✅Asisitiza Sheria ya Uhifadhi hairuhusu utafiti, uchimbaji madini mengine isipokuwa Urani, Gesi Asilia na Mafuta


✅Aeleza Sheria Ya Madini inamtaka Mmiliki wa Leseni Kupata Ridhaa ya Maandishi toka Mamlaka za Hifadhi ya Misitu


Serikali imesema itaendelea kutoa Vibali vya Uchimbaji wa Madini katika maeneo ya Hifadhi yanayoruhusiwa Kisheria kwa wananchi na wawekezaji watakaokidhi masharti husika na kupata vibali kutoka Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TSF), Mamlaka ya usimamizi wa Wanyamapori (TAWA) na   Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC)  kadri maombi yanavyowasilishwa.

Hayo yamebainishwa Agosti 26, 2026 bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Madini Mhe. Dkt. Steven Kiruswa wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Josephine Kapoma aliyetaka kujua ni lini Serikali itaruhusu wananchi kupewa vibali vya kuchimba madini kwenye hifadhi.

 Dkt. Kiruswa amefafanua kuwa, kwa mujibu wa kifungu cha 26 cha Sheria ya Misitu, Sura ya 323, uchimbaji wa madini ndani ya Hifadhi za Misitu zinazosimamiwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) na unaruhusiwa pale ambapo mwombaji amepewa leseni au kibali kwa mujibu wa Sheria hiyo huku akitakiwa kuwa amekamilisha Tathmini ya Athari kwa Mazingira (EIA).

"Kwa upande wa Mapori ya Akiba yanayosimamiwa TAWA, vifungu vya 20(2) na 20(3) vya Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori, Sura ya 283, vinazuia utafutaji au uchimbaji wa madini ndani ya Pori la Akiba, isipokuwa mafuta, gesi asilia na madini ya urani, baada ya kufanyika kwa EIA, kulipwa gharama za ulinzi wa eneo, ada ya leseni, na Serikali kuwa mwanzilishi wa mradi husika," amesema Dkt. Kiruswa.

Pia, ameeleza kuwa, kifungu cha 120 (1)(c) cha Sheria ya Madini, Sura ya 123, kinamtaka mmiliki wa leseni ya madini kupata ridhaa ya maandishi ya mamlaka zinazosimamia Hifadhi ya Misitu, Pori la Akiba, eneo la hifadhi ya malisho au eneo jingine la hifadhi kabla ya kutumia haki zake za madini katika eneo husika.


Share To:

Post A Comment: