Katibu Wakuu wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Wizara za Fedha, Afya na Maji, wamekutana jijini Dodoma mahsusi kuhusu utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba kuhakikisha huduma ya majisafi na salama inafika katika shule na vituo vya afya nchini.

Hatua hiyo inafanyika ikiwa ni maandalizi ya Mpango wa Kuboresha Huduma za Maji, Usafi wa Mazingira na Usafi wa Mtu Binafsi (Presidential WASH Compact).

Mpango unalenga kuhakikisha huduma za majisafi, usafi wa mazingira na usafi wa mtu binafsi zinapatikana kwa uhakika, usawa na ubora nchini ifikapo 2030.

WASH Compact ni mkataba unaobeba ahadi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, unaolenga kuimarisha usalama wa maji na utoaji endelevu wa huduma za maji, usafi wa mazingira na usafi wa mtu binafsi. 

Mkataba huo unaainisha matokeo yanayotarajiwa, mageuzi ya kisekta, uwekezaji unaohitajika pamoja na misingi ya uwajibikaji.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri akiongoza kikao amesema lengo kuu la kikao hicho ni kujenga uelewa wa pamoja miongoni mwa sekta mtambuka zinazotekeleza WASH kabla ya kuanza rasmi kwa utekelezaji.

“Ni muhimu kwa sekta zote kushirikiana na kuwa na uelewa wa pamoja ili kuhakikisha mpango huu unatekelezwa kwa ufanisi na kuleta matokeo chanya,” Mhandisi Mwajuma amesema.

Ameongeza, licha ya Sekta ya Maji kuwa mhimili muhimu wa maendeleo, mafanikio ya mpango huo yanategemea ushirikiano madhubuti kati ya sekta zote husika.

Kikao kimewahusisha wataalamu kutoka wizara mbalimbali pamoja na wataalamu washauri wa mpango huo, ambao wamesisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano wa kisekta ili kufanikisha utekelezaji wake.

Miongoni mwa mambo yaliyojadiliwa ni pamoja na kuongeza uwekezaji katika miundombinu ya huduma ya maji, hususan maeneo ya vijijini na yenye uhitaji mkubwa, pamoja na kuimarisha matumizi ya mifumo ya kidigitali katika utoaji wa huduma.

Viongozi hao wamejadili mbinu za kuhakikisha upatikanaji endelevu wa rasilimali fedha, ikiwemo ushirikishwaji wa sekta binafsi na washirika wa maendeleo katika utekelezaji wa mpango huo.

Mpango katika utekelezaji utajikita katika nguzo kuu tatu ; kuongeza upatikanaji wa huduma za WASH katika maeneo mbalimbali kama kaya, shule na vituo vya afya, kuimarisha mifumo ya utoaji huduma pamoja na kuboresha mbinu za upatikanaji wa rasilimali fedha.

Mpango wa WASH Compact ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuharakisha maendeleo ya jamii na uchumi, ukitarajiwa kuleta mageuzi makubwa katika ustawi wa maisha ya wananchi.














Share To:

Post A Comment: