Na Oscar Assenga,Muheza, Tanga

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais anayeshughulikia Maendeleo ya Vijana, Joel Nanauka amesema serikali itaendelea kuvipa kipaumbele vikundi vya vijana vinavyoonyesha uwajibikaji kwa kurejesha mikopo wanayopewa ili viweze kukuza shughuli zao za kiuchumi.

Nanauka aliyasema hayo leo wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii iliyotembelea kikundi cha Vijana cha Mali Hai kilichopo wilayani Muheza mkoani Tanga kwa lengo la kukagua shughuli zao za uzalishaji pamoja na miradi iliyopata fedha kupitia mikopo ya halmashauri.

Akiwa kwenye kikundi hicho alionyesha kuridhishwa na juhudi na nidhamu ya kikundio hicho kurejesha mikopo baada ya kufanikiwa kukuza mtaji wake kutoka shilingi milioni 20 hadi kufikia zaidi ya shilingi milioni 50, hatua inayotajwa kuwa mfano bora kwa vikundi vingine vya vijana nchini.

Nanauka alisema kikundi cha Mali Hali ni miongoni mwa vikundi vichache nchini vilivyofanikiwa kurejesha mikopo kwa wakati, jambo ambalo limekifanya kupata nafasi ya kuangaliwa kwa karibu zaidi katika mipango ya kusaidiwa kuongeza mtaji na kupanua shughuli zake.

Alisema katika mchakato unaoendelea wa kusaidia wajasiriamali wadogo na kurasimisha shughuli zao, serikali itaangalia namna ya kukiweka kikundi hicho kwenye orodha ya vikundi vitakavyosaidiwa ili kuimarisha shughuli zao za uzalishaji.

Aidha, alieleza kuwa serikali inatekeleza maelekezo ya Rais ya kuhakikisha vijana wanaochukua hatua ya kufanya kazi na kuonyesha juhudi wanapatiwa mikopo na serikali ili waweze kujikwamua kiuchumi na pia kutoa ajira kwa wengine.

“Vijana hawa wameonyesha mfano mzuri kwa watanzania wengine wameanza na mtaji mdogo mwaka 2008,wakapata msaada wa shilingi milioni tano mwaka 2018 na baadaye mkopo wa shilingi milioni 20 mwaka wa fedha 2020/2021. Leo hii wameongeza mtaji wao hadi kufikia zaidi ya milioni 50. Huu ni ushahidi kwamba ndoto kubwa zinaweza kuanza na mwanzo mdogo,” alisema Nanauka.

Aliongeza kuwa serikali itahakikisha vijana wenye juhudi kama hao wanapata fursa zaidi, ikiwemo mikopo mingine, pamoja na kushirikishwa katika zabuni za serikali ili waweze kukuza biashara zao.

Nanauka pia aliwashauri vijana nchini kutokudharau mwanzo mdogo na kuwa na uvumilivu wanapotekeleza ndoto zao za kimaendeleo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii, Hawa Mchafu, alisema kamati hiyo ipo katika ziara ya kawaida ya kukagua miradi ya maendeleo kabla ya kuanza kwa Bunge la Bajeti, ambapo wamepita katika maeneo mbalimbali kutathmini miradi iliyopata fedha za serikali.

Alisema kamati hiyo imevutiwa na kazi nzuri inayofanywa na kikundi hicho cha vijana, lakini imebaini changamoto ya eneo la uzalishaji kuwa dogo na huenda lisiweze kukidhi mahitaji yao iwapo wataongeza mtaji zaidi.

Kutokana na hali hiyo, kamati imeitaka wizara husika kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga kuhakikisha vijana hao wanapatiwa eneo kubwa zaidi la kufanyia shughuli zao za uzalishaji ili waweze kupanua biashara zao.

“Eneo walilonalo sasa ni dogo ukilinganisha na malengo yao ya kupanua uzalishaji hivyo tunashauri wapatiwe eneo kubwa zaidi na lililopo sasa likibaki kama sehemu ya maonesho ya bidhaa wanazozalisha,” alisema Mchafu.

Pia aliishauri serikali kuangalia uwezekano wa kukipa kikundi hicho mkopo mwingine wa kifedha ili kiweze kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazokikabili, ikiwemo kununua gari kwa ajili ya shughuli za uzalishaji na usafirishaji wa bidhaa.

Aidha, alitumia nafasi hiyo kuwakumbusha vijana nchini kutumia fursa zilizotolewa na serikali kupitia mifuko mbalimbali ya maendeleo ya vijana badala ya kujikita kwenye mfuko mmoja pekee.

Mchafu alisema kuwa Rais ametoa zaidi ya shilingi bilioni 200 kwa ajili ya kusaidia maendeleo ya vijana kupitia wizara na taasisi mbalimbali, hivyo vijana wanapaswa kuzitumia fursa hizo kujikwamua kiuchumi.

Kamati hiyo pia imeishauri serikali kuhakikisha sheria ya manunuzi ya umma inayotaka asilimia 30 ya zabuni za serikali zitolewe kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu inatekelezwa kikamilifu ili kuwapatia vijana nafasi ya kukua kiuchumi.

Kwa sasa kikundi cha Mali Hali kinadaiwa kuajiri vijana zaidi ya 20 katika shughuli zake za uzalishaji, jambo ambalo limeelezwa kuwa linaunga mkono dhamira ya serikali ya kukuza ajira kwa vijana na kuimarisha uchumi wa wananchi.

Vijana wa kikundi hicho pia wamemshukuru Rais kwa kuendelea kutoa fursa na kuahidi kuendelea kufanya kazi kwa bidii ili kufikia ndoto zao za kuanzisha kampuni kubwa inayoweza kutoa ajira kwa vijana wengi zaidi katika Mkoa wa Tanga na maeneo mengine nchini.

Mwisho.

Share To:
Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

OSCAR ASSENGA

Post A Comment: