▪️Azindua na Zoezi la Urushaji wa Helikopta ya Utafiti wa Madini ya Barrick 

▪️Maeneo ya Leseni za Vijana,Wanawake na Wenye Ulemavu Kufanyiwa Utafiti kwa Helikopta

▪️Rais Dkt. Samia Apongezwa kwa Maelekezo na Maono Yake Sekta ya Madini

▪️Baraza la Dhahabu Duniani Lavutiwa na Programu ya MBT

▪️Waziri Mavunde Aagiza Mitambo ya Uchorongaji ya STAMICO Kufika Mara Baada ya Utafiti Kukamilika

Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, amezindua rasmi Programu ya Mining for a Brighter Tomorrow (MBT), maarufu kama “Kesho Iliyo Njema,” na kueleza kuwa programu hiyo ni hatua ya kimkakati ya Serikali katika kufungua milango mipya ya fursa na uwezeshaji kwa vijana, wanawake na watu wenye mahitaji maalum kushiriki kikamilifu katika Sekta ya Madini na kwamba programu inalenga kuwasaidia walengwa kuondokana na uchimbaji wa kubahatisha na kuelekea kwenye uchimbaji wenye tija, unaotumia maarifa, teknolojia na taarifa sahihi za kijiolojia, huku Serikali ikiendelea kuweka mazingira wezeshi ya upatikanaji wa maeneo ya uchimbaji, leseni na fursa za kiuchumi zinazotokana na rasilimali madini.

Waziri Mavunde amebainisha hayo, leo Agosti 31, 2026,  katika eneo la Nyamongo, Wilaya ya Tarime, Mkoani Mara, wakati akizungumza katika hafla hiyo iliyokwenda sambamba na uzinduzi wa utafiti wa kina wa madini unaofanywa na Barrick Gold Corporation, 

Mhe. Mavunde ametumia nafasi hiyo kumpogeza na kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa maelekezo na maono yake ya kuweka mazingira wezeshi kwa makundi hayo na kuongeza kuwa Rais Dkt. Samia ameagiza asilimia 10 ya mapato yatokanayo na makusanyo ya Sekta ya Madini kutengwa kwa ajili ya utafiti wa kina wa madini, hatua ambayo inalenga kuongeza taarifa za rasilimali madini nchini na kufungua fursa zaidi kwa wananchi.

Waziri Mavunde pia ameishukuru Barrick kwa kukubali kufanya utafiti katika maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya wachimbaji wadogo Nyamongo, akieleza kuwa ndani ya wiki mbili utafiti huo unaweza kufanyika katika eneo lenye ukubwa wa takribani kilomita za mraba 6,000 na kusisitiza kuwa dhamira ya Serikali kuhakikisha matokeo ya utafiti yanageuka kuwa fursa halisi kwa wananchi, sambamba na kumuelekeza Kamishna wa Madini, kwa kushirikiana na GST na STAMICO, kukaa na Barrick na kuhakikisha mara utafiti utakapokamilika, mitambo ya uchorongaji inafika Nyamongo kwa ajili ya hatua inayofuata ya utafiti.

Aidha, Waziri Mavunde amesema uzinduzi huo unaashiria mwanzo wa safari ya kujenga “Kesho Iliyo Njema” katika Sekta ya Madini, huku akieleza kuwa Rais wa Baraza la Dhahabu Duniani (World Gold Council) amevutiwa na programu ya MBT na kwamba vijana wa Nyamongo ndio watakaokuwa miongoni mwa vijana wa kwanza kunufaika na mpango huo. 

“Tunaenda kupanda mbegu, tunaanza safari; leo mnaianza safari ya kwenda kubadilisha maisha yenu na mimi nitasimamia programu hii ili tufikie lengo,” amesema Mavunde.

Kwa upande mwingine, Waziri Mavunde amesema kuwa amedhamiria kuipima Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa ya Kimadini kwa kuhakikisha maeneo maalum yanatengwa kwa ajili ya makundi ya vijana na wanawake, huku leseni zikitolewa kwa kasi ili kuwawezesha kushiriki katika shughuli za uchimbaji, amesema lengo ni kuona programu ya MBT ikienda sambamba na ukusanyaji wa maduhuli na kwamba angependa kuona kila siku fursa mpya za leseni zikitolewa kwa vijana kupitia programu hiyo. Aidha, ametoa wito kwa viongozi wa vijana wachimbaji kuweka pembeni tofauti zao, kushirikiana na kuepuka kuwagawa vijana, akisisitiza kuwa Serikali haitakubali migogoro ya makundi iwe kikwazo cha utekelezaji wa programu hiyo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Brigedia Jenerali Evans Mtambi amesema kuwa, Kupitia programu hiyo na tafiti zinazofanyika, tunaamini vijana wataweza kuchimba kisayansi zaidi, kwa kutumia taarifa na teknolojia badala ya kuchimba kwa kubahatisha na kwamba hatua hiyo itasaidia kupunguza gharama na hasara zisizo za lazima, kuongeza tija na hatimaye kuwawezesha wachimbaji wetu kupata matokeo makubwa zaidi kutokana na juhudi wanazoweka katika shughuli zao na kwamba ukosefu wa taarifa sahihi zinazoweza kuwaongoza wachimbaji kujua madini yapo wapi kwa kiwango gani na namna bora ya kuyafikia ndiyo ilikuwa changamoto kubwa.

Awali, Meneja Mkazi (Country Manager) wa Kampuni ya Barrick Gold nchini Tanzania, Dkt. Melkiory Ngido ameeleza kuwa kama  Barrick wanajivunia kuwa miongoni mwa wadau walioshiriki katika programu tangu mwanzo. 

“Tulichukua hatua ya kimkakati ya kurudisha leseni ya eneo ambalo tayari tulikuwa tumelifanyia utafiti na kubaini kuwa lina uwezo wa kutoa fursa kwa makundi ya wachimbaji wadogo. Tuliona ni muhimu eneo hilo lisibaki chini ya umiliki wetu wakati linaweza kuwa chanzo cha ajira, kipato na fursa za kiuchumi kwa Watanzania wanaojihusisha na uchimbaji mdogo. Hatua hii inaakisi dhamira yetu ya kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha rasilimali za madini zinawanufaisha wananchi na zinachangia maendeleo ya jamii zinazozunguka maeneo ya migodi.” Amesema Ngido

Makamu Rais wa FEMATA, Victor Tesha ameeleza kuwa wao kama wachimbaji wadogo wa madini nchini Tanzania wanayo furaha kubwa kwa hatua hii iliyofikiwa na wanaiona programu ya Mining for a Brighter Tomorrow (MBT) kama hatua muhimu sana katika kutatua changamoto ambazo zimekuwa zikituathiri kwa muda mrefu, ameongeza kuwa wana imani kubwa na Serikali na wanaamini kupitia programu hiyo, maisha ya wachimbaji wadogo na familia zinazotegemea shughuli za madinj yanaenda kubadilika kwa kiwango kikubwa.

















Share To:

Post A Comment: