Watendaji wa uchaguzi wamesisitizwa kuheshimu viapo vyao na kutekeleza majukumu kwa kuzingatia Katiba, sheria na kanuni wakati wote wa utekelezaji wa majukumu yao.

Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Jacobs Mwambegele leo tarehe 02 Novemba, 2026 mkoani Dodoma katika Halmashauri ya Chamwino wakati akifunga mafunzo ya watendaji wa uchaguzi.

Mafunzo hayo ni sehemu ya mchakato wa maandalizi ya uchaguzi mdogo wa ubunge kwenye Jimbo la Chamwino Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino, Mkoa wa Dodoma na Kata 11 za Tanzania Bara unaotarajiwa kufanyika tarehe 04 Novemba, 2026.

“Ninawasisitiza kuheshimu viapo vyenu kwa nafasi mlizoteuliwa, tekelezeni majukumu yenu kwa kuzingatia Katiba ya Nchi, sheria za uchaguzi na kanuni zake, kanuni za maadili ya uchaguzi na maelekezo mbalimbali yanayotolewa na yatakayotolewa na Tume katika kipindi hiki cha uchaguzi,” amesema Jaji Mwambegele.

Amewaasa watendaji hao kuhakikisha kuwa pamoja na uzoefu ambao baadhi yao wanao katika uendeshaji wa uchaguzi, wanaepuka kufanya kazi kwa mazoea kwa kuwa kila uchaguzi unatofautiana na uchaguzi mwingine.

Uchaguzi huo mdogo wa Ubunge katika Jimbo la Chamwino utafanyika sambamba na kata 11 za Tanzania Bara ambazo ni Nonde halmashauri ya Jiji la Mbeya, Lugenge, Halmashauri ya Mji Njombe; Bargish, Halmashauri ya Mji Mbulu; Makole, Halmashauri ya Wilaya ya Muheza; Mwera, Halmashauri ya Wilaya ya Pangani na Oldonyosambu, Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro.

Nyingine ni Igalula iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Uyui; Shelui, Halmashauri ya Wilaya ya Iramba; Mvumi, Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa; Nyarero, Halmashauri ya Wilaya ya Tarime na Ilolangulu, Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe.
Share To:

OSCAR ASSENGA

Post A Comment: