
Na Mwandishi Wetu - DAR ES SALAAM
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki, ametoa maelekezo manne kwa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), akitaka Awamu ya Pili ya Mradi wa Faiba Mlangoni Kwako (FTTH) iwanufaishe wananchi kupitia huduma yenye ubora, uhakika na gharama nafuu.
Mhe. Kairuki alitoa maelekezo hayo wakati akizindua rasmi utekelezaji wa awamu hiyo katika Ukumbi wa Johari Rotana, Dar es Salaam, akisisitiza kuwa mafanikio ya mradi hayapaswi kupimwa kwa idadi ya Home Pass pekee, bali kwa idadi ya wananchi wanaounganishwa, ubora wa huduma, kasi ya intaneti na kiwango cha kuridhika kwa wateja.
Ametaka TTCL kupanua huduma ya faiba hadi maeneo yenye makazi yanayokua, masoko, maeneo ya biashara, viwanda, shule, vyuo, vituo vya afya na ofisi za Serikali Tanzania Bara na Zanzibar.
Pia ameagiza Shirika kudumisha ubora wa huduma na kuimarisha huduma kwa wateja, ikiwemo kushughulikia malalamiko kwa haraka na kwa ufanisi.
Waziri huyo amelitaka TTCL kuhakikisha huduma inapatikana kwa gharama nafuu kwa kuandaa vifurushi vinavyokidhi mahitaji ya familia, wanafunzi, vijana na wafanyabiashara wadogo na wa kati.
Katika agizo la nne, amesisitiza uwajibikaji na nidhamu ya kibiashara katika usimamizi wa mradi, akitaka wazabuni na wakandarasi wasimamiwe kwa ufanisi ili kazi zikamilike kwa wakati, kwa ubora na kwa kuzingatia thamani ya fedha.
Amesema Faiba Mlangoni Kwako si mradi wa kujenga miundombinu ya mawasiliano pekee, bali ni hatua ya kimkakati ya kufungua fursa za elimu, biashara, ajira na ubunifu na kuchochea uchumi wa kidijitali.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, CPA Moremi Marwa, amesema Awamu ya Pili ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Biashara wa Miaka 10 wa Shirika wa 2025/26–2034/35.
Marwa amesema Awamu ya Kwanza imewezesha TTCL kujenga zaidi ya Home Pass 280,000 na kufikisha karibu 300,000 maungio ya huduma ya nyuzi za macho nchini.
Amesema katika Awamu ya Pili TTCL inalenga kuongeza zaidi ya Home Pass 400,000, huku ikiendelea kutumia teknolojia ya Gigabit Passive Optical Network (GPON) ili kuongeza ufanisi, kupunguza gharama za uendeshaji na kuboresha ubora wa huduma.
Ameongeza kuwa utekelezaji unafanyika kwa ushirikiano na makandarasi wa ndani na wa kimataifa, wakiwemo Huawei, ZTT na Visoll.
Waziri Kairuki amewataka wananchi kutumia huduma hiyo katika kujifunza, kufanya biashara, kuongeza uzalishaji, kubuni ajira na kupata huduma za Serikali kidijitali, huku akiwataka pia kulinda miundombinu ya mawasiliano dhidi ya uharibifu na wizi.










Post A Comment: