📌 Vijana maeneo ya mradi wa umeme kwenye vitongoji kupewa kipaumbele kwenye ajira
Bodi ya Nishati Vijijini (REB) imetoa wito kwa wananchi kuwa walinzi wa kwanza wa miundombinu ya miradi ya kufikisha umeme vijijini inayotekelezwa na serikali, huku ikieleza kusikitishwa na matukio ya wizi wa vifaa vya umeme ikiwemo waya za mashine umba (transfoma) katika baadhi ya maeneo.
Wito huo umetolewa leo Mei 11, 2026 Mkoani Manyara na Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini, Mhe. Balozi Meja Jenerali (Mstaafu), Jacob Kingu wakati akihitimisha ziara ya Bodi hiyo katika mikoa ya Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara ya kukagua utekelezaji wa miradi ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ikiwa ni miradi ya nishati safi ya kupikia pamoja na miradi ya kusambaza umeme katika vitongoji.
Balozi Kingu amesema serikali imetumia fedha nyingi kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya umeme, hivyo ni jukumu la kila mwananchi kushiriki kikamilifu katika kulinda miundombinu hiyo dhidi ya vitendo vya hujuma na wizi vinavyoweza kuchelewesha maendeleo ya wananchi.
Katika ziara hiyo mkoani Manyara, Bodi ya REB imefanya kikao na Wakandarasi wanaotekeleza mradi wa kupeleka umeme katika vitongoji ambao ni kampuni ya Sagemcom Energy & Telecom Tanzania pamoja na China Railway Seventh Group.
Awali akitoa taarifa ya utekelezaji wa miradi hiyo, Msimamizi wa Miradi wa REA Mkoa wa Manyara, Mhandisi Geofrey Mkeni, amesema serikali kupitia REA imetenga zaidi ya shilingi bilioni 45.8 kwa ajili ya miradi ya kusambaza umeme katika vitongoji 267 vya mkoa wa Manyara.
Mhandisi Mkeni amesema miradi hiyo inalenga kuongeza upatikanaji wa huduma ya umeme kwa wananchi wa vijijini ili kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Pia ametoa wito kwa wananchi wanaoishi katika maeneo yanayofikiwa na miradi hiyo kuanza kufanya maandalizi ya miundombinu ya ndani ya nyumba ikiwemo wiring ili wawe tayari kuunganishiwa huduma ya umeme mara baada ya miradi hiyo kukamilika.
Kwa upande wao, wakandarasi wanaotekeleza miradi hiyo wameahidi kuhakikisha kazi zinakamilika kwa wakati huku wananchi wakinufaika kupitia ajira zinazotokana na utekelezaji wa miradi hiyo.
Akizungumza kwa niaba ya kampuni ya Sagemcom Energy & Telecom Tanzania, Afisa Mahusiano ya Jamii na Mazingira, Oliver Charles, amesema miradi hiyo imefungua fursa mbalimbali za ajira kwa vijana wanaoishi katika maeneo yenye miradi ili wawe sehemu ya maendeleo yanayoletwa na serikali.
Naye Mhandisi wa Miradi kutoka kampuni ya China Railway Seventh Group, Estheria Fumbuka, amesema kampuni hiyo itaendelea kufanya kazi kwa bidii kuhakikisha miradi yote inakamilika kwa wakati ili malengo ya serikali ya kuwafikishia wananchi huduma ya umeme vijijini yaweze kutimia.


Post A Comment: