Na: OWM–TAMISEMI, Dodoma
Mwenyekiti wa Umoja wa Mama na Baba Lishe Tanzania (UMALITA), Bi. Havijawa Omary, amesema kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, wamepokea na kutekeleza maelekezo ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuwa na vazi rasmi litakalowatambulisha mama lishe na baba lishe nchini, ambalo kwa sasa liko katika hatua za mwisho za kukamilishwa na litazinduliwa hivi karibuni.
Bi. Havijawa amesema hayo leo, Oktoba 29, 2026, wakati mama lishe na baba lishe hao walipotembelea jengo jipya la Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI lililopo katika Mji wa Serikali, kwa lengo la kupata uelewa wa huduma zinazotolewa na Serikali kupitia Ofisi hiyo.
“Tunaomba mabwana afya na mabibi afya wote nchini watusaidie kusimamia mama lishe na baba lishe kuvaa vazi hilo rasmi na kuwachukulia hatua watakaoshindwa kulivaa, kwani litakuwa ni utambulisho wetu kwa wananchi tunapowahudumia,” amesema Bi. Havijawa.
Aidha, Bi. Havijawa ameiomba Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI kuhakikisha mama lishe na baba lishe wanapewa maeneo ya biashara, pamoja na vizimba vikubwa vitakavyowawezesha kupika kwa kutumia nishati safi na kutekeleza kaulimbiu yao isemayo, “Vaa kishua, pika kishua; kuwa mama na baba lishe wa kishua,” kwa kupikia nishati safi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa Serikali za Mitaa wa OWM–TAMISEMI, Bw. Stephen Motambi, amesema amepokea ombi la mama lishe na baba lishe hao la kupatiwa maeneo na vizimba vya kufanyia shughuli zao, na kwamba litafanyiwa kazi na wahandisi, maafisa biashara na wataalamu wa sayansi ya chakula na lishe, kwa kuzingatia matumizi ya teknolojia ya nishati safi.
Sanjari na hilo, Bw. Motambi amesema Serikali inatambua kuwa baadhi ya mama lishe wana watoto wadogo, hivyo katika miundombinu ya masoko inayoendelea kujengwa, itahakikisha kunakuwa na vituo vya malezi ya watoto wadogo ili mama lishe waweze kuwaacha watoto katika vituo hivyo na kuendelea na shughuli zao.
Bw. Motambi ameongeza kuwa OWM–TAMISEMI itaendelea kushirikiana na maafisa afya wenye jukumu la kuwasimamia mama lishe na baba lishe, huku akiwataka kuwasilisha Ofisini hapo changamoto zote zinazowakabili katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
Naye, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini wa OWM–TAMISEMI, Bi. Roida Andusamile, amesema amefurahishwa na ziara ya mama lishe na baba lishe hao na kuwataka kuendelea kutembelea Ofisi hiyo kwa ajili ya kujifunza na kutumia fursa zinazopatikana.

Post A Comment: