Na Mwandishi Wetu
BENKI ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) na Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Zanzibar (ZEEA) zimesaini Hati ya Makubaliano (MoU) kwa lengo la kuongeza upatikanaji wa fedha kwa wakulima na wajasiriamali, kuongeza uzalishaji na kuimarisha minyororo ya thamani ya kilimo Zanzibar.
Makubaliano hayo yaliyosainiwa katika Hoteli ya Golden Tulip, Mbweni Zanzibar, yanalenga kuunganisha upatikanaji wa mitaji na mahitaji ya mnyororo wa thamani wa kilimo, kuanzia uzalishaji, ukusanyaji na uchakataji hadi usafirishaji na masoko.
Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri wa Vijana, Ajira na Uwezeshaji wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Shaaban Ali Othman, aliipongeza TADB na ZEEA kwa ushirikiano huo, akisema utachangia kuongeza ajira kwa vijana, ujasiriamali, usalama wa chakula na uwezeshaji wananchi kiuchumi.
Kupitia makubaliano hayo, TADB na ZEEA zitaandaa Miradi Jumuishi ya Ufadhili wa Mnyororo wa Thamani (IVCF) katika maeneo ya kilimo cha bustani, ufugaji wa kuku, mifugo, viungo, mpunga, miwa na Uchumi wa Buluu.
Taasisi hizo pia zinalenga kuanzisha bidhaa kati ya tatu hadi tano za mikopo ya kilimo, huku TADB ikiisaidia ZEEA kuimarisha uwezo katika tathmini ya mikopo, uchambuzi wa minyororo ya thamani, usimamizi wa vihatarishi na urejeshaji wa mikopo.
Wakulima wadogo, wanawake, vijana pamoja na wafanyabiashara wadogo na wa kati (MSMEs) wamepewa kipaumbele katika fursa zitakazotokana na ushirikiano huo.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Frank Nyabundege, alisema Benki hiyo imejenga msingi mzuri wa uwekezaji Zanzibar, ambapo hadi sasa imetoa mikopo yenye thamani ya Sh bilioni 15.87 kwa miradi 57.
Alisema mwaka 2026 pekee TADB imeidhinisha Sh bilioni 15 kwa sekta ya karafuu na Sh bilioni tano kupitia taasisi za fedha kwa ajili ya kuendeleza utoaji wa mikopo katika sekta ya kilimo, ikiwemo mifugo na uvuvi.
“TADB haiji Zanzibar kuanza safari mpya kutoka sifuri, bali tunajenga juu ya msingi wa ushirikiano na uwekezaji ambao tayari umeanza kuleta matokeo,” alisema Nyabundege.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa ZEEA, Juma Burhan Mohamed, alisema makubaliano hayo yataunganisha uwezeshaji wa wananchi, upatikanaji wa mitaji, maendeleo ya kilimo, urasimishaji wa biashara na uendelezaji wa minyororo ya thamani.
Alisema ushirikiano huo utasaidia wananchi kuzalisha, kukuza biashara, kupata mitaji na masoko pamoja na kuongeza kipato na kujitegemea kiuchumi.
Katika hafla hiyo, ZEEA pia ilisaini Hati ya Makubaliano na Wakala wa Usajili wa Biashara na Mali Zanzibar (BPRA), kwa lengo la kurahisisha urasimishaji wa biashara, huduma za usajili na upatikanaji wa taarifa muhimu kwa wajasiriamali.
Ushirikiano huo pia utahusisha maonesho ya pamoja ya kibiashara yatakayowapa wajasiriamali fursa za kutangaza bidhaa na huduma zao, kupata masoko mapya, kujenga mitandao ya biashara na kuunganishwa na wawekezaji na taasisi za fedha.
TADB na ZEEA zimesema utekelezaji wa makubaliano hayo utasimamiwa na Kamati ya Pamoja ya Uratibu (JCC), itakayokutana angalau mara mbili kwa mwaka kufuatilia maendeleo na kushughulikia changamoto zitakazojitokeza.
Nyabundege alisema mafanikio ya makubaliano hayo hayatapimwa kwa hati iliyosainiwa pekee, bali kwa miradi itakayoandaliwa, fedha zitakazohamasishwa, biashara zitakazokuzwa, ajira zitakazochochewa na wananchi watakaonufaika.
Ushirikiano huo unatarajiwa pia kuimarisha uhusiano kati ya wazalishaji wa Zanzibar na sekta ya utalii kwa kuwezesha hoteli, migahawa na biashara nyingine kupata chakula na bidhaa zinazozalishwa nchini humo.

















Post A Comment: