Na: OWM (KAM) – Doha, Qatar
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu, amesema Tanzania na Qatar zimeendelea kushiurikiana kwa karibu katika sekta mbalimbali, ikiwemo masuala ya ajira ambapo tangu nchi hizo ziliposaini makubaliano ya ushirikiano wa ajira mwaka 2018 mafanikio makubwa yameonekana katika kuongezeka kwa fursa za ajira kwa Watanzania.
Aidha, amesema kupitia diplomasia ya uchumi inayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Watanzania wengi wameendelea kunufaika na fursa za ajira katika soko la ajira la nchini Qatar.
Mhe. Sangu amesema hayo leo Julai 7, 2026 jijini Doha, nchini Qatar wakati wa ziara yake ya kikazi iliyolenga kukutana na Waziri wa Kazi wa Qatar Mhe. Dkt. Ali bin Samikh Al Marri ili kuimarisha ushirikiano katika sekta hiyo.
Amesema katika kipindi cha miezi sita iliyopita, kwa kushirikiana na Chama cha Wakala Binafsi wa Ajira, zaidi ya vijana 9,500 wameunganishwa na fursa mbalimbali za ajira ndani na nje ya nchi, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mikakati ya Serikali ya kuongeza ajira zenye tija.
“Vijana wa Kitanzania waliopo nchini Qattar wameendelea kuonesha weledi, uadilifu, bidii na nidhamu kazini, jambo lililoifanya Serikali ya Qatar kuendelea kuamini uwezo wao na kutafuta njia za kupanua zaidi ushirikiano katika sekta ya ajira,” amesema
Kwa upande mwengine, Waziri Sangu amesema katika utekelezaji wa Dira ya 2050 Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano ina jukumu kubwa la kutafuta fursa za jaira kwa ajili ya nguvu kazi ya Tanzania.
Pamoja na hayo amepongeza Serikali ya Qatar kwa maboresho ya sheria za kazi nchini Qatar, ambazo zimeweka adhabu kali dhidi ya waajiri wanaokiuka haki za wafanyakazi.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wakala Binafsi wa Ajira (TRAA), Abdallah Mohamed ameishukuru Serikali kwa namna inavyoendelea kushirikiana nan chi mbalimbali ikiwemo Qatar katika kuongeza wigo wa fursa za ajira kwa vijana wa Kitanzania.
Ameongeza kuwa, Mkataba waliosaini na JUSOUR, utawezesha vijana kuomba ajira hizo moja kwa moja, huku waajiri kutoka Qatar wakiendelea na uratibu wa usaili na kutoa mikataba yenye maslahi bora kwa waajiriwa.
Kupitia ziara hiyo, Mhe. Sangu alishuhudia kusainiwa kwa makubaliano ya ushirikiano kati ya Taasisi ya Serikali ya Qatar inayosimamia huduma za ajira (JUSOUR) na Chama cha Mawakala Binafsi wa Ajira Tanzania.
Alisema makubaliano hayo yatafungua ukurasa mpya wa ajira za kitaalamu ikiwemo madaktari, wahandisi, wataalamu wa TEHAMA pamoja na wahadhiri wenye Shahada za Uzamivu (PhD)
Kadhalika, ujumbe huo pia ulitembelea chuo maalumu cha mafunzo ya wahudumu wa watoto kinachowaandaa wafanyakazi watakaohudumia familia za kifalme (Royal Families) ambapo vijana 77 wa Kitanzania tayari wamepata mafunzo hayo kwa ufadhili wa masomo na kuajiriwa, huku vijana wengine 20 wakitarajiwa kujiunga na mafunzo hayo baada ya kukamilisha taratibu.











Post A Comment: