
Mkuu wa Wilaya ya Ludewa, Mkoa wa Njombe, Mhe. Olivanus Thomas, akizungumza na viongozi mbalimbali wa wilaya hiyo wakati wa mkutano wa elimu ya fedha iliyotolewa na timu ya wataalamu kutoka Wizara ya Fedha na taasisi zake, Wilaya ya Ludewa, mkoani Njombe. Elimu hiyo ni sehemu ya mwendelezo wa zoezi la kuwaelimisha wananchi kuhusu huduma na fursa za kifedha zinazopatikana nchini.

Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Njombe, Mhe. Balozi, Dkt. Pindi Chana, akizungumza na viongozi mbalimbali wa wilaya hiyo wakati wa mkutano wa elimu ya fedha iliyotolewa na timu ya wataalamu kutoka Wizara ya Fedha na taasisi zake, Wilaya ya Ludewa, mkoani Njombe. Elimu hiyo ni sehemu ya mwendelezo wa zoezi la kuwaelimisha wananchi kuhusu huduma na fursa za kifedha zinazopatikana nchini.

Meneja Uhusiano kutoka Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), Bw. Charles Shirima, akitoa elimu kuhusu masoko ya mitaji na dhamana, fursa za uwekezaji katika masoko hayo na umuhimu wa kufanya maamuzi sahihi ya uwekezaji kwa viongozi wa Wilaya ya Ludewa, wakati wa programu maalumu ya elimu ya fedha iliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa, Mkoa wa Njombe.

Afisa Usimamizi wa Fedha Mwandamizi kutoka, Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha, Bw. Salim Khalfan Kimaro, akitoa mada kuhusu masuala ya fedha na umuhimu wa kusajili vikundi vya kutoa Huduma Ndogo za Fedha na vile vya kijamii kwa viongozi wa Wilaya ya Ludewa, kwenye program maalum ya elimu ya fedha iliyotolewa katika Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa, Mkoa wa Njombe.

Afisa Uendeshaji na Biashara kutoka Dhamana ya Uwekezaji na Usimamizi Rasilimali Tanzania, (UTT AMIS), Bw. Benedict Raphael, akitoa elimu kuhusu uwekezaji kupitia mifuko ya uwekezaji wa pamoja (Collective Investment Schemes), umuhimu wa kuweka akiba na namna wananchi wanavyoweza kuwekeza fedha zao kulingana na uwezo wao ili kukuza kipato na kujenga ustawi wa kifedha, Wilaya ya Ludewa, wakati wa programu maalumu ya elimu ya fedha iliyofanyika katika Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa, Mkoa wa Njombe.

Baadhi ya viongozi kutoka Wilaya ya Ludewa, mkoani Njombe, wakiwa pamoja na Timu ya Wataalamu wa Elimu ya Fedha kutoka Wizara ya Fedha na Taasisi zake Wilayani humo, wakichangia mada mbalimbali kuhusu elimu ya fedha waliyoipata kuhusu matumizi sahihi ya fedha, umuhimu wa kupanga bajeti na kuitekeleza, umuhimu wa kusajili vikundi vya huduma ndogo za fedha , utunzaji wa fedha binafsi, umuhimu wa kushirikisha familia na watu wa karibu kwenye masuala ya fedha na uwekezaji, umuhimu wa kukata bima ya biashara na mali nyingine.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-WF, Njombe)
Na Chedaiwe Msuya, WF, Njombe
Mkuu wa Wilaya ya Ludewa, Mhe. Olivanus Thomas, amewahimiza viongozi wa wilaya hiyo kuwa mabalozi wa elimu ya fedha kwa wananchi ili kuwasaidia kutambua na kutumia fursa mbalimbali za kifedha zinazotolewa na Serikali na taasisi za sekta ya fedha kwa ajili ya kukuza mitaji, kuongeza kipato na kuimarisha maendeleo ya kiuchumi.
Mhe. Thomas ametoa wito huo wakati wa programu ya utoaji wa elimu ya fedha kwa viongozi wa Wilaya ya Ludewa, mkoani Njombe, iliyowakutanisha wataalamu kutoka Wizara ya Fedha na taasisi mbalimbali za sekta ya fedha nchini kwa lengo la kuongeza uelewa kuhusu huduma za kifedha, uwekezaji na fursa za kiuchumi zinazopatikana nchini.
Akizungumza katika programu hiyo, Mhe. Thomas amesisitiza umuhimu wa viongozi kuwaelimisha wananchi kuhusu fursa za kifedha zilizopo, ikiwemo mikopo inayotengwa kwa ajili ya makundi maalumu, yakiwemo wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, ili waweze kuitumia kwa malengo yaliyokusudiwa.
“Ni muhimu viongozi kuwa na uelewa wa masuala ya fedha ili waweze kuwaelimisha wananchi kuhusu fursa zinazopatikana, ikiwemo mikopo inayotolewa kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, na kuwahamasisha kuitumia kwa malengo yaliyokusudiwa kwa ajili ya kukuza mitaji, kuongeza kipato na kuimarisha maendeleo ya jamii,” amesema Mhe. Thomas.
Mhe. Thomas, ameongeza kuwa upatikanaji wa taarifa sahihi kuhusu huduma za kifedha ni hatua muhimu katika kuwawezesha wananchi kuanzisha na kuendeleza biashara, kukuza mitaji na kuongeza kipato cha kaya. Aidha, ameeleza kuwa viongozi wana nafasi kubwa ya kuhakikisha elimu hiyo inawafikia wananchi wa makundi mbalimbali na kuwasaidia kufanya maamuzi sahihi ya kifedha.
Kwa upande wake, Mbunge wa Viti Maalumu, Mhe. Balozi, Dkt. Pindi Chana, amewataka wananchi wa Ludewa kutumia elimu inayotolewa na wataalamu wa sekta ya fedha kama fursa ya kujifunza mbinu za kusimamia mapato na matumizi yao, pamoja na kutambua huduma za kifedha zinazoweza kuwasaidia kuboresha shughuli zao za kiuchumi.
Dkt. Chana amesisitiza umuhimu wa wananchi kutafuta taarifa sahihi na kupata ufafanuzi wa kina kuhusu masharti ya mikopo, huduma za benki na fursa za uwekezaji kabla ya kufanya maamuzi ya kifedha, ili kuepuka hasara zinazoweza kusababishwa na ukosefu wa taarifa za kutosha.
“Ninawahimiza wananchi wa Ludewa kutumia fursa ya uwepo wa wataalamu wa sekta ya fedha kupata elimu na ufafanuzi kuhusu huduma za kifedha, masharti ya mikopo na fursa za uwekezaji, ili muweze kufanya maamuzi sahihi yanayoendana na uwezo wenu wa kifedha na kuboresha shughuli zenu za kiuchumi,” amesema Dkt. Chana.
Dkt. Chana, ameeleza kuwa uelewa wa huduma za kifedha utawawezesha wananchi kuchagua fursa zinazoendana na uwezo wao wa kifedha na kuzitumia katika kuendeleza biashara, kuongeza uzalishaji na kuimarisha kipato cha familia kitakachopelekea kukuza Uchumi wa mtu mmoja mmoja na nchi kwa ujumla.
Dkt. Chana, amewataka wananchi wa Ludewa kuchangamkia uwepo wa wataalamu kutoka Wizara ya Fedha na taasisi mbalimbali za sekta ya fedha wilayani hapo kwa kushiriki kikamilifu katika mafunzo , akisisitiza kuwa elimu watakayoipata inapaswa kutumika kwa vitendo ili kuleta manufaa katika shughuli zao za kila siku na kuchangia ustawi wa Ludewa.
Programu maalum ya elimu ya fedha inayotolewa na Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali za sekta ya fedha inalenga kuwawezesha wananchi kuelewa huduma za kifedha, fursa za uwekezaji, masoko ya mitaji na umuhimu wa kuweka akiba kwa ajili ya maendeleo ya wananchi ya sasa na baadae.
Kupitia elimu inayotolewa na wataalamu kutoka na Wizara ya Fedha , CMSA na UTT AMIS, wananchi wanapata fursa ya kuelewa njia mbalimbali za kukuza mitaji, kuwekeza kulingana na uwezo wao wa kifedha na kufanya maamuzi sahihi kwa kuzingatia taarifa sahihi, malengo yao na kubaini vihatarishi vinavyoweza kujitokeza katika uwekezaji.

Post A Comment: