Articles by "Babati"
Showing posts with label Babati. Show all posts



Na John Walter -Babati

Mahakama ya Mwanzo Babati imewahukumu kifungo cha miezi miwili gerezani vijana wawili, Abubakari Semburi (18) na Abdul Hamza (18), wakazi wa Maisaka, kwa kosa la kuharibu mali ya Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Babati (BAWASA).

Washitakiwa hao walikutwa na hatia ya kuharibu mita za maji za BAWASA na kuziuza kama chuma chakavu katika kesi iliyowasilishwa na mlalamikaji, Sebastian Honorath, ambaye ni Meneja wa Ufundi wa BAWASA. 

Hukumu hiyo ilitolewa Januari 10, 2025, na Mheshimiwa Hakimu Kangida Kalembo, kwa mujibu wa kifungu cha 326(1) cha Sheria ya Kanuni za Adhabu, sura ya 16, marejeo ya mwaka 2022.

Wawili hao walikutwa na mita hizo  Desemba 24, 2024, majira ya saa saba mchana, katika maeneo ya Maisaka, mjini Babati.

Meneja wa Huduma kwa Wateja wa BAWASA, Rashidi Chalahani, amesema wamekuwa wakifuatilia kwa muda mrefu visa vya wizi wa mita za maji kutoka kwa wateja wao ambapo uchunguzi walioufanya ulipelekea kugundua mita hizo zikiwa zimeuzwa kwenye eneo la biashara ya chuma chakavu, hatua iliyosababisha kufunguliwa kwa kesi hiyo mahakamani.

Bw. Chalahani ametoa wito kwa jamii kutambua kuwa mita za maji ni mali ya umma na zinapaswa kuheshimiwa na kutunzwa. 

Aidha, amewataka wananchi kutoa taarifa kwa mamlaka husika endapo wataona uharibifu au uhujumu wa miundombinu ya maji. 

Amesema vitendo kama hivyo vinakwamisha juhudi za serikali za kuhakikisha huduma ya maji inawafikia wananchi wote.

Hukumu hii ni onyo kwa wale wanaojihusisha na uharibifu wa miundombinu ya umma, huku ikisisitiza umuhimu wa kushirikiana katika kulinda rasilimali za taifa.

 




Na John Walter-Babati

Mkuu wa wilaya ya Babati Lazaro Twange amekabidhi pikipiki nane za awamu ya kwanza kwa  watendaji wa kata nane za Halmashauri ya wilaya Babati zilizonunuliwa na serikali kwa ajili ya kurahisisha majukumu yao katika kata.

Mkuu wa wilaya amesema ni mapinduzi makubwa yanayofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan ambapo mwaka jana katika wilaya ya Babati alikabidhi pikipiki Zaidi ya hamsini kwa maafisa ugani.

Twange amesisitiza nidhamu katika matumizi ya piki piki hizo kwa kuziendesha kwa kuzingatia taratibu zote za usalama bara barani.

Pikipiki hizo nane zilizokabidhiwa kwa watendaji leo Machi 6,2023 zimenunuliwa na serikali kupitia ofisi ya Rais TAMISEMI, fedha zilizotokana na sehemu ya kodi ya majengo inayokusanywa na hazina.

Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Babati Anna Mbogo,  amesema wameanza kuzigawa kwenye kata nane za pembezoni ikiwemo Qash, Gidas, Duru,Secheda,Dabil, Qameyu,Magara na Nkaiti.

Mbogo amewataka watendaji hao wakazitumie pikipiki hizo katika shughuli za serikali na kuzitunza kwa kuzifanyia marekebisho ya mara kwa mara.