RAIS SAMIA AAGIZA VIJANA WANUFAIKE NA FURSA ZA UCHUMI WA KIDIJITALI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameiagiza Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana kuhakikisha vijana wananufaika kikamilifu na fursa zitokanazo na ukuaji wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).
Akizungumza leo Ijumaa Aprili 10, 2026 katika ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention Centre jijini Dodoma, mara baada ya kuzindua minara 758 ya mawasiliano pamoja na maunganisho ya mkongo wa taifa katika wilaya 85, Rais Samia amesema hatua hiyo ni muhimu katika kukuza ajira na ubunifu kwa vijana.
Amesema serikali inapaswa kuhakikisha miundombinu ya mawasiliano iliyopo inatumika ipasavyo kuwawezesha vijana kuongeza ujuzi wa kidijitali na kushiriki katika shughuli za kiuchumi.
“Ni muhimu kuhakikisha vijana wetu wanapata fursa za kunufaika na uchumi wa kidijitali kupitia ubunifu, ajira na matumizi sahihi ya teknolojia,” alisema.
Rais Samia pia amesisitiza umuhimu wa kuwezesha kampuni changa (start-up) zinazomilikiwa na vijana kwa kuwapatia mitaji ili ziweze kukua na kuongeza ushindani katika soko la ajira na biashara.
Aidha, amewataka wadau wa sekta binafsi kushirikiana na serikali katika kukuza ubunifu na uwekezaji katika TEHAMA, akieleza kuwa vijana ndio chachu ya maendeleo ya uchumi wa kisasa unaotegemea maarifa na teknolojia.
Katika hatua nyingine, Rais Samia ameelekeza kulindwa kwa miundombinu ya mkongo wa taifa wa mawasiliano ili kuhakikisha inaendelea kutoa manufaa yaliyokusudiwa kwa taifa.
Amesisitiza kuwa, utekelezaji wa maagizo hayo utasaidia kuhakikisha hakuna kijana anayebaki nyuma katika safari ya kuelekea uchumi wa kidijitali na jumuishi nchini.

Post A Comment: