Articles by "JERRYSILAA"
Showing posts with label JERRYSILAA. Show all posts

 


Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Jerry William Silaa (Mb) amesema Tanzania itaendelea kushirikiana na nchi nyingine duniani katika kukuza uchumi wa kidijitali kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa katika sekta ya TEHAMA.

Waziri Silaa aliyasema hayo wakati akifungua kikao kazi cha Jukwaa la Jamii ya Habari Duniani (WSIS) Kanda ya Afrika, kinachofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam, tarehe 9-11 Oktoba 2024.

“Rais Samia amezindua mkakati wa Tanzania ya Kidijitali wa miaka 10 (2024-2034) unaoonesha jinsi Tanzania itakavyojumuisha TEHAMA kwenye uchumi na masuala ya kijamii,” alisema Waziri Silaa.

Aliongeza kuwa, Serikali imefanya uwekezaji mkubwa kwenye miundombinu ya TEHAMA, ikiwa ni pamoja na Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano na ujenzi wa minara ya mawasiliano, pamoja na kuanzisha sera na sheria mbalimbali zinazolenga kuhakikisha Tanzania inashiriki kikamilifu katika uchumi wa kidijitali.

Waziri Silaa alimtaja Rais Samia kama kiongozi aliyewezesha na kutoa maelekezo yanayowezesha Wizara kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi, na hivyo kupelekea Tanzania kuibuka kidedea katika masuala ya TEHAMA.

Aidha, Waziri Silaa alitumia jukwaa hilo kuwakaribisha washiriki wa Kikao kazi hicho kushiriki katika Kongamano la Nane la TEHAMA Tanzania la mwaka 2024, litakalofanyika kuanzia tarehe 13 hadi 17 Oktoba, 2024 jijini Dar es Salaam ambapo mgeni rasmi atakuwa Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. 

Waziri Silaa amebainisha kuwa katika Kongamano hilo masuala ya akili mnemba (AI) na roboti yatapewa kipaumbele, huku akisisitiza umuhimu wa kuongeza uelewa kuhusu teknolojia hizo kutokana na mchango wao katika shughuli za kiuchumi na kijamii.

Aidha, Waziri Silaa alisisitiza kuwa Tanzania ni miongoni mwa vinara wa usalama mtandao Duniani na ikiwa moja kati ya nchi 5 kutoka barani Afrika, akitolea mfano Jarida la Kimataifa la kupima ukomavu wa Usalama Mtandao kwa kila nchi (Global Cybersecurity Index) lililotolewa tarehe 23 Septemba, 2024 ambalo hutolewa kila miaka minne (4) na Shirika la Mawasiliano Duniani (ITU). 

Alifafanua kuwa ulinzi wa kimtandao unapaswa kuwa kipaumbele, kwani kutokana na maendeleo ya kiteknolojia na ukuaji wa uchumi wa kidijitali shughuli nyingi, ikiwemo huduma za kifedha na uhifadhi wa taarifa binafsi, zinafanyika mtandaoni.

Kwa kuimarisha usalama wa mtandao, Tanzania ina Sheria nzuri za Usalama Mtandaoni, mikakati mizuri ya Usalama Mtandao na uwepo wa Kitengo cha TZ-CERT kilichopo Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), ambacho kinajihusisha na ulinzi wa mtandao na kubaini mashambulizi kabla hayajatokea kwa ujumla ni baadhi ya masuala yaliyochangia kuifanya Tanzania kuibuka kinara katika Usalama Mtandao Duniani.

Tanzania ina mifumo kadhaa ya kisheria na udhibiti inayoongoza sekta ya mawasiliano na TEHAMA ili kuhakikisha huduma ya intaneti ya kasi inawafikia wananchi wote huku Serikali ikiendelea kuhakikisha usalama katika matumizi ya mtandao kwa wananchi na wadau wote wa ndani na nje ya nchi. 

Akihutubia wakati akifungua Kongamano la C2C (Connect2Connect) leo Septemba 18, 2024 jijini Arusha, Waziri wa Habari Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Jerry William Silaa (Mb) amesema kuwa Serikali inawekeza katika Sekta ya TEHAMA kwa kuwa ni nyenzo muhimu ya nchi kuwa na uchumi wa kidijitali.

Amesema kuwa Mkutano wa Connect2connect kwa mwaka 2023 uliofanyika katika Hoteli ya Madinat Al Bahr huko Zanzibar na kuhudhuriwa na washiriki kutoka nchi 20 uliangazia juhudi za pamoja zinazohitajika kuziba pengo la kidigitali na kukuza maendeleo endelevu barani Afrika.

Mhe. Silaa ametoa rai kwa washiriki wa Kongamano la mwaka huu kuchangia mawazo na kujadili kwa kina namna ya bora ya kuunganisha nchi za bara la Afrika na miundombinu ya kidijitali ili kuwezesha maendeleo endelevu ya uchumi wa kidigitali. 

Naye Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Extensia Limited, Bw. Tariq Malik amesema kuwa Kongamano la mwaka huu chini ya kauli mbiu ya 'Maunganisho yenye manufaa' unalenga kujadili vipengele muhimu vya maendeleo ya TEHAMA vinavyosukuma ukuaji wa uchumi, ujumuishi wa kijamii, na maendeleo endelevu barani Afrika. 

Ameongeza kuwa mada zitakazojadiliwa ni pamoja na hali ya sekta, athari za uchumi wa kidijitali kwa Tanzania, na nafasi ya vituo vya data katika mabadiliko ya kidijitali ili kubadilishana maarifa muhimu kuhusu mipango ya ukuaji wa baadaye na mfumo wa ikolojia ya TEHAMA ili kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Bw. Mohammed Khamis Abdulla amesema kuwa Kongamano la C2C limekuwa taa ya maendeleo, likituongoza kuelekea siku zijazo ambapo teknolojia inakuwa kichocheo cha maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Ameongeza kuwa kupitia ushirikiano wa Wizara hiyo, kampuni ya Extensia ya Uingereza na washirika wengine matokeo makubwa yameonekana katika kupanua wigo wa miundombinu ya mawasiliano nchini ambapo kwa mwaka huu Kongamano hilo litahusisha mahitaji muhimu ya miundombinu na uunganishaji wa mipakani, ambayo ni muhimu sana kwa kuharakisha ajenda ya TEHAMA ya Afrika.

Katika hatua nyingine Mhe. Silaa amewakaribisha washiriki wa kongamano hilo kushiriki katika Kongamano la Nane la mwaka la TEHAMA litakalofanyika jijini Dar es Salaam, tarehe 13 hadi 17 Oktoba, 2024 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa  Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan lenye kaulimbiu "Kufungua Nguvu ya Akili Mnemba na Roboti kwa Mabadiliko ya Kiuchumi na Kijamii".





Kampuni ya simu za mkononi Airtel kupitia kwa Mkurugenzi wa Biashara Joseph Muhele amesema kuwa mtandao huo mwaka huu 2024 unaendelea kufangua huduma  zake za mawasiliano katika miji na Vijiji ambapo kwa mjini kuwezesha kupata huduma ya 3G,4G,5G na Kampuni inaendelea na Uwekezaji na upanuzi wa mtandao maeneo ya Vijiji ili kuwezesha kupata huduma ya 3G 4G na 5G.

Aidha ameeleza kuwa kwa mwaka 2013 kampuni hiyo ilifunga mtambo mpya Submarinecable ambao ni mkubwa wenye uwezo wa kupokea na kutumia data kwa kiwango kikubwa ,uwekezaji huo umefanywa kwa ajili ya Watanzania na nchi jirani kwajili ya mawasiliano. 

Muhele ameendelea kufafanua kuwa lengo la Mkutano huo wa 8 ni kuwaleta Wadau wote pamoja katika teknolojia, ambapo kampuni hiyo inaendelea kuvifikia Vijiji vyote ambavyo havijafikiwa na huduma hiyo ambapo sasa wanajenga huduma ya 5G kwa ajili ya wateja Ujenzi ambao unaenda sambamba na kuhakikisha gharama zinakuwa nafuu.

Kwa upande wake Waziri wa Habari ,Mawasiliano Teknolojia ya habari Jerry Slaa akifungua kogamano hilo la siku mbili (Connect2Connect Summit) ambapo limewakutanisha wadau wote wa Mawasiliano nchini pamoja na wadau wengine ambapo amesema Watanzania zaidi ya Mil.75 wana simu za mkononi 35% wanamtandao wa intaneti ambapo mwaka mei 2023 Serikali ilizindua mkakati wa ujenzi wa minara 758 kupitia USAF mfuko uliotengenezwa na seeikali ambapo kila mtoa huduma anachangia ili kupeleke huduma 

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kongamano hilo Mhe. Always alisema minara mingine 636 mradi huo utaanza Oktoba 2024 huku akiwatak wananchi wanaofanya shughuli zao kupitia mitandao wapo salama zaidi na Serikali imetunga Sheria ya kulinda data za mtu binafsi katika matumizi ya mtandao na kila mtumiaji analindwa na hairuhusiwi kutumia data za mtu bila ridhaa yake.

Aidha Waziri Slaa,amesema hadi sasa 89% ya Watanzania wanapata huduma mtandao lengo likiwa Wananchi wote wapate huduma ya mtandao  wa Internet,simu ,habari ,redio na televisioni yakuwemo maeneo ya Utalii ambayo yamepewa kipaumbele 

Kwa upande wake injinia Cecil Mkomola Francis  mkurugenzi wa ufundi na Uendeshaji wa Shirika la mawasiliano Tanzania TTCL amesema wanadhamana kubwa ya kutoa huduma ya mawasiliano, kupitia mkongo wa mawasiliano wa Taifa kwani wameendelea kufanya kazi na kuhakikisha kuwa nchi inaongea kwa kuunganishwa mikoa wilaya ambapo jumla ya wilaya 106 zimeunganishwa Tanzanzania bara Kati ya wilaya 139,mkongo huo ndio kiungo kikuu cha  Mawasiliano na Intaneti. 

Amesema kuwa kazi kubwa waliyonayo kama Shirika ni kutoa mchango mkubwa wa mawasiliano kuhakikisha kwamba wanafikisha huduma kwa Wananchi na kupungiza gharama za matumizi

upande wake  ,Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Shirika la mhandis Francis Mkomola,amesema Shirika hilo lina dhamana kubwa ya kutoa huduma bora za mawasiliano kupitia mkongo wa taifa  ambao ulianza kutekeleza mwaka 2013.

Vilevile wameunda mkongo huo na nchi jirani za Kenya,Uganda ,Rwanda,Burundi ,Zambia,Malawi na kuna maunganusho yanayoenda kwenye mpaka na Msumbijina sasa wanaanza kushughulikia maunganusho na nchi ya DRC Congo,kupitia ziwa Tanganyika hadi mji wa Kalemii Nchini DRC pia wanashugulikia maunganisho  kwenda kwenye kituo  kilichopo baharini hadi Mombasa Nchini Kenya.

TTCL inaendelea kutoa mchango wa mawasiliano kuhakikisha mkongo unaojengwa inakuwa na ubora wa hali ya juu kwa lengo la kufikisha huduma  kwa Wananchi na kupunguza gharama ambapo Tanzania ni kiunganishi kikuu cha Mawasiliano kwenye ukanda wa nchi za EAC na SADC, wilaya ambazo  hazijaunganishwa kwenye mkongo wa taifa zitaunganishwa mwaka huu na wakandarasi wapo wanaendelea na shughuli hiyo

Mkutano huu umehusisha wadau wote wa mawasiliano nchini  Tanzania chini ya kauli mbiu ya ‘Meaningful Connectivity’






Mbunge wa Jimbo la Ukonga ambaye pia ni Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Jerry Silaa amewataka wanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM) katika Jimbo hilo, kushirikiana na kuyasema mambo mazuri yote yanayofanywa na Serikali, ikiwepo utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Amesema katika kipindi cha miaka mitatu ya Rais Samia Suluhu Hassan madarakani ameweza kuimarisha miundombinu ya barabara, hospitali, shule na huduma nyingi za kijamii hivyo katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajia kufanyika Novemba 27, ni muhimu wananchi wakachagua viongozi wanaotokana na chama hicho.

Mhe. Silaa ameyasema hayo leo Septemba 09, 2024, katika Mkutano Mkuu wa Kata mbili za Ukonga na Gongo la Mboto, na semina kwa Viongozi wa CCM kuhusu uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

“Nimekuja tukumbushane kwamba tunao wajibu wa kuhakikisha tunayasema hadharani mambo makubwa yaliyofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan, hapa Ukonga kuna mambo tulikuwa tunayaona ni ndoto, ametujengea barabara nzuri zikiwepo za mwendo kasi, tuna maji ya uhakika, sasa tunaenda kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa, tujipange kuyanadi haya katika uchaguzi huu” amesema Mhe. Silaa.

Awali akimkaribisha Mhe. Silaa kuhutubia katika Mkutano huo, Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM Wilaya ya Ilala na Mjumbe wa Kamati ya Siasa Wilaya Mhe. Juma Mizungu amesema, katika kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa, wanachama wa chama hicho wanapaswa kujitokeza kwa wingi kupiga kura pamoja na kuwachagua viongozi wa CCM.

“Huu ni mwaka wa uchaguzi, zawadi tunayopaswa kumpa mheshimiwa Rais wetu Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha Kata zote 13 za Jimbo la Ukonga zinaenda kwa CCM, nawaomba sana ndugu zangu, tujitokeze kwa wingi kupiga kura kuchagua viongozi wa chama chetu” amesema Mhe. Mizungu.    



Na Eleuteri Mangi, Dodoma

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Jerry Silaa ametoa siku 90 kwa Bodi ya Usajili ya Wathamini (VRB) kuzindua mihuri ya Wathamini ya kisasa yenye alama za kidijiti ili wananchi wajiridhishe kazi yao inayofanywa na mtaalam aliyesajiliwa kisheria.

Waziri Silaa amesema hayo Juni 7, 2024 jijini Dodoma wakati wa mahafali ya Wathamini ya tatu ya Bodi ya       Usajili wa Wathamini inayosimamiwa na Bodi ya Usajili wa Wathamini.

“Namwelekeza Mwenyekiti wa Bodi ndani ya siku 90 kuanzia leo napenda kuona bodi inazindua mihuri ya wataaalam yenye Barcode kwa maana ya kuwa na alama za ulinzi za kielekroniki ambao utaunganishwa na mfumo wenu wa kutambua Wathamini ili kusimamia misingi ya taaluma na weledi katika kutekeleza majukumu yao.” amesema Waziri Silaa.

Ameongeza kuwa mihuri ya Wathamini itasaidia wananchi wa kawaida kuwatambua wathamini kwa kuwa kila mmoja atakuwa na alama ambazo hazitafanana na mwingine hatua itakayowasaidia kutambua kuwa kazi hiyo imefanywa na mtaalam ambaye anatambulika kisheria na kumchukulia hatua za kinidhamu kama atakiuka taaluma yake na misingi ya kazi yake.

Aidha, Waziri Silaa amewaasa wahitimu wa hao kufanya kazi yao ya Uthamini kwa kumtanguliza na kumheshimu Mungu na kuwatumikia watanzania katika kupata huduma za uthamini kwa haki kwa kufuata misingi ya taaluma na sheria za nchi.

Awali akimkaribisha Waziri wa Ardhi, Nyumba na Makazi Mhe. Jerry Silaa wakati wa uzinduzi wa Bodi hiyo, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Mhandisi Anthony Sanga amewasisitiza wajumbe hao kusimamia taaluma na weledi katika kazi ya uthamini kwa mujibu wa taaluma yao na milango ya wizara ipo wazi wakati wote waendelee kushirikiana ili kuleta maandeleo endelevu kwa taifa na watu wake na kuleta mabadiliko chanya ambayo yataacha alama katika kipindi cha uongozi wao.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili ya Wathamini Bw. Zidikheri Mgaya Mudeme amemhakikishia Waziri Silaa na Menejimenti ya Wizara ushirikiano wakati wote wa kutekeleza majuku yao hatua itayowasaidia Bodi hiyo kusimamia maadili ya taaluma ya Uthamini.

Mahafali hayo yamehudhuriwa na wahitimu 91 ambao wanatambuliwa na Bodi ya Usajili wa Wathamini ambao wamekula kiapo cha uadilifu katika kutekeleza majukumu yao kwa kwa haki.

 



Na Eleuteri Mangi, WANMM, Dodoma

 

 

Makamishna wa Ardhi Wasaidizi nchini wametakiwa kufanya kazi kwa uadilifu wakitabua kila maamuzi wanayoyafanya yanaishi na wawe na uwezo wa kuelezea wamefikiaje maamuzi hayo ili watu wengine wakipitia watambue kweli kazi ya kuridhisha imefanyika.

 

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Jerry Silaa wakati akiongea na Makamishna hao kutoka mikoa yote Tanzania Bara jijini Dodoma Mei 28, 2024 mara baada ya bajeti ya Wizara hiyo   kupitishwa na Bunge Mei 27, 2024.

 

“Mikoa yote niliyopita, naridhishwa sana na utendaji wenu wa kazi. Nilazima huko mikoani msimamie suala la ardhi, nawapa mfano wa Kamishna wa Mwanza anafanya kazi vizuri, anashauri na taarifa yake kwenye kumbukumbu, government moves on paper. Ukiona Waziri yeyote anakuagiza jambon a unaona limekaa kushoto mwandikie dokezo kwa Kamishna wa Ardhi” amesema Waziri Silaa.

 

Amesema ni lazima uwepo utaratibu mzuri wa kufanyakazi kama wizara kwa kuwapa watumishi mafunzo ya kufanyakazi kikamilifu ili kuwahudumia wananachi na kusisitiza kuwa kuna kazi kubwa ya kujipanga kufanyakazi kama taasisi.

 

Aidha, Waziri Silaa amesema Kliniki za Ardhi zitaendelea katika mikoa yote ili kuendelea kutatua na kumaliza migorogoro ya ardhi katika maeneo mbalimbali nchini.

 

Akimkaribisha Waziri kuongea na Makamishna hao, Katibu Mkuu Wizara hiyo Mhandisi Anthony Sanga amewakumbusha kuhusu misingi sita ya kufanyakazi aliyotoa Mhe. Waziri akijibu hoja za Wabunge wakati kupitisha bajeti ya wizara hiyo kuwa ili watendaji wa wizara wazingatie kwenye utendaji wao wa kazi.

 

Misingi hiyo ni uharaka wa jambo wakati unafanyakazi ya umma kwa sababu wananchi wanaohudumiwa wanahitaji kwenda kufanya shughuli zao, msingi wa pili ni kujali na kutoa huduma ni lazima kuwajali watanzania na kuwahudumia kwa upendo, msingi wa tatu ni nidhamu ya kujali muda, kujali na kuheshimu watu, msingi wa nne ni lazima kuwasikiliza na kuwaelewa, ukimsikiliza mwananchi ni lazima umsikilize kwa makini ili umwelewe na kumtatulia tatizo lake, msingi wa tano ni lazima kuwa na majawabu ya matatizo ya watanzania na msingi wa sita ni lazima kufanyakazi kwa uadilifu.