Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mhe. Subira Mgalu, amepongeza hatua madhubuti zinazochukuliwa na Wizara ya Nishati pamoja na taasisi zake katika kuhamasisha na kusambaza nishati safi ya kupikia nchini.

Mhe. Mgalu ametoa pongezi hizo jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kutambuliwa kuwa Kinara wa Nishati Safi Afrika, iliyoandaliwa na Taasisi ya Women and Youth Future Initiative (WYFI).

Amesema Wizara ya Nishati na taasisi zake, ikiwemo Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), zimeendelea kutekeleza hatua mbalimbali zinazolenga kuhakikisha nishati safi ya kupikia inawafikia wananchi wengi zaidi.

Mhe. Mgalu amebainisha kuwa Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia unalenga kuhakikisha takriban asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi na salama ya kupikia ifikapo mwaka 2034, huku Serikali ikijipanga kutumia takriban shilingi trilioni 24.6 katika uwekezaji na utekelezaji wa miundombinu ya nishati safi nchini.

Ameongeza kuwa, katika kuwezesha upatikanaji wa nishati mbadala na nafuu kwa wananchi, Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) limeanza uzalishaji wa mkaa mbadala unaotokana na makaa ya mawe, ambao unapatikana kwa bei nafuu. Aidha, kiwanda cha Kisarawe kinazalisha mkaa na majiko mbadala, huku kukiwa na takriban viwanda vitano vinavyofanya kazi katika mikoa mbalimbali na mipango ya kufungua kiwanda kipya mkoani Dodoma ikiendelea.

Mhe. Mgalu ametoa wito kwa Watanzania kuunga mkono juhudi za Serikali za kuhamia kwenye matumizi ya nishati safi ya kupikia, akisisitiza kuwa hatua hiyo inalinda mazingira na afya ya jamii, inapunguza changamoto zinazowakabili wanawake kutokana na matumizi ya nishati zisizo safi na kuchangia ukuaji wa uchumi wa Taifa.

Aidha, ameahidi kuwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini itaendelea kuishauri na kuisimamia Serikali kwa karibu ili kuhakikisha ajenda ya nishati safi ya kupikia inatekelezwa kikamilifu kwa manufaa ya Watanzania wote.

Kwa upande wake, Meneja wa Elimu kwa Walipa Kodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), CPA Paul Walalaze, amesema Serikali imeendelea kutoa misamaha mbalimbali ya kodi, hususan Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT), kwa baadhi ya vifaa vinavyotumika katika nishati safi ya kupikia, ikiwemo mitungi ya gesi, hatua inayolenga kuongeza upatikanaji na matumizi ya nishati hiyo nchini.







Share To:
Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

Post A Comment: