Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limekifungia kiwanda cha SAN SHAN na BAI-LY PAPER CO. LTD kwa kukiuka sheria na taratibu za mazingira, hatua iliyochukuliwa baada ya timu ya ukaguzi wa mazingira uliofanyika katika Wilaya ya Mkuranga ukiongozwa na Meneja wa Utekelezaji wa Sheria wa NEMC, Mhandisi Luhuvilo Mwamila.

Akizungumza baada ya ukaguzi huo, Mhandisi  Luhuvilo alisema kiwanda cha SAN SHAN kinachojihusisha na uchakataji wa mafuta machafu (waste oil) kimekuwa kikizalisha moshi mzito na harufu kali kutokana na kukosa mfumo wa kudhibiti hewa chafuzi. 

Aidha, kiwanda hicho kimekuwa kikitiririsha maji taka yenye mafuta machafu kwenye mazingira na kusababisha uchafuzi mkubwa katika maeneo ya jirani.

NEMC imebainisha kuwa kiwanda hicho hakina Cheti cha Tathmini ya Athari kwa Mazingira na Jamii (TAM) na kwamba mwekezaji wake amekuwa akiwazuia wakaguzi kutekeleza majukumu yao ya ukaguzi, hali iliyokwamisha juhudi za kitaalamu za kushauri maboresho ya uzalishaji unaozingatia uhifadhi wa mazingira. 

NEMC pia ilieleza kuwa viongozi wa Halmashauri walishindwa kukikagua kiwanda hicho kutokana na vikwazo vilivyowekwa na uongozi wa kiwanda.

Kwa upande wa kiwanda cha BAI-LY PAPER CO. LTD, kinachozalisha karatasi za chooni (Toilet paper), kimekutwa kikitiririsha maji taka kwenye mazingira na kusababisha uchafuzi unaohatarisha afya za wakazi wa maeneo ya jirani.

Kutokana na changamoto hizo, NEMC ilishirikiana na Jeshi la Polisi kufanikisha ukaguzi wa viwanda hivyo na hatimaye kuvifungia. 

Mhandisi Luhuvilo ametoa rai kwa viwanda vyote nchini kufanya Tathmini ya Athari kwa Mazingira, kuweka mifumo madhubuti ya kudhibiti uchafuzi wa mazingira na kushirikiana na wakaguzi ili kulinda afya za wananchi na mazingira kwa ujumla.
Share To:

OSCAR ASSENGA

Post A Comment: