Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameupongeza mfuko wa Beginnings (Beginnings Fund) unaoratibiwa na na Taasisi ya Afya Ifakara kwa kushirikiana na Wizara ya Afya Wizara ya TAMISEMI na wadau wengine kwa kukubaliana kutekeleza afua za kupunguza vifo vya akina mama na watoto wachanga katika mikoa 13 kwenye jumla ya vituo 210 tanzania bara.

Akizungumza Novemba 26, 2026, jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa Mkutano wa Tatu wa Kitaifa wa Kisayansi kuhusu Afya ya Uzazi, Mama, Mtoto Mchanga, Mtoto, Vijana na Lishe, unaofanyika kuanzia Novemba 25 hadi 27, 2026, Rais Samia amesema mchango wa mfuko huo utasaidia Serikali kufikia malengo ya Mpango wa Sifuri Tatu (Three Zeros), yanayolenga kuhakikisha wajawazito wote wanajifungulia katika vituo vya kutolea huduma za afya, kuzuia vifo vya mama na mtoto pamoja na kuhakikisha watoto wote wanapata chanjo zinazostahili.

Aidha, Rais Samia amesisitiza umuhimu wa kuimarisha huduma bora za afya ili ziweze kuwafikia wanawake na akina mama wote nchini kwa kuzingatia mahitaji yao, huku akieleza kuwa Serikali kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya afya imeendelea kutekeleza maboresho mbalimbali yanayolenga kuongeza upatikanaji wa huduma hizo. Amesema juhudi hizo zimechangia ongezeko kubwa la vituo vya kutolea huduma za afya nchini.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Beginnings Fund, Bi. Alice Kang’ethe, amesema mfuko huo unaendelea kuunga mkono juhudi za Serikali kupitia utekelezaji wa Mpango wa Kitaifa wa Huduma Salama Wakati wa Kujifungua na Huduma kwa Mtoto Mchanga pamoja na kuboresha upatikanaji wa dawa muhimu, vifaa vya uchunguzi, mashine za ultrasound na vifaa vya kidijitali vitakavyosaidia kufuatilia hali ya mama na mtoto wakati wa kujifungua.

Ameongeza kuwa Beginnings Fund iko tayari kuendelea kushirikiana na Serikali katika kufikia malengo ya kitaifa ya mwaka 2030, yanayolenga kupunguza kwa asilimia 33 vifo vya akina mama na watoto wanaozaliwa wakiwa wamefariki tumboni, pamoja na kupunguza kwa asilimia 50 vifo vya watoto wachanga. Kupitia jitihada hizo, mfuko unalenga kusaidia kuzuia zaidi ya vifo 50,000 vya akina mama na watoto wanaozaliwa wakiwa wamefariki tumboni ifikapo mwaka 2031.

Share To:

Alex Sonna

Post A Comment: