Waziri wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga (Mb), amesema sekta ya viwanda na biashara ni miongoni mwa nguzo muhimu za uchumi wa Taifa, ikichangia asilimia 15 ya Pato la Taifa na kutarajiwa kuendelea kukua kwa wastani wa asilimia sita kila mwaka.

Waziri Kapinga ameyasema hayo Novemba 2, 2026, jijini Dodoma, wakati akifungua Maonesho ya bidhaa na huduma za viwanda na Biashara sambamba na Huduma za Kliniki za Biashara yanayofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete (JKCC), kuelekea uzinduzi wa Sera ya Maendeleo Endelevu ya Viwanda ya mwaka 2025 pamoja na Sera ya Maendeleo ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati ya mwaka 2003, Toleo la mwaka 2025, zitakazozinduliwa Novemba 4, 2026.

Amesema maonesho hayo ni sehemu ya juhudi za Serikali kuimarisha sekta ya viwanda na biashara kwa kuweka mazingira yanayowezesha kukuza uzalishaji, kuongeza thamani ya bidhaa za ndani na kupanua masoko ya bidhaa za Tanzania.

Waziri Kapinga amesisitiza kuwa ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi ni muhimu katika kufikia azma ya kuwa na uchumi mkubwa zaidi, huku sekta ya viwanda na biashara ikiendelea kuwa chanzo muhimu cha ajira na fursa za kiuchumi kwa wananchi.

Aidha, amewahimiza wananchi kutembelea maonesho hayo ili kujionea bidhaa zinazozalishwa nchini, teknolojia zinazotumika viwandani pamoja na ubunifu wa wajasiriamali na wafanyabiashara, akieleza kuwa Serikali inalenga kuhakikisha bidhaa za Tanzania zinaongezwa thamani ili kukidhi mahitaji ya soko la ndani na kushindana katika masoko ya kimataifa.

Katika maonesho hayo, taasisi mbalimbali zilizo chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara zimeshiriki, zikiwemo Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO), Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade), Wakala wa Vipimo (WMA), Tume ya Ushindani (FCC), Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Taasisi ya Utafiti wa Viwanda Tanzania (TIRDO), Shirika la Maendeleo ya Viwanda Vidogo (TEMDO), Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade), pamoja na taasisi nyingine za sekta hiyo.

Aidha, Waziri Kapinga ametoa pongezi na shukrani kwa kampuni na wadau mbalimbali walioshiriki katika maonesho hayo na kuunga mkono maendeleo ya sekta ya viwanda na biashara, zikiwemo ALAF, Wilmar Pasta, KEDA, Lodhia, Pepsi, Coca-Cola, Goodwill na kampuni nyingine. 

Pia alitumia fursa hiyo kuwatambua na kuwashukuru wasanii waliojitokeza kushiriki na kuhamasisha wananchi pamoja na makundi mbalimbali kushiriki katika shughuli za ufunguzi wa maonesho hayo.

Maonesho hayo pia yamehudhuriwa na wanafunzi kutoka Chuo cha Biashara (CBE), viongozi waandamizi wa Wizara, wakurugenzi na wakuu wa taasisi zilizo chini ya Wizara pamoja na wadau mbalimbali wa sekta ya viwanda na biashara.





Share To:

OSCAR ASSENGA

Post A Comment: