Na Atley Kuni, WAF – Ruvuma
Wananchi katika baadhi ya Halmashauri za Mkoa wa Ruvuma wameanza kuchukua tahadhari dhidi ya athari zinazoweza kujitokeza kutokana na mvua za El Niño pamoja na tishio la magonjwa ya mlipuko, ikiwemo Ebola, kufuatia elimu inayotolewa na Serikali kupitia timu za Mawasiliano ya Hatari na Ushirikishwaji wa Jamii (RCCE).
Hali hiyo imebainika Septemba 28, 2026, mbele ya Kikosi Kazi kinachofanya zoezi la kupitia dodoso na kuandaa timu za RCCE katika Halmashauri za mkoa huo kwa ajili ya tahadhari dhidi ya El Niño na Ebola.
Afisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri ya Madaba, John Mashauri, amesema elimu kwa wananchi ni muhimu katika kuwafanya wachukue tahadhari mapema, ikiwemo kuhifadhi chakula na kufuatilia taarifa sahihi za afya na hali ya hewa.
“Kwa sasa jamii imepata mwamko, kwani hata bei ya soko kwa upande wa mazao imeanza kuchangamka. Debe la mahindi lililokuwa likinunuliwa kati ya shilingi 3,500 hadi 4,000 limepanda na kufikia 7,000. Tafsiri yake ni kwamba wengi wameamua kuhifadhi chakula,” amesema Mashauri.
Zoezi hilo la kupitia dodoso na kuandaa timu za Mpango wa Haraka wa Mawasiliano na Ushirikishwaji wa Jamii, linalofanywa chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu-TAMISEMI, Wizara ya Afya na UNICEF, limeendelea mkoani humo huku waratibu wakizitaka timu kuwa na mpango wa dharura wenye kupimika.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Mratibu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu-TAMISEMI, Chipole Mpelembe, amesema zoezi hilo linaendelea katika mikoa 12 nchini na linalenga kuziweka timu katika utayari, huku pamoja na mambo mengine zikizingatia makundi maalum kama watoto wa shule.
“Timu za RCCE zina jukumu la kukusanya taarifa na kutumia matokeo ya dodoso ili kupanga elimu inayolenga mahitaji halisi ya jamii,” amesema Mpelembe.
Mpelembe amewaambia wataalamu hao kuwa maandalizi ya mapema yanaweza kusaidia kupunguza athari pale changamoto zinapojitokeza, akisisitiza umuhimu wa Halmashauri kuimarisha mifumo ya uratibu na utayari.
Kauli hiyo imekuja wakati Serikali ikiendelea kuimarisha maandalizi dhidi ya Ebola na changamoto zinazoweza kuhusishwa na mvua kubwa za El Niño, wakati kwa kipindi cha Juni 2026, tetesi 64 za Ebola kutoka mikoa 21 zilikuwa zimechunguzwa bila kubainika maambukizi nchini.







Post A Comment: