Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza, Mhe. Jubilate Lauwo, amefungua rasmi Kliniki ya Viwango (Viwango Clinic), iliyoandaliwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kwa lengo la kusogeza huduma karibu na wananchi.
Akizungumza jijini Mwanza Jumatano Oktoba 21, 2026 wakati wa ufunguzi wa kliniki hiyo, Mhe. Lauwo amewataka wafanyabiashara wa bidhaa za chakula na vipodozi kutumia fursa hiyo kusajili bidhaa zao hatua itakayosaidia pia kuongeza imani kwa wateja wao.
“Wafanyabiashara mnapaswa kuhakikisha bidhaa mnazouza ni salama na zinakidhi viwango vinavyotakiwa na TBS hivyo mna wajibu wa kuzingatia taratibu za biashara zenu kwa kuhakikisha mnasajiliwa” amesema Mhe. Lauwo.
Aidha Mhe. Lauwo amesema Viwango Clinic ni fursa kwa wafanyabiashara wa bidhaa za chakula na vipodozi jijini Mwanza kupata elimu na huduma ya usajili karibu yao huku pia wananchi wakipata elimu itakayowasaidia kuepuka matumizi ya bidhaa zisizokidhi viwango vya TBS.
“Kwa mujibu wa mwongozo wa TBS, wafanyabiashara wa chakula na vipodozi wanapaswa kuzingatia taratibu za usajili wa bidhaa, maeneo ya biashara zao kama vile maghala, maduka na migahawa” amesisitiza Mhe. Lauwo wakati akizungumza kwenye ufunguzi huo uliohudhuriwa pia na viongozi, wananchi na wafanyabiashara mbalimbali.
Naye Meneja wa TBS Kanda ya Ziwa Mashariki, Happy Brown amesema Viwango Clinic inayofanyika eneo la Soko Kuu jijini Mwanza itadumu kwa siku tano imekwishaanza Jumatatu Oktoba 19, 2026 hadi Ijumaa Oktoba 23, 2026 ambapo lengo ni kusogeza elimu na huduma karibu na wananchi.



Post A Comment: