Uwekezaji katika miundombinu ya sekta ya nishati unahitaji ushirikiano wa karibu kati ya Serikali, sekta binafsi na taasisi za fedha ili kuhakikisha miradi mikubwa inapata rasilimali zinazohitajika na kutekelezwa kwa ufanisi.

Akizungumza katika Kongamano la Siku ya Nishati (Energy Day) linaloendelea wakati wa Maonesho ya Sabasaba jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Sera na Mipango wa Wizara ya Nishati, Bw. Petro Lyatuu, amesema uwekezaji katika miradi mikubwa ya nishati unahitaji mifumo imara ya ufadhili pamoja na ushirikiano wa wadau mbalimbali.

Bw. Lyatuu amesema miradi ya uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme inahitaji uwekezaji mkubwa wa kifedha ambao hauwezi kutegemea chanzo kimoja pekee, hivyo kuna umuhimu wa kuendelea kuvutia wawekezaji na kushirikiana na taasisi za fedha katika kuwezesha utekelezaji wa miradi hiyo.

Ameeleza kuwa Serikali ina nafasi muhimu katika kuweka mazingira wezeshi, kuandaa sera na mikakati inayosaidia kuvutia uwekezaji, huku taasisi za fedha zikiwa na jukumu la kusaidia upatikanaji wa mitaji kwa ajili ya miradi ya kimkakati ya sekta ya nishati.

Aidha, amesema kwa miradi mikubwa inayohusisha uzalishaji wa umeme, njia za kusafirisha umeme na miundombinu ya usambazaji, kunahitajika rasilimali fedha za kutosha pamoja na ushirikiano wa muda mrefu kati ya Serikali, sekta binafsi na washirika wa maendeleo.

Ameongeza kuwa Tanzania ina fursa kubwa ya kuendeleza sekta ya nishati, hivyo ni muhimu kuimarisha mifumo ya kifedha, kuondoa vikwazo vya uwekezaji na kuhakikisha miradi ya nishati inatekelezwa kwa manufaa ya maendeleo ya Taifa.

Share To:

Post A Comment: