📌Aipongeza TPDC kwa ujenzi wa vituo vya CNG; utekelezaji wa ajenda ya nishati safi ya kupikia
📌Asisitiza kuhusu ushirikishwaji kamilifu wa wazawa katika miradi
Watendaji katika Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) wametakiwa kutekeleza kwa vitendo maelekezo ya Viongozi Wakuu wa Kitaifa yanayolenga kuendeleza sekta ya mafuta na gesi asilia, ikiwemo agizo la kuhakikisha mazungumzo ya Mradi wa Kuchakata Gesi kuwa Kimiminika (LNG) yanakamilika kwa wakati ili utekelezaji wake uanze.
Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba, amesema hayo tarehe 20 Februari, 2026 jijini Mwanza wakati akifunga kikao kazi cha menejimenti ya TPDC kilicholenga kujadili mipango na bajeti ya Shirika kwa mwaka 2026/2027 pamoja na kufanya tathmini ya utendaji kazi wa Shirika.
“Maelekezo mengine yaliyotolewa ni pamoja na kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2030 ujenzi wa Bomba la Kusafirisha Gesi Asilia kutoka Kinyerezi hadi Chalinze unakamilika, pamoja na kuharakisha ujenzi wa vituo vya Gesi Asilia Iliyoshindiliwa (CNG) katika mikoa ya Morogoro na Dodoma. Haya ni maelekezo ya kimkakati yanayohitaji mshikamano, umakini na kasi ya utekelezaji kutoka TPDC na wadau wake, na utekelezaji wa maelekezo haya utafanyiwa tathmini,” amesema Mhe. Salome.
Aidha, Mhe. Salome amelitaka Shirika hilo kuhakikisha kunakuwa na upatikanaji wa mafuta ya kutosha, ikiwemo kwa kujenga miundombinu ya hifadhi ya mafuta, kuimarisha shughuli za utafutaji, uzalishaji na usambazaji wa gesi asilia viwandani, kwenye taasisi, majumbani na kwenye magari, pamoja na kukamilisha miradi ya kimkakati ukiwemo wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP).
Kuhusu utekelezaji wa Ajenda ya Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia, Mhe. Salome amepongeza jitihada za TPDC katika miradi ya usambazaji wa gesi asilia kama nishati safi ya kupikia katika mikoa ya Mtwara, Lindi, Pwani na Dar es Salaam, na kulitaka Shirika hilo kuongeza kasi ili kufikia mikoa mingine.
Vilevile ameipongeza TPDC kwa mchango wake katika kuchochea matumizi ya CNG na hivyo kupunguza foleni katika vituo vya kujaza gesi kwenye magari. Amesema juhudi za TPDC pia zimeonekana kupitia ujenzi wa kituo mama cha CNG katika Barabara ya Sam Nujoma, Dar es Salaam, ambacho kinaendelea kuchochea wawekezaji binafsi kuanzisha vituo vyao kutokana na uhakika wa upatikanaji wa gesi. Pia amepongeza utoaji wa idhini kwa kampuni binafsi kuwekeza katika biashara ya CNG.
Katika hatua nyingine, TPDC pia imetakiwa kutokubaki nyuma katika matumizi ya teknolojia na mageuzi ya kidijitali, ikiwemo matumizi ya Akili Mnemba (Artificial Intelligence – AI), mifumo ya kidijitali na uchambuzi wa takwimu kwani Serikali inatarajia TPDC ijipambanue kidijitali ili kurahisisha utoaji wa huduma, kupunguza urasimu, kuongeza uwazi katika manunuzi, kupunguza gharama za uendeshaji na kuongeza faida.
“Jambo jingine kubwa kwenu TPDC, mnapaswa wakati wote mjiridhishe kuhusu ushirikishwaji wa wazawa kwa kuhakiki uhalali wa kampuni za wazawa, si kwa usajili tu hapa nchini bali kwa uhalisia wa umiliki wa kampuni hizo. Nasisitiza pia umuhimu wa uwajibikaji kwa jamii (CSR), kwani miradi ya mafuta na gesi inapaswa kuleta manufaa yanayoonekana kwa jamii zinazozunguka maeneo ya miradi. Tayari mmeanza kufanya vizuri katika eneo hili, lakini mnapaswa kuongeza juhudi,” amesema Mhe. Salome.
Naye, mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati (Mafuta na Gesi Asilia), Mhandisi Antelimi Raphael ameipongeza TPDC kwa kikao hicho cha kujitathmini, akisema ni hatua muhimu katika kuendeleza Shirika.
Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Mussa Makame, alisema kikao hicho kililenga kujadili mipango na bajeti ya Shirika kwa mwaka 2026/2027. Pia kililenga kufanya tathmini ya utendaji kazi ili kubaini changamoto na kuzitatua, hivyo kuiwezesha miradi kuendelea kwa kasi iliyokusudiwa.
Kikao hicho pia kilienda sambamba na mafunzo mbalimbali ikiwemo ya uongozi.










Post A Comment: