
Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, akiwasilisha Hotuba ya Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027 leo Mei 22,2026 bungeni Dodoma.
Na.Alex Sonna-DODOMA
Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB) imeweka mikakati kabambe ya kuimarisha utendaji wa Mfumo wa Stakabadhi za Ghala katika mwaka wa fedha 2026/2027, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuongeza ufanisi wa masoko ya mazao na kulinda ubora wa bidhaa nchini.
Akiwasilisha bajeti ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026-2027,bungeni Waziri wa Viwanda na Biashara,Judith Kapinga,amesema kuwa WRRB inalenga kuhakikisha mfumo huo unafanya kazi kwa viwango vya juu zaidi kupitia usimamizi madhubuti wa ubora wa bidhaa zinazoingia na kutoka katika maghala mbalimbali nchini.
Amesema mpango huo, Bodi itaongeza ufuatiliaji wa karibu wa watendaji wa mfumo huo wakiwemo waendesha maghala, wakaguzi pamoja na mameneja dhamana, ili kuhakikisha kunakuwa na uwajibikaji na uzingatiaji wa kanuni zilizowekwa.
"WRRB imejipanga kuendeleza kampeni za elimu kwa umma na uhamasishaji kuhusu matumizi ya Mfumo wa Stakabadhi za Ghala, hatua inayolenga kuongeza uelewa kwa wakulima na wafanyabiashara kuhusu faida za mfumo huo katika uhifadhi na uuzaji wa mazao."amesema Mhe.Kapinga
Vilevile, Bodi hiyo inaendelea na mchakato wa kupata cheti cha ithibati ya ubora wa kimataifa (ISO), hatua inayotarajiwa kuongeza uaminifu wa mfumo huo ndani na nje ya nchi pamoja na kuufanya uwe na ushindani katika masoko ya kikanda na kimataifa.
Serikali inaamini kuwa uboreshaji wa Mfumo wa Stakabadhi za Ghala utaongeza thamani ya mazao ya wakulima, kupunguza upotevu wa mazao baada ya mavuno, na kuimarisha mapato ya wananchi pamoja na pato la taifa kwa ujumla.
WRRB imeeleza kuwa utekelezaji wa mipango hiyo ni sehemu ya juhudi za muda mrefu za kuifanya sekta ya kilimo kuwa na tija zaidi kupitia mifumo ya kisasa ya uhifadhi, usimamizi na uuzaji wa mazao nchini.

Post A Comment: