📌 Utekelezaji Mradi wa TAZA wafikia asilimia 95

📌 Ili kuukamilisha mradi kutakuwa na katizo la muda la umeme Novemba 14 na 15 katika baadhi ya maeneo ya Kanda ya Kaskazini, Magharibi na Ziwa.


Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limefikia hatua muhimu katika utekelezaji wa Mradi wa Usafirishaji Umeme wa Tanzania na Zambia (TAZA), ambao sasa umefikia asilimia 95 ya utekelezaji na unatarajiwa kuiwezesha Rukwa kuunganishwa na gridi ya Taifa ifikapo Desemba 5, 2026, hatua itakayoboresha upatikanaji na uhakika wa huduma ya umeme mkoani humo.

Mradi huo utaiwezesha Rukwa kuacha kutegemea umeme kutoka Zambia na badala yake kupata umeme kupitia gridi ya Taifa ya Tanzania. Hatua hiyo ni muhimu katika kuimarisha usalama wa upatikanaji wa nishati, kuunga mkono ukuaji wa shughuli za kiuchumi na kijamii na kufungua fursa zaidi za maendeleo kwa wananchi na wawekezaji.

Ili kufanikisha hatua za mwisho za mradi huo, TANESCO imetangaza kuwapo kwa katizo la muda la umeme Novemba 14 na 15, 2026, katika baadhi ya maeneo ya Kanda ya Kaskazini, Magharibi na Ziwa, kuanzia saa 12:30 asubuhi hadi saa 11:30 jioni kwa kila siku.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma leo, Novemba 12, 2026, Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Usambazaji Umeme, Mhandisi Timothy Mgaya, amesema katizo hilo ni sehemu ya maandalizi ya kitaalamu yanayohitajika ili kuwezesha mkandarasi kukamilisha kazi zilizobaki na kuiweka miundombinu katika hali ya utayari wa kuanza kutumika.

“Kazi ilipofikia inatulazimu kuzima umeme kwa siku ya Jumamosi na Jumapili katika mikoa ya Kanda ya Kaskazini, Kanda ya Magharibi na Kanda ya Ziwa ili kumruhusu mkandarasi kumalizia kazi,” amesema Mhandisi Mgaya.

Mikoa itakayoathirika na katizo hilo ni Singida, Manyara, Arusha, Kigoma, Kagera, Tabora, Shinyanga, Simiyu, Geita, Mwanza na Mara.

Ameongeza kuwa TANESCO imejipanga kuhakikisha kuwa taarifa kwa wateja wake zinawafikia wateja wake na kazi hizo zinakamilika ndani ya muda uliopangwa ili kupunguza usumbufu kwa wananchi na kurejesha huduma kwa wakati.

Akifafanua manufaa ya mradi huo, Meneja wa Mradi wa TAZA, Mhandisi Deogratius Nyamtumbaga, amesema kukamilika kwa mradi kutaiwezesha Rukwa kupata umeme kutoka katika gridi ya Taifa ya Tanzania badala ya kutegemea umeme unaotoka Zambia kama ilivyo sasa.

“Hadi kufikia Desemba 5, 2026, Mkoa wa Rukwa utakuwa umeunganishwa kwenye gridi ya Taifa,” amesema Mhandisi Nyamtumbaga.

Mradi wa TAZA unahusisha ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovolti 400 kutoka Iringa hadi Sumbawanga mkoani Rukwa. Miundombinu hiyo itaongeza uwezo wa usafirishaji wa umeme na kuimarisha mfumo wa usambazaji wa nishati nchini.

Kukamilika kwa mradi huo ni hatua muhimu katika kuimarisha miundombinu ya nishati nchini, kuongeza uhakika wa upatikanaji wa umeme na kuweka mazingira bora ya uwekezaji, uzalishaji na ukuaji wa uchumi.















Share To:
Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

Post A Comment: