Serikali kupitia Bohari ya Dawa (MSD) itaendelea kununua dawa zinazozalishwa na wawekezaji wa ndani ili kuimarisha uzalishaji wa ndani wa bidhaa za afya na kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje ya nchi.
Hayo yamesemwa Waziri wa Afya, Mohammed Mchengerwa leo Mei 11 2026 akiwasilisha Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Afya kwa mwaka wa fedha 2026/27 Bungeni, Jijini Dodoma.
“Serikali imejipanga kuhakikisha MSD inanunua kwanza dawa zinazozalishwa ndani ya nchi zilizokidhi viwango vya Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) kabla ya kwenda kununua kutoka nje ya nchi, hatua inalenga kukuza viwanda vya ndani, kuongeza ajira na kuimarisha uchumi wa Taifa” amesema Waziri Mchengerwa
Amesema Serikali itaendelea kuweka mazingira rafiki na wezeshi kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi, ikiwemo kuboresha upatikanaji wa ardhi, miundombinu muhimu pamoja na kuratibu uwekezaji katika sekta ya dawa na bidhaa za afya ili kuvutia uwekezaji zaidi nchini.
Waziri Mchengerwa amesema Serikali imeendelea kuimarisha upatikanaji wa bidhaa za afya nchini kwa kutoa Shilingi trilioni 1.4 kupitia MSD ili kuhakikisha wananchi wanapata dawa na bidhaa muhimu za afya kwa wakati.
“Upatikanaji wa bidhaa muhimu za afya umeongezeka kutoka asilimia 58 mwaka 2021/22 hadi asilimia 88 mwezi Machi 2026” amesema Waziri Mchengerwa.
Amesema kuwa Wizara ya Afya itaendelea kuhamasisha wawekezaji wa ndani na nje ya nchi pamoja na kuwawekea mazingira rafiki na wezeshi, ikiwemo upatikanaji wa ardhi na miundombinu muhimu, ili kuwavutia kuwekeza katika ujenzi wa viwanda vya bidhaa za afya na kupunguza utegemezi.
Waziri Mchengerwa amesisitiza kuwa dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma bora za afya, dawa salama na huduma zenye ubora bila kuachwa nyuma.

Post A Comment: