Na; Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Tanzania inatarajiwa kuingiza zaidi ya Sh bilioni 10 kutokana na mauzo ya biashara ya kaboni baada ya Serikali kuidhinisha miradi minne itakayouza tani milioni 4.2 za kaboni katika soko rasmi la kimataifa la biashara ya Kaboni.
Tani milioni 4.2 za kaboni zilizothibitishwa zina thamani ya zaidi ya dola za Marekani milioni 52.1, sawa na takribani Sh bilioni 135.5, huku Serikali ikitarajia kupata zaidi ya dola za Marekani milioni mbili, sawa na zaidi ya Sh bilioni 1
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni ameyasema hayo wakati akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam Agosti 5, 2026 ambapo amebainisha kuwa mapato hayo yanatokana na asilimia nane ambayo Serikali hupata kutokana na mauzo ya kaboni kwa mujibu wa Kanuni za Usimamizi wa Biashara ya Kaboni.
Ameitaja miradi iliyopata kibali ni nishati safi ya kupikia unaotekelezwa na Burn Manufacturing, programu ya athari za kijamii inayosimamiwa na AP Energy Group kwa kushirikiana na Sayari SA Limited, mradi wa maji safi wa Water Mission International Tanzania na mradi wa majiko banifu unaotekelezwa na Bridge Carbon Tanzania Limited. Hivyo kusaidia utekelezaji wa lengo la Serikali la kuhakikisha asilimia 85 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.
Waziri Masauni, amebainisha kuwa miradi ya nishati safi ya kupikia itasambaza Majiko bora zaidi ya 900,000 kwa kaya zaidi ya 600, 000 Vijini na Mijini. Aidha, mradi wa maji utatoa ajira 1000 na utatekelezwa katika mikoa yote nchini, ambapo utatoa ajira za mtu mmoja mmoja na kwa wasambazaji zaidi ya 100.
“Fedha hizi zinatokana na juhudi za Serikali za kujenga mfumo imara wa biashara ya kaboni unaolinda maslahi ya taifa na kuongeza mchango wa sekta hii katika uchumi,” alisema Masauni.







Post A Comment: