Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu (MB) (Mwenye Suti) akisikiliza maelezo ya Huduma zinazopatikana katika banda la Mfuko wa PSSSF katika Maonesho ya Kilimo (Nanenane) Kanda ya Kusini yanayoendelea katika Viwanja vya Ngongo Manispaa ya Lindi Agosti 5, 2026

 

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi Ajira na Mahusiano,  Mh.Deus Sangu (MB) (wanne kushoto),  akipokea zawadi toka kwa Meneja wa PSSSF Kanda ya Kusini, Bw.  Jafari Merai Mgala, alipotembelea banda la Mfuko huo kwenye Maonesho ya Kilimo (Nanenane) Kanda ya Kusini, Viwanja vya Nganga Mkoani Lindi Agosti 5, 2026.

Wananchi wakiwa kwenye banda la Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), wakati Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano Mhe. Deus Sangu, alipokuwa akizungumza kwenye Maonesho ya Kilimo (Nanenane) Kanda ya Kusini kwenye Viwanja vya Ngongo Manispaa ya Lindi Agosti 5, 2026

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu (MB) (Mwenye Suti) akiwasili kwenye Banda la PSSSF ndani ya maonesho ya Kilimo (Nanenane)  yanayoendelea katika Viwanja vya Ngongo Manispaa ya Lindi, Agosti 5, 2026.

Lindi, Agosti 5, 2026


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu, amesema kaulimbiu ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) ya "Tunalipa Jana" si kauli tu, bali inatekelezwa kwa vitendo na imeonyesha ukwasi wa Mfuko huo kupitia ulipaji wa mafao kwa wakati kwa wanachama wanaostaafu.

Mhe. Sangu ameyasema hayo Agosti 5, 2026, alipotembelea banda la PSSSF katika Maonesho ya Kilimo (Nanenane) Kanda ya Kusini yanayoendelea katika Viwanja vya Ngongo, Manispaa ya Lindi, ambapo alizungumza na wanachama, wastaafu na wananchi waliotembelea banda hilo.

"Wastaafu wengine wanashangaa kuona fedha zimeingia kwenye akaunti zao mara tu wanapotoka kazini na kujiuliza, 'Hizi fedha ni zangu kweli?' Hilo linaonesha wazi ukwasi wa Mfuko wa PSSSF na utekelezaji wa kaulimbiu ya Tunalipa Jana," amesema Mhe. Sangu.

Ameongeza kuwa hata wastaafu wanaopokea pensheni za kila mwezi hulipwa ifikapo tarehe 25 ya kila mwezi, na wakati mwingine hupokea malipo yao kabla ya watumishi walio bado kazini kupokea mishahara yao.

"Wastaafu wetu tumewapa kipaumbele. Mafanikio haya yametokana na maboresho makubwa yaliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambayo yameuwezesha Mfuko kuendelea kukua na kutoa huduma bora kwa wanachama na wastaafu," amesisitiza.

Kwa upande wake, Meneja wa PSSSF Kanda ya Kusini, Bw. Jafari Merai Mgala, amesema mafanikio ya utoaji wa huduma kwa haraka na kwa ufanisi yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na maboresho ya mifumo ya TEHAMA.

Amesema kwa sasa mwanachama au mstaafu anaweza kuwasilisha madai ya mafao akiwa mahali popote kupitia simu janja, kompyuta au kifaa kingine chenye uwezo wa kuunganishwa na intaneti, hatua iliyorahisisha upatikanaji wa huduma za Mfuko.

"Natoa wito kwa wanachama na wananchi wote wa Kanda ya Kusini kutembelea banda la PSSSF katika Maonesho ya Nanenane ili kupata elimu kuhusu huduma zetu pamoja na kufahamu fursa mbalimbali zinazotolewa na Mfuko," amesema Bw. Mgala.

Mwisho

Share To:

OSCAR ASSENGA

Post A Comment: