Na OWM – TAMISEMI, Dar es Salaam
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM-TAMISEMI), Mhe. Prof. Riziki Shemdoe amekutana na Wakuu wa Mikoa wapya wa Mkoa wa Kagera na Mtwara, Mhe. Kanali Yahya Ramadhani Kido na Mhe. Kanali Donald Wiliam Msengi ili kujipanga kiutendaji katika kutekeleza maelekezo ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyoyatoa ili kuimarisha ufanisi na uwajibikaji katika kuwatumikia wananchi.
Prof. Shemdoe amekutana na Wakuu hao leo Februari 09, 2026 katika Ofisi Ndogo ya TAMISEMI Jijini Dar es Salaam, mara baada ya viongozi hao kuapishwa na Mhe. Rais katika Ikulu ya Magogoni, ambapo Mhe. Rais amewataka viongozi hao kwenda kuimarisha uwajibikaji ili kukidhi matarajio ya wananchi hususani kwenye eneo la upatikanaji wa huduma za kijamii pamoja na ulinzi na usalama wa wananchi na mali zao.
Katika kuhakikisha viongozi hao wanatekeleza maelekezo ya Mhe. Rais kwa ufanisi, Prof. Shemdoe amewataka kuhakikisha, wanakwenda kuandikisha wakazi wote kwenye daftari la makazi, pamoja na kusikikiliza na kutatua kero za wananchi kwa kushirikiana na viongozi na watumishi waliopo katika maeneo yao mapya ya Utawala.
Kikao kazi hicho cha Prof. Shemdoe na Wakuu wa hao ni hatua ya awali ya kujipanga na utekelezaji wa maelekezo ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyoyatoa leo, wakati wa uapisho wa viongozi aliowateua Februari 06, 2026 kwa lengo la kuleta mabadiliko yatakayo imarisha ufanisi na uwajibikaji ili kuendana na kasi ya mahitaji ya wananchi.

Post A Comment: