GENEVA, Uswisi: Tanzania imefafanua kuwa mfumo wake wa kisheria hautambui jamii za asili, watu wa asili na ardhi za mababu, ikisisitiza kuwa wananchi wote ni raia wenye haki sawa bila kujali kabila, asili, mila, dini, rangi au hali zao za kijamii.
Ufafanuzi huo umetolewa na Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya UNESCO ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Profesa Hamisi Masanja Malebo, aliyewasilisha hotuba kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Mapitio ya Hali ya Haki za Binadamu (Universal Periodic Review – UPR) yanayofanyika katika Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa, Geneva, Uswisi, Novemba 5, 2026.
Katika hotuba hiyo, Profesa Malebo amesema Tanzania ina zaidi ya makabila 120 yanayounda jamii yenye utajiri wa lugha, mila, tamaduni na historia mbalimbali.
Amebainisha kuwa jamii za Tanzania zinawakilisha familia kuu nne za lugha za Afrika ambazo ni Khoisan, Cushitic, Bantu na Nilotic, zikiwa na historia tofauti za uhamaji na mwingiliano wa kijamii uliochangia kuunda jamii za sasa.
Akifafanua kuhusu utambuzi wa jamii za asili (Indigenous Peoples) na ardhi za mababu (Ancestral Land), amesema Katiba na sheria za ndani za Tanzania hazitambui kundi maalumu la kisheria la watu wa asili wala aina tofauti ya ardhi inayotambulika kisheria kama ardhi za mababu.
Amesisitiza kuwa msimamo wa Serikali ni kwamba wananchi wote ni raia wenye haki sawa, bila kujali kabila, asili, mila, dini, rangi au hali zao za kijamii.
Katika hotuba hiyo, ameeleza pia muktadha wa kihistoria kuhusu uhamaji wa jamii mbalimbali nchini, ikiwemo Wamasai, na mwingiliano wao na makundi mengine katika maeneo mbalimbali ya Tanzania.
Kwa mujibu wa maelezo yaliyowasilishwa, uhamaji wa kihistoria wa Wamasai kuelekea kusini ulihusisha mwingiliano na migogoro kuhusu matumizi ya ardhi na maeneo ya malisho kati ya jamii mbalimbali.
Ametaja pia makundi ya Khoisan, Cushitic na Bantu, pamoja na jamii za Wadatoga, akieleza kuwa historia ya makazi na mwingiliano wa jamii hizo ni sehemu ya muktadha wa mijadala kuhusu haki na madai ya ardhi.
Kuhusu changamoto zinazohusishwa na masuala hayo, Profesa Malebo amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kuzishughulikia kwa kuzingatia misingi ya utawala wa sheria, heshima kwa haki za binadamu na utawala bora, huku ikilinda utu, maisha na mila za wananchi.
Katika sehemu nyingine ya hotuba hiyo, ameeleza kuwa Serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, inaendelea kuimarisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi sambamba na kulinda haki za binadamu.
Ametaja uhuru wa kujieleza, uhuru wa kutembea na haki ya kukusanyika kwa amani kuwa miongoni mwa haki zinazopaswa kuheshimiwa kwa mujibu wa Katiba na mikataba ya kimataifa na kikanda ambayo Tanzania imeridhia.
Aidha, Tanzania imesisitiza umuhimu wa Baraza la Haki za Binadamu kuzingatia misingi ya ulimwengu wote, kutokuwa na upendeleo, usawa na kutobagua katika kushughulikia masuala ya haki za binadamu.
Ushiriki wa Profesa Malebo katika ujumbe wa Tanzania unaonesha nafasi ya Tume ya Taifa ya UNESCO katika mijadala ya kimataifa inayohusisha maeneo ya kazi za UNESCO, yakiwemo utamaduni, lugha, urithi wa jamii, mawasiliano na upatikanaji wa taarifa.
Kupitia ushiriki huo, Tume inaendelea kushiriki katika mijadala inayolenga kuendeleza uelewa kuhusu umuhimu wa kuhifadhi urithi wa kitamaduni, kuthamini utofauti wa jamii na kukuza heshima kwa haki na utu wa binadamu.
Mapitio ya Hali ya Haki za Binadamu (UPR) ni utaratibu wa Umoja wa Mataifa unaofanyika chini ya Baraza la Haki za Binadamu, ambapo nchi wanachama huwasilisha taarifa kuhusu hatua walizochukua katika kukuza na kulinda haki za binadamu, hupokea mapendekezo kutoka kwa nchi nyingine na kueleza hatua wanazokusudia kuchukua katika kuimarisha utekelezaji wa haki hizo.




Post A Comment: