Kampuni ya AMSONS Group inakusudia kutoa Shilingi Bilioni 100 (Dola za Marekani Milioni 38) kwa ajili ya kujenga wodi 11 za mama na mtoto katika mikoa tisa ya Tanzania Bara na Zanzibar.

Mpango huo umetangazwa Novemba 26, 2026, katika Mkutano wa Tatu wa Kisayansi wa RMNCAH+N jijini Dar es Salaam, wakati wa hafla ya utiaji saini iliyoshuhudiwa mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan

Wodi hizo zitajengwa katika mikoa ya Dar es Salaam, Ruvuma, Tabora, Singida, Geita, Songwe, Mara, Mwanza na moja Zanzibar. Mradi huo unatarajiwa kuhudumia takribani akina mama na watoto milioni moja kila mwaka. AMSONS Group itagharamia ujenzi wake na kuzikabidhi kwa Serikali kwa ajili ya uendeshaji na utoaji wa huduma kwa umma, bila kuisababishia Serikali deni la ujenzi.

Uwekezaji huo unakuja wakati Tanzania ikiendelea kupiga hatua katika kuboresha afya ya mama na mtoto. Vifo vya uzazi vimepungua hadi 76 kwa kila vizazi hai 100,000 mwaka 2026, kutoka 556 mwaka 2015/16. Vilevile, vifo vya watoto wachanga vimepungua kutoka 24 hadi 17 kwa kila vizazi hai 1,000, huku vituo maalumu vya kuhudumia watoto wachanga vikiongezeka kutoka 14 mwaka 2018 hadi 438 mwaka 2025. Zaidi ya asilimia 85 ya Watanzania sasa wanapata huduma za afya ndani ya kilomita tano kutoka wanapoishi.

“Amsons Group imekuwa mshirika wa Serikali katika kuboresha huduma za afya ya mama na mtoto. Mwaka 2018, AMSONS ilijenga na kukabidhi wodi ya kisasa ya wazazi katika Hospitali ya Amana, na baadaye kuchangia ujenzi wa wodi katika Hospitali za Mwananyamala na Temeke jijini Dar es Salaam. Aidha, kupitia AMSONS Foundation, kampuni hiyo imetenga Dola za Marekani milioni 35 kwa ajili ya kujenga, kuweka samani na vifaa tiba katika hospitali 10 za mama na mtoto nchini Kenya” amebainisha Mkurugenzi Mtendaji wa AMSONS Group, Edha Nahdi.

Uwekezaji huu unaimarisha ushirikiano kati ya Serikali na wadau wa Sekta ya Afya katika kuendeleza ajenda ya Sifuri Tatu (Three Zeros): Sifuri ya uzazi wa nyumbani, sifuri ya vifo vinavyoweza kuzuilika kwa mama na mtoto mchanga, na sifuri ya watoto wasiopata chanjo muhimu.

Share To:

Alex Sonna

Post A Comment: