NA EMMANUEL MBATILO, BAGAMOYO
WAZIRI wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Zanzibar, Dkt. Riziki Pembe Juma, akiambatana na viongozi wengine wa wizara hiyo, ametembelea Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) kwa lengo la kujadili maeneo ya ushirikiano yatakayosaidia kupanua fursa za mafunzo ya sanaa na utamaduni kwa wananchi wa Zanzibar.
Katika ziara hiyo iliyofanyika Novemba 16, 2026, Dkt. Riziki amependekeza kuimarishwa kwa ushirikiano kati ya TaSUBa na wizara hiyo ili kuweka utaratibu wa kutoa mafunzo ya sanaa na utamaduni Zanzibar kwa kutumia wakufunzi kutoka taasisi hiyo.
Amesema hatua hiyo itasaidia kupunguza gharama zinazowakabili wanafunzi wa Zanzibar wanaotamani kujiunga na TaSUBa lakini wanashindwa kutokana na gharama za usafiri na maisha wanapokuwa Bagamoyo kwa kipindi chote cha masomo.
" Kupitia ushirikiano wetu, tunaweza kuwa na kozi ambazo wakufunzi wa TaSUBa watakuja kuzifundisha Zanzibar. Hii ni nafasi nzuri kwa TaSUBa kuwa na tawi,” amesema Dkt. Riziki.
Aidha, amependekeza TaSUBa kuanzisha mfumo wa mafunzo kwa njia ya mtandao (Online Courses) utakaowawezesha watu wasiokuwa na nafasi ya kufika chuoni kupata elimu na ujuzi katika fani mbalimbali za sanaa na utamaduni.
Amesema mfumo huo utakuwa fursa muhimu pia kwa wasanii maarufu wanaotaka kujiendeleza kielimu lakini wanakabiliwa na changamoto ya kuhudhuria masomo chuoni kutokana na majukumu yao ya kikazi na mazingira yanayoambatana na umaarufu wao.
“Kipaji peke yake hakitoshi bila kunolewa. Kipaji kinapoendelezwa kwa kupewa elimu, uwezo na ujuzi, kinaweza kuwa na manufaa makubwa kwa jamii, ikiwemo kuchochea maendeleo ya kiuchumi,” amesisitiza.
Vilevile, Dkt. Riziki ameipongeza TaSUBa kwa mchango wake katika kuzalisha na kuendeleza wataalamu na wasanii mbalimbali katika tasnia ya sanaa, akieleza kuwa taasisi hiyo ina nafasi muhimu katika kukuza vipaji na kuimarisha sekta ya sanaa na utamaduni.
Kwa upande wake, Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo anayeshughulikia Mipango, Fedha na Utawala, Dkt. Benignus Mbiro, amesema ziara hiyo imefungua fursa kwa TaSUBa kupanua wigo wa utoaji wa mafunzo kwa kuangalia uwezekano wa kuanzisha kampasi nyingine Zanzibar.
Amesema ujio wa ujumbe huo ni fursa kwa pande zote mbili kubadilishana mawazo, kuimarisha ushirikiano na kujifunza shughuli zinazotekelezwa na kila upande ili kubaini namna bora ya kuongeza wigo wa ufundishaji wa sanaa na utamaduni.
Ameeleza kuwa ushirikiano huo unaweza kuwa hatua muhimu katika kuimarisha upatikanaji wa mafunzo ya sanaa na utamaduni na kuwafikia wananchi wengi zaidi wa Zanzibar.

Post A Comment: