Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, amewaalika wafanyabiashara wa Ufaransa kuwekeza Tanzania, akisisitiza kuwa mazingira mazuri ya uwekezaji yaliyopo nchini yanatoa fursa kubwa za kukuza biashara, kuzalisha ajira, kuhamisha teknolojia na ujuzi, pamoja na kuharakisha ujenzi wa uchumi wa viwanda wenye manufaa kwa Tanzania na Ufaransa.
Akizungumza Julai 6, 2026, katika Mjadala wa Kibiashara kati ya Tanzania na Ufaransa (Tanzania–France Business Roundtable) uliofanyika katika Ofisi za Ubalozi wa Tanzania jijini Paris, Dkt. Mwigulu alisema ushirikiano wa kiuchumi kati ya sekta binafsi za nchi hizo mbili unafungua ukurasa mpya wa uwekezaji na biashara.
“Leo tumefanya mjadala wa kibiashara na sote tumeshuhudia makubaliano yakisainiwa kati ya Tanzania Private Sector Foundation (TPSF) na International Chamber of Commerce (ICC) ya Ufaransa. Makubaliano haya si mkataba wa kawaida, bali ni daraja litakalotupeleka kwenye mafanikio makubwa ya kiuchumi na kibiashara katika siku zijazo,” alisema.
Aliwahimiza wawekezaji wa Ufaransa kuitumia vyema fursa hiyo ya kipekee, akieleza kuwa maamuzi yatakayofanywa sasa yataweka msingi wa ukuaji wa sekta mbalimbali za uchumi kwa manufaa ya vizazi vijavyo.
“Ninawahimiza wafanyabiashara wa Ufaransa mtumie vyema fursa hii. Wale watakaowekeza Tanzania leo hawatakuwa tu sehemu ya mageuzi ya uchumi wetu, bali watakuwa washirika muhimu katika kujenga moja ya uchumi wenye ushindani mkubwa zaidi barani Afrika,” alisisitiza.
Dkt. Mwigulu alisema Ufaransa ina uzoefu na teknolojia za kiwango cha kimataifa katika sekta za nishati, miundombinu, uhandisi, viwanda, fedha, huduma za afya na ubunifu wa teknolojia, ambazo zinaweza kuchangia kwa kiasi kikubwa katika safari ya Tanzania kuelekea uchumi wa kisasa na wenye ushindani.
Katika Mjadala huo, Mhe. Waziri Mkuu alishuhudia pia utiaji saini wa Hati ya Makubaliano (MoU) kati ya International Chamber of Commerce (ICC) ya Ufaransa na Tanzania Private Sector Foundation (TPSF).
Makubaliano hayo yalisainiwa na Mtendaji Mkuu wa TPSF, Bw. Deo Massawe, pamoja na Naibu Katibu Mkuu wa ICC, Bw. Julia Kassum, yakilenga kuimarisha ushirikiano wa biashara na uwekezaji kati ya sekta binafsi za nchi hizo mbili.
Mjadala huo uliwakutanisha viongozi wa serikali, taasisi za biashara na wawekezaji kutoka Ufaransa wanaowakilisha kampuni zinazojishughulisha na sekta mbalimbali, ikiwemo nishati jadidifu, hususan mifumo ya nishati ya jua na taa za barabarani, usafirishaji, maji, miundombinu, ujenzi, viwanda, mazingira na ufugaji wa viumbe maji, ikiwemo uzalishaji wa mwani wa baharini.
Aidha, kampuni nyingine zilizoshiriki ni watoa huduma za teknolojia ya satelaiti zinazotoa suluhisho bunifu katika utangazaji wa sauti na picha, intaneti ya kasi (broadband), huduma za data, pamoja na mifumo ya mawasiliano kwa sekta za usafiri wa anga na baharini, hatua inayoonesha fursa pana za ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na Ufaransa.






Post A Comment: