▪️Atoa wito kwa nchi za Afrika kuimarisha ushirikiano wa kikanda, kuongeza thamani ya madini na kuharakisha utekelezaji wa Dira ya Madini ya Afrika.
📍Accra, Ghana
Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Peter Mavunde, amezitaka nchi za Afrika kuacha kufanya kazi kwa kujitenga na badala yake kuunganisha nguvu katika usimamizi na uendelezaji wa rasilimali za madini ili kukuza viwanda, ajira na uchumi wa bara hilo.
Ameyasema hayo leo Oktoba 19 wakati akizungumza katika mjadala wa jopo la Mawaziri kutoka nchi za Tanzania, Nigeria na Liberia uliokuwa na mada isemayo “From Vision to Delivery: Making the African Mining Vision Work for Member States”,katika mkutano wa Kimataifa wa Mining in Motion unaofanyika kwasiku tatu kuanzia Oktoba 19 hadi 21, 2026 jijini Accra Ghana.
Mhe. Mavunde amesema wakati umefika kwa nchi za Afrika kuweka pembeni tofauti zao na kushirikiana kutekeleza mikakati ya pamoja ya maendeleo ya Sekta ya Madini.
Amesema Afrika ina zaidi ya asilimia 32 ya rasilimali za madini muhimu zinazojulikana duniani, lakini bado sehemu kubwa ya utajiri huo husafirishwa nje ya bara bila kuongezwa thamani ya kutosha na kuwa hali hiyo inanyima nchi za Afrika fursa za kujenga viwanda, kutengeneza ajira na kuongeza mapato.
Akifafanua hatua zinazochukuliwa na Tanzania, Mhe. Mavunde amesema mageuzi ya kisheria yaliyofanyika mwaka 2017 yameimarisha usimamizi wa rasilimali za madini na ushiriki wa Serikali, huku hatua za kuzuia usafirishaji wa madini ghafi zikichochea uongezaji thamani nchini.
Ameeleza kuwa Tanzania sasa chini ya uongozi wa Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ina zaidi ya viwanda vinane vya kusafisha dhahabu na viwanda zaidi ya 16 vya uchakataji na usafishaji wa madini ya metali za msingi na kuwa Sekta ya Madini inachangia asilimia 10.3 ya Pato la Taifa, huku wachimbaji wadogo wakichangia takribani asilimia 40 ya uzalishaji wa sekta hiyo ikiwa ni matokeo ya hatua za dhati za Serikali kuimarisha sekta hiyo.
Katika kuimarisha ushirikiano wa kikanda, Mhe. Mavunde amezitaja Tanzania, Madagascar na Msumbiji kuwa na fursa ya kuunganisha nguvu katika uendelezaji wa rasilimali za grafiti, uchakataji na uoanisha wa sera ili kujenga mnyororo wa thamani unaowanufaisha wananchi wa nchi hizo.
Amesisitiza kuwa Dira ya Madini ya Afrika haipaswi kubaki kwenye nyaraka na majadiliano, bali inapaswa kuambatana na utekelezaji wa vitendo huku akihimiza nchi wanachama kuimarisha mifumo ya mazungumzo na maamuzi ya pamoja ili kuharakisha utekelezaji wa mikakati iliyokubaliwa.
“Ni wakati sasa kwa Afrika kuanza kufanya kazi pamoja. Afrika ni moja, na tunapaswa kufanya kazi kama timu moja,” amesisitiza Mhe. Mavunde, akieleza kuwa ushirikiano ni muhimu katika kuhakikisha rasilimali za madini zinachochea maendeleo ya viwanda na ukuaji wa uchumi.
Waziri Mavunde ametoa wito kwa nchi za Afrika kugeuza utajiri wa madini kuwa fursa za viwanda, ajira, teknolojia na mapato zaidi, badala ya kuendelea kuuza madini ghafi na kununua bidhaa zilizoongezwa thamani kutoka nje ya bara hilo.
Awali akifungua rasmi Mkutano huo, Rais wa Jamhuri ya Ghana Mheshimiwa John Dramani Mahama amesema kuwa ni muda wa Afrika kugeukia soko la madini muhimu na mkakati kutokana na uhitaji mkubwa wa nishati safi ulimwenguni, lengo ni kuyaongezea thamani madini haya kabla hayajaenda katika soko la dunia.


.jpeg)

.jpeg)

.jpeg)

Post A Comment: