
Na WMA- Dodoma
Wakala wa Vipimo (WMA) umetakiwa kupanua mpango wa kuanzisha klabu za vipimo shuleni hadi katika shule za sekondari, ili kuongeza wigo wa elimu ya vipimo na kuhakikisha uelewa wa matumizi sahihi ya vipimo unafika hadi ngazi ya kaya.
Wito huo umetolewa na Mhadhiri wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), Patroba Chaulo, ambaye amepongeza WMA kwa kuanzisha klabu hizo katika shule za msingi, akisema matumizi ya wanafunzi kama mabalozi wa elimu ya vipimo ni mkakati wenye tija kubwa kwa jamii.
Amesema mpango huo unatoa fursa ya kutumia mfumo wa elimu wa “mtoto kwa mtoto” (child-to-child), ambapo wanafunzi huweza kufikisha elimu na ujumbe kwa wenzao kwa urahisi zaidi, na hatimaye kuwafikishia wazazi na familia zao.
Kwa mujibu wa Chaulo, njia hiyo inaweza kuwa na ufanisi mkubwa kwa sababu wanafunzi wana nafasi kubwa ya kushirikiana na kuwasiliana na wenzao kwa lugha rahisi na inayoeleweka, jambo linalorahisisha uenezaji wa elimu ya vipimo.
“Mtoto anaweza kumwelewesha mtoto mwenzake kwa urahisi zaidi kuliko mtu mzima anapojaribu kumwelewesha mwanafunzi. Hii inafanya mfumo wa child-to-child kuwa fursa muhimu katika kueneza elimu ya vipimo,” amesema.
Ameeleza kuwa umuhimu wa mpango huo hauishii shuleni pekee, bali unaweza kusaidia elimu ya vipimo kufika hadi ngazi ya kaya, kwa kuwa wanafunzi wanaotoka katika klabu hizo wanaishi katika familia na jamii mbalimbali.
Amesema kupitia wanafunzi hao, WMA inaweza kuwa na mtandao mpana wa mabalozi ambao utasaidia kufikisha ujumbe kuhusu umuhimu wa vipimo sahihi katika maeneo ambayo ni vigumu kwa Wakala kufika moja kwa moja.
“WMA haiwezi kufika katika kila nyumba, lakini wanafunzi hawa wanatoka katika kaya mbalimbali. Hivyo, wanakuwa kiungo muhimu cha kufikisha elimu hii kutoka shuleni hadi katika familia na jamii kwa ujumla,” amesisitiza.
Chaulo amesema elimu hiyo ni muhimu katika kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu matumizi ya vipimo sahihi na vilivyothibitishwa, hususan katika shughuli za kila siku zinazohusisha biashara na miamala mbalimbali.
Amesema jamii yenye uelewa kuhusu vipimo inaweza kutambua umuhimu wa kuhakikisha bidhaa zinapimwa kwa vipimo sahihi na kulinda haki za watumiaji pamoja na wafanyabiashara.
Kwa msingi huo, amependekeza WMA kuendelea kuimarisha klabu hizo katika shule za msingi na kuzitanua hadi shule za sekondari ili kuwafikia vijana wengi zaidi na kujenga kizazi chenye uelewa mpana kuhusu viwango na vipimo.
Ameongeza kuwa uwekezaji katika elimu ya vipimo kupitia shule ni hatua muhimu ya kujenga utamaduni wa matumizi sahihi ya vipimo nchini, huku wanafunzi wakitumiwa kama sehemu ya suluhisho la kufikisha elimu hiyo katika jamii.
Mpango huo pia unatarajiwa kuongeza uelewa wa Watanzania kuhusu umuhimu wa kuwa na viwango na vipimo sahihi na vilivyothibitishwa (standards in measurements) katika maisha ya kila siku, hususan katika shughuli zinazohusisha biashara, ununuzi na uuzaji wa bidhaa.




Post A Comment: