Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya, Mkoa wa Dodoma limewasikiliza wananchi wa jamii ya Kiiraqw waliofika katika Baraza hilo kuwasilisha hoja na ushahidi wao katika mgogoro wa ardhi, wakidai kumiliki kihalali shamba lenye ukubwa wa ekari nane lililopo Wilaya ya Chamwino, Mkoa wa Dodoma.
Hatua hiyo imekuja kufuatia maombi ya wadaawa hao ambao ni pande mbili zinazohusika katika shauri hilo, kubainisha kuwa wanakabiliwa na changamoto ya lugha, hali iliyokuwa ikiathiri uwezo wao wa kujitetea na kueleza kwa uwazi hoja zao mbele ya Mwenyekiti wa Baraza hilo, Mhe. Omary Mbega.
Kutokana na hilo, Baraza lilitoa huduma ya ukalimani kupitia mkalimani, Ndg. Simon Tlatlaa Emmay, ambaye alitafsiri maelezo yao na kuwawezesha wadaawa hao kufafanua kwa kina madai yao, kuwasilisha ushahidi pamoja na vielelezo muhimu bila kikwazo cha lugha.
Shauri hilo ni Shauri la Ardhi Na. 92 la mwaka 2025, linalomhusu Ekaristi Ngu’nda kama Mleta Maombi dhidi ya Lolote Nanacha na Martin Lolo Nanacha, ambao ni Wajibu Maombi. Mgogoro huo unahusu umiliki wa shamba lenye ukubwa wa ekari nane lililopo Kitongoji cha Msunjirire, Kijiji cha Zajilwa, Kata ya Zajilwa, Wilaya ya Chamwino, Mkoa wa Dodoma.
Katika madai yake, Mleta Maombi anadai kuwa ndiye mmiliki halali wa eneo hilo la ardhi, akieleza kuwa ekari hizo ziliuzwa na Wajibu Maombi kwa utaratibu unaozua mgogoro wa kisheria.
Akizungumza mara baada ya kusikilizwa kwa shauri hilo, mmoja wa Wajibu Maombi, Ndg. Lolo Nanacha, alisema uwepo wa mkalimani umeimarisha imani yake katika mfumo wa utoaji haki.
“Leo nimejisikia huru kueleza ukweli wangu. Nimeeleweka vizuri, na ninaamini haki itatendeka,” alisema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza hilo, Mhe. Omary Mbega, alisisitiza kuwa huduma ya ukalimani ni sehemu muhimu ya kuhakikisha kila mwananchi anapata haki sawa bila kujali tofauti ya lugha au asili yake.
Shauri hilo limeahirishwa hadi tarehe 15 Aprili 2026, ambapo mashahidi zaidi watasikilizwa kabla ya kutolewa uamuzi wa mwisho.




Post A Comment: