matamasha hayo.

 Tamasha hilo limepambwa na wasanii mbalimbali na linatarajiwa kumalizika hapo kesho.

 


Na Happiness Shayo-Arusha

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi, Dkt. Pindi Chana amesisitiza umuhimu wa kuwa na mikakati endelevu katika kukuza Sekta ya Utalii na Ukarimu hususan katika nyanja za utunzaji wa mazingira, ustawi wa jamii, kutumia teknolojia za kidijitali na kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi kwa maendeleo endelevu na ustawi wa Sekta ya Utalii.

Ameyasema hayo leo Novemba 21, 2024 wakati akifungua rasmi Mkutano wa tatu wa Kimataifa wa Kuunganisha wanataaluma na wadau wa Utalii na Ukarimu katika Nchi Zinazoendelea uliofanyika jijini Arusha.

"Mkutano huu una lengo la kuunganisha wanataaluma na wadau wa sekta ya utalii ambapo kupitia mkutano huu wanataaluma watatoa matokeo ya tafiti na mifumo ya kinadharia inayohitajika kuelewa changamoto kubwa zilizopo, wakati wadau wa sekta watatoa ufahamu wa vitendo kupitia uzoefu wao katika kazi na biashara za utalii ili kusaidia kuleta uvumbuzi, kuimarisha mafunzo, na kuongeza ajira" amesema Mhe. Chana.

Amefafanua kuwa ili Sekta ya Utalii na Ukarimu iendelee ni vyema kukawa na hatua za kulinda mazingira kwa kuhifadhi misitu, wanyamapori, na rasilimali za baharini pamoja na kuwepo na ushirikishwaji wa jamii kwa kuwepo na utalii wa kijamii.

Kuhusu matumizi ya teknolojia ya kidijitali, Mhe. Chana amefafanua kuwa msisitizo juu ya teknolojia katika mkutano huo ni muhimu hasa katika kujadili mada za Mawasiliano ya kidigitali na matumizi ya kompyuta katika Ukarimu na Utalii akitolea mfano kutalii kidigitali na kuwa na vyumba vya hoteli vinavyoendeshwa kidigitali.

Aidha, amesema mabadiliko ya Tabianchi na Maendeleo ya Utalii yanapelekea kufikiria upya kuwa, utalii sio tu njia ya kufikia malengo bali unaambatana na utunzaji wa mazingira na uboreshaji wa jamii.

"Mijadala kuhusu kupunguza athari za mazingira katika Ukarimu na Utalii pia usimamizi wa taka katika upande wa  Ukarimu, zinatoa changamoto ya kufikiria upya namna ilivyofanyiwa kazi na kuhakikisha kwamba Tanzania inapata namna nzuri endelevu itakayosaidia sekta ya Utalii kukua.

Naye,  Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Utalii (NCT), Dkt. Florian Mtey amesema kuwa wakati dunia inakabiliwa na mabadiliko ya tabianchi ni muhimu kuwepo na mijadala endelevu kuhusu namna ya kukabiliana nayo pamoja na namna ya  kukuza utalii na ukarimu kwa kutumia mbinu rafiki wa mazingira, teknolojia za kidijitali, na fursa zingine zilizopo.

Mkutano huo wenye kaulimbiu "Mikakati ya Utalii Endelevu na utalii wa bahari kufikia malengo endelevu na ya kidigitali, yaani “Green and Blue Tourism Strategies Towards Sustainability and Digitalization,” ulioandaliwa na NCT kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Teknolojia cha Tshwane kutoka nchini Afrika Kusini na Chuo cha Utalii cha Kenya kutoka nchini Kenya umehudhuriwa na wadau wa utalii kutoka Kenya, Afrika Kusini, Zambia, Malawi, Botswana, Marekani, Finland, Korea Kusini, India, Sweden, Ethiopia, Ujerumani, China, Uholanzi pamoja na Wakuu wa Taasisi za Wizara ya Maliasili na Utalii,Wakuu wa Taasisi za Elimu kutoka Nchi mbalimbali, Wawakilishi kutoka Mashirika ya Utalii na Wawakilishi kutoka Vyama vya Usafiri wa Anga Nchini.

 


Na Happiness Shayo - Serengeti 

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi, Dkt. Pindi Chana (Mb) amezindua miradi ya kuendeleza utalii ikiwemo Mradi ya Barabara ya Utalii km22 uliogharimu takribani 761.3 na Mradi wa ujenzi wa Vituo Viwili  vya kupokea na kukagua wageni(Ikona Gate na Visitors  Gate) uliogharimu takribani shilingi milioni 143.5 katika Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori Ikona iliyopo Wilaya ya Serengeti Mkoani Mara.

Uzinduzi huo umefanyika leo Novemba 15,2024 katika Jumuiya ya Hifadhi ya Ikona Serengeti Mkoani  Mara.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi huo,  Mhe. Chana ameitaka jumuiya hiyo kuisimamia na kuitumia vyema miradi hiyo kwa malengo yaliyokusudiwa ya kukuza utalii huku akisisitiza maadili katika utendaji kazi.

"Natoa rai kwa Wafanyakazi kuwa waadilifu katika kutekeleza majukumu ya ulinzi na uhifadhi wa rasilimali za Taifa" amesisitiza Mhe. Chana.

Aidha, ameipongeza Menejimenti na Jumuiya ya Ikona huku akitoa rai kuendelea kushirikiana kwa karibu na Halmashauri za Wilaya, Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) na Wizara ya Maliasili na Utalii katika kutekeleza majukumu yao.

Naye, Mhasibu wa Jumuiya ya Ikona, Mariam Magessa amesema kuwa tangu kuanzishwa  kwa Jumuiya hiyo,  imefanikiwa kupunguza matukio ya ujangili hivyo kupelekea ongezeko la wanyamapori huku ikivutia shughuli za utalii na wawekezaji.

"Matokeo chanya ya uhifadhi yamepelekea kupata jumla ya wawekezaji 9 ambapo 8 wamewekeza kwenye utalii wa picha na mmoja kwenye utalii wa uwindaji" amesisitiza Mariam na kusema kuwa hiyo imekuwa ni sehemu ya mapato ya Jumuiya hiyo.

Jumuiya ya Ikona ilianzishwa mwaka 2005 kwa dhumuni la kuendeleza uhifadhi na Usimamizi endelevu wa Maliasili na vivutio vya utalii kama njia ya kukuza uchumi na hivyo kupunguza kiwango cha umaskini kwa wananchi wanaoishi katika vijiji wanachama.









 


Waziri wa Maliasili na Utalii,  Mhe. Balozi, Dkt. Pindi Chana (Mb) ameweka jiwe la msingi na kuzindua Mradi wa Maji wa Kilewani wenye gharama ya shilingi milioni 597.6.

Uzinduzi huo umefanyika katika Kijiji cha Kilewani Wilaya ya Kalambo  Mkoani Rukwa leo Oktoba 1,2024.

Akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara,  Mhe. Chana amesema Serikali imedhamiria kuhakikisha inasogeza huduma za maji kwa wananchi na kumtua mama ndoo kichwani.

"Mradi huu umekuja katikati ya Makazi ya wananchi ili msipate changamoto ya kutumia muda mrefu kutafuta maji" amesisitiza Mhe. Chana.

Aidha,  amewataka wananchi kutunza mradi huo ili ulete manufaa yaliyokusudiwa ya kuwezesha shughuli mbalimbali kama ujasiriamali kufanyika.

Naye, Kaimu Meneja, Wakala wa Usambazaji Maji Vijijini (RUWASA), Francis Mapunda amesema mradi huo ni miongoni mwa miradi iliyojengwa kwa fedha za Mfuko wa Taifa wa Maji (National Water Fund) na unahudumia wakazi wapatao 3,847.

Ameongeza kuwa mpaka sasa mradi huo umetekelezwa kwa asilimia 98 na unatoa huduma iliyokusudiwa kwa wananchi.



Imeelezwa kuwa Kampuni za Kitanzania zinaendelea kuwa vinara wa kutoa huduma na bidhaa za migodini kutokana na mazingira wezeshi yaliyowekwa na Serikali kuwa chachu ya watanzania kuwekeza katika Sekta ya Madini nchini kupitia Sheria ya Ushiriki wa Watanzania katika Sekta ya Madini (Local Content) ambapo Jiji la Mwanza limekuwa mfano mzuri kupitia Kampuni za JC Gear Group (T) Limited na Rock Solutions Limited, kampuni za ndani zinazojihusisha na utengenezaji na usambazaji wa vifaa na bidhaa muhimu zinazotumika katika shughuli za uchimbaji migodini.

Hayo yamebainishwa Septemba 30, 2024, jijini Mwanza na Viongozi wa Kampuni hizo kwa nyakati tofauti wakati wakizungumza na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Madini kuhusu maendeleo ya Miradi ya Kampuni hizo mbili tofauti zilizojikita jijini Mwanza kwa asilimia kubwa.

Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya JC Gear Group (T) Limited, James Makanyaga alisema kuwa, Kampuni hiyo imejikita katika kutengeneza bidhaa muhimu zinazotumika katika mitambo ambayo hutumika migodini pamoja mashine za viwandani, magari ya usafirishaji, na vifaa vya ujenzi ikiwa ni pamoja na matengenezo na ukarabati wa mashine, usambazaji wa vipuri kama bearings, shafts, na gearboxes, pamoja na utoaji wa ushauri wa kiufundi kwa wateja wao.

Makanyaga maarufu kama Jimmy alisema kupitia uwekezaji huo, wanajivunia kutoa ajira za moja kwa moja 36 kwa vijana ambao wote ni watanzania, kwani kupitia kiwanda hicho vijana wamepata mafunzo kuhusu teknolojia mpya na ya kisasa na kwamba matarajio yao ni kuongeza nafasi za ajira kadiri watavyokuwa wanapata kazi kutoka kwenye migodi.

“Sisi bidhaa zetu hazibagui, zinatumika kwenye migodi yote, na katika mitambo yote hadi chini kabisa kwenye migodi, kwa mfano tunakarabati na kutengeneza bidhaa kulingana na mahitaji ya mteja wetu, tunakarabati na kutengeneza bidhaa ambazo hutumika sana kwenye mashine za uchimbaji madini, vifaa vya kuvuta na kusaga mawe, na mitambo mizito inayotumika kwenye uchimbaji wa chini ya ardhi au juu ya ardhi, pia, mitambo inayozalisha umeme, kama vile turbines, hutumia gia kwa ajili ya kusambaza nishati, sisi tunatengeneza hizo hapa” alisisitiza Makanyaga.

Aliongeza kuwa, kama kampuni ya ndani inayotoa huduma za ubunifu na ufundi wa hali ya juu, JC Gear Group (T) Limited ni mfano mzuri wa jinsi Watanzania wanavyoweza kuwekeza katika sekta ya mitambo na kuleta tija kwenye sekta ya madini na viwanda vingine vinavyohusiana kutokana na mazingira wezeshi yaliyowekwa na Serikali.

Kwa upande wake, Meneja wa Kampuni ya Rock Solutions Limited Fabian Mayenga alieleza kuwa Kampuni hiyo imejikita katika usambazaji wa vifaa vya uchimbaji madini kuanzia juu hadi chini ya migodi.

“Kampuni yetu itatoa vifaa vya msingi vinavyohitajika kwa ajili ya uchimbaji wa madini, kama vile nyundo zinazotumika kwenye uchimbaji,  compressors, na vilainishi vya mitambo, huduma zetu ni za kina na zinagusa kila nyanja ya uchimbaji wa madini, kutoka usambazaji wa vifaa vya kisasa kama huduma za kiufundi kama msaada wa ufungaji wa vifaa, matengenezo, na ushauri wa kitaalamu” alieleza Mayenga.

Aliongeza kuwa hivi sasa Kampuni ina wafanyakazi 50 wote wakiwa ni Watanzania na kwamba siku za usoni wataongezeka kufikia hadi 150 kulingana na uzalishaji na kadri biashara itakavyokuwa huku akisisitiza kuwa shughuli rasmi za uzalishaji zinatarajia kuanza mwanzoni mwa mwaka 2025.

Naye, Mkaguzi Mwandamizi wa Hesabu za Migodi kutoka Ofisi ya Afisa Madini Mkoa wa Mwanza Elinami Kimaro alisema kuwa, lengo Serikali ya Tanzania kufanya marekebisho ya Sheria ya Madini mwaka 2017 ni pamoja na kuweka mkazo mkubwa katika kuhakikisha kwamba Watanzania wanashiriki kikamilifu kwenye sekta ya madini kupitia Kanuni ya Local Content. 

“Nitoe wito kwa wenzetu Watanzania waliopo katika nafasi tofauti katika Kampuni zinazomiliki migodi hapa nchini kutoa kipaumbele Watanzania wanaoomba hizo kazi, maana kuna malalamiko tunapokea kuwa wenzetu walioko huko kuna namna wanatukwamisha na kwamba Sheria ya Madini kifungu cha 102 inaelekeza kuwapa kipaumbele wazawa kushiriki katika mnyororo wa thamani wa sekta ya madini, iwe kwa kutoa bidhaa, huduma, au ajira” alisisitiza Kimaro

Kampuni kama JC Gear Group (T) Limited na Rock Solutions Limited zinachangia kwa kiasi kikubwa kufanikisha Kanuni hiyo ya Ushiriki wa Watanzania katika Sekta ya Madini kwa kutoa bidhaa na huduma zinazosaidia kuendeleza sekta ya madini na viwanda vingine nchini.

Kwa kuzingatia michango ya Kampuni hizo katika sekta ya madini, ni wazi kuwa Watanzania  wamejipambanua kama wadau muhimu katika kuhakikisha kuwa sekta ya madini inapata vifaa na huduma za hali ya juu, zinazosaidia kuboresha ufanisi wa kazi na kuongeza tija kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi na kuonesha kuwa Watanzania wana uwezo wa kutoa huduma bora zinazokidhi viwango vya kimataifa, na hivyo kuleta ushindani wa haki na kuongeza ajira kwa wananchi.


 


Machifu nchini wamepongezwa kwa kazi kubwa wanayofanya katika kuungana na Serikali chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Kuimarisha amani na Utulivu nchini.

Pongezi hizo zimetolewa leo Septemba 22,2024 na Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Balozi, Dkt. Pindi Chana (Mb) aliyeambatana na Katibu Mkuu,  Dkt. Hassan Abbasi Mkoani Ruvuma alipokutana na Machifu kutoka makabila mbalimbali ya hapa nchini waliofanya ziara ya kutembelea Makumbusho ya Historia ya Vita vya MajiMaji Mjini Songea kama sehemu ya Maandalizi ya mapokezi ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anayetarajiwa kuitembelea Makumbusho hiyo hapo kesho. 

Mhe. Chana aliwahakikishia Machifu hao kuwa Wizara anayoingoza itaendelea kushirikiana nao  kikamilifu katika Uhifadhi na kuendeleza urithi wa Kihistoria nchini ili watanzania waweze kunufaika na Mazao hayo ya Utalii wa Historia na Malikale. 

Pamoja na kukutana na Machifu hao, Mhe. Balozi Chana amekagua maandalizi ya mapokezi ya Mhe. Rais Samia kwenye Makumbusho hiyo iliyohifadhi Historia adhimu na adimu katika ukombozi wa Tanzania na Afrika kwa ujumla dhidi ya Ukoloni Miaka takribani 119 iliyopita.







Vikundi nane vya Wajasiriamali kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa vimenufaika na mtaji wezeshi kutoka Benki ya CRDB kiasi cha shilingi milioni 101.6 kwa ajili ya kuimarisha biashara zao na kukuza mitaji.

Hafla ya kukabidhi hundi hiyo imefanyika leo  Septemba 18,2024 sambamba na ufunguzi wa semina ya siku moja ya kuvijengea uwezo vikundi vya wanawake wajasiriamali na vijana wanufaika wa programu ya Imbeju katika Halmashauri ya Ludewa ambapo Waziri wa Maliasili na Utalii na Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Njombe, Mhe. Balozi, Dkt. Pindi Chana amefungua rasmi  mafunzo hayo na kuwataka wanufaika kutumia vizuri mafunzo ya ujasiriamali yanayotolewa na Benki ya CRDB.

Vikundi vilivyopokea hundi hiyo ni Faraja Luilo, Hope Women Mlangali, Lake Nyasa, Nipende Group, Tupendane Lupanga, Wanawake Luilo, Wanawake Mwangaza Luilo na Mboga Mboga Group.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Semina hiyo ya Imbeju inayotolewa na CRDB Bank Foundation, Mhe. Chana ameweka bayana kuwa huo ni mwendelezo wa juhudi za Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha anaboresha maisha ya wananchi hasa vijana na wanawake kwa kuweka sera zinazoruhusu uwezeshaji wananchi kiuchumi.

Amesisitiza kuwa ni vyema wananchi hasa wanawake na vijana wakatumia vizuri kila fursa ya mafunzo na kuzingatia mafunzo wanayopewa  ili  kukuza uchumi wao binafsi.

“Uwepo wa Taasisi ya CRDB Bank Foundation Wilayani Ludewa ni fursa kwa wanawake na vijana wa Halmashauri hii kuelimika na kuanza kufanya biashara kwa malengo makubwa yatakayosaidia kukuza kipato cha mtu binafsi, uchumi wa kaya na taifa kwa ujumla” amesisitiza Mhe. Chana

Naye, Meneja wa Benki ya CRDB, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Jenipher Tondi amesema akuwa mafunzo hayo yatasaidia kukuza biashara za wajasiriamali, kutanua mitaji yao na kuimarisha kipato binafsi huku akiwataka kutumia mafunzo hayo vizuri kuimarisha kipato na kukuza Uchumi.

“Programu hii iliyozinduliwa mwaka 2023 inalenga kuboresha maisha ya wananchi na kuchochea ustawi wa jamii” amesisitiza.

Hafla hiyo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Chama na Serikali pamoja na wananchi kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa.










Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Njombe na Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Balozi, Dkt. Pindi Chana (Mb) amezindua rasmi zahanati ya Ivilikinge iliyopo Wilayani Makete Mkoani Njombe sambamba na kukabidhi vifaa mbalimbali vya hospitali vilivyotolewa na Benki ya NMB.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi huo, leo Septemba 16,2024, Mhe. Chana amesema uwepo  wa zahanati hiyo ni miongoni mwa vipaumbele vya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan vya kuhakikisha huduma za afya zinawafikia  wananchi mpaka vijijini.

" Hizi ni baadhi ya huduma tulizoahidi kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi hivyo tunapochagua viongozi tuchague ambao watatuletea maendeleo" amesisitiza Mhe. Chana.

Amesema kuwa kupitia zahanati hiyo wananchi wa Isapulano na vijiji vya jirani watapata huduma  bora za afya na kuwaomba wananchi hao kuhakikisha wanaitumia ipasavyo zahanati hiyo.

Naye, Kaimu Meneja wa Benki ya NMB Kanda ya Nyanda za Juu, Willy Mponzi amesema kwa kuzingatia  juhudi za Rais katika kusimamia upatikanaji wa huduma bora za afya mijni na vijijini, changamoto  za Sekta ya Afya  ni kipaumbele kwa Benki ya NMB kwa sababu afya ni kipaumbele kwa maendeleo ya Taifa lolote.

Kufuatia hatua hiyo,benki ya NMB inakabidhi vifaa mbalimbali vya hospitali kwa zahanati hiyo ikiwemo Vitanda vya kujifungulia (2),Vitanda vya uchunguzi (2),vitanda vya hospitali (5),Magodoro (5),folding screen (4),folding stretcher (2),delivery kit (5),drip stend(5), mashuka 50 na viti vyenye magurudumu (3) vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 9.

Awali, akiwasilisha taarifa ya ujenzi wa mradi huo, Mganga Mkuu wa Zahanati ya Isapulano, Hassan Omar  alisema kuwa mradi huo umegharimu takribani milioni 146.1 ambayo inatokana na michango ya wananchi (milioni 26.5), Wadau wazawa (milioni 6.6, Mbunge wa Jimbo la Makete,Mhe. Festo Sanga (milioni 4) ,Diwani (laki 5 na elfu 30), Benki ya NMB Mabati (milioni 8.5) na Serikali (milioni 100).

Amefafanua kuwa lengo la mradi huo ni kuboresha upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi wa Ivilikinge na vijiji vya jirani, kupunguza umbali wa kufuata huduma kwa mama wajawazito, watoto na wazee.







 


Askari Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA) wametakiwa kujenga mahusiano mazuri na wananchi wanaozunguka Hifadhi ya Ngorongoro ili kuendeleza juhudi za uhifadhi za eneo hilo.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi, Dkt. Pindi Chana (Mb) ameyasema hayo leo Septemba 12, 2024 alipokuwa akizungumza na watumishi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro katika Makao Makuu ya Ofisi za NCAA Wilayani Karatu Mkoani Arusha.

"Tuendelee kuboresha mahusiano kati yetu na wananchi na kuwasikiliza wanapokuwa na maoni au changamoto kwa sababu watatusaidia katika mipango yetu ya uhifadhi" amesisitiza Mhe. Chana.

Aidha, amewataka kuendelea kufuata  maelekezo mbalimbali ya Serikali ikiwa ni pamoja na kuboresha utoaji wa huduma za kijamii kwa wananchi kama geti na vyoo vya wanafunzi.

Amewataka kufanya kazi kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizopo kwa kuwa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ana imani kubwa sana na  NCAA katika kutoa huduma, kukusanya mapato na kuendeleza  uhifadhi.

Pia amewataka kuwa wazalendo na kusimamia vizuri zoezi la kuhama kwa hiari ili zoezi liende vizuri.

Naye, Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi amesema hifadhi hiyo imeongeza idadi ya watalii kwa asilimia 21 kwa takwimu za mwezi Januari hadi Juni, 2024 Watalii wa nje walikuwa 180,000 mpaka 200,000 na zaidi huku akisisitiza kuwa Wizara imeendelea kutimiza wajibu wake katika kuisimamia NCAA.

Ameweka bayana kuwa pamoja na mafanikio hayo Mheshimiwa Rais amefanya azimio kubwa la kutoa asilimia 3 ya mapato kwa ajili ya uhifadhi na asilimia 6 kwa ajili ya kutangaza utalii.

Mapema akizungumza katika kikao hicho Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, Dkt. Elirehema Doriye ameipongeza wizara ya Maliasili na Utalii kwa kuendelea kusimamia vizuri kazi mbalimbali za mamlaka hiyo.








 


Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi, Dkt. Pindi Chana (Mb) amesema Serikali itaendelea kuweka  mikakati madhubuti za kuwalinda wananchi dhidi ya wanyamapori wakali na waharibifu hususan tembo huku akisisitiza kuwa  ni wajibu Serikali kuhakikisha usalama wa wananchi wake.

Ameyasema hayo leo Septemba 6, 2024 alipokutana na baadhi ya Madiwani wa Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Meatu Mkoani Simiyu, leo kwenye ukumbi mdogo wa Pius Msekwa, Bungeni jijini Dodoma.

“Wakati umefika wa kuwalinda wananchi wetu na kuendelea kuchukua tahadhari za kutosha hasa kwenye maeneo ambayo ni korido za wanyamapori na  nimezielekeza taasisi zetu kuweka vibao ili kuwataarifu wananchi wasipite katika maeneo hayo” amesema Mhe. Chana.

Aidha, amesema Wizara ya Maliasili na Utalii inatekeleza mikakati mbalimbali ya kukabiliana na wanyamapori wakali na waharibifu kuhakikisha wananchi wanakuwa salama ikiwa ni pamoja na kuangalia namna ya kuwaelimisha wananchi kupanda mazao ambayo hayavutii tembo kama ufuta, kuvalisha tembo viongozi kola za kuonyesha kundi la tembo linaelekea wapi na kujenga vituo vya askari wanyamapori.

Naye, Mbunge wa Jimbo la Meatu, Mhe. Leah Komanya ameishukuru Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kazi nzuri ya uhifadhi na kupambana na changamoto ya tembo katika Wilaya ya Meatu kwa kuwapatia gari, pikipiki nne na kuwajengea kituo cha Askari Wanyamapori.

 Awali, akiwasilisha taarifa ya Baraza la Madiwani, Diwani wa Kata ya Mwandoya, Mhe. Basu Kayungilo amesema kuwa kumekuwa na athari za wanyamapori wakali na waharibifu kwa wananchi wanaoishi katika vijiji vinavyopakana na Pori la Akiba Maswa na Jumuiya ya Wanyamapori Makao.

Mhe. Kayungilo ameongeza kuwa Baraza hilo liliazimia kuunda timu itakayoonana na Waziri wa Maliasili na Utalii kwa lengo la kupata muafaka wa changamoto hiyo ikiwemo utaratibu wa malipo ya kifuta jasho/machozi pamoja na mgawanyo wa asilimia 25 zinazotolewa kama rufaa ya vijiji vinavyopakana na hifadhi.

Kikao hicho kimehudhuriwa na baadhi ya watumishi waandamizi kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii wanaohusika na masuala ya wanyamapori.